M’Cheyne Bible Reading Plan
Gavana Pilato Amhoji Yesu
(Mt 27:1-2,11-14; Lk 23:1-5; Yh 18:28-38)
15 Asubuhi na mapema, Mara tu ilipofika asubuhi viongozi wa makuhani, viongozi wazee wa Kiyahudi, walimu wa sheria, na baraza kuu lote la Wayahudi liliamua jambo la kufanya kwa Yesu. Walimfunga Yesu, wakamwondoa pale, na wakamkabidhi kwa Pilato.
2 Na Pilato akamwuliza: “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu “Hayo ni maneno yako mwenyewe.”
3 Na viongozi wa makuhani wakamshitaki Yesu kwa mambo mengi. 4 Kwa hiyo Pilato akamwuliza Yesu swali lingine. Akasema, “Wewe hata kujibu hujibu? Angalia una mashitaka mengi wanayokuletea!”
5 Lakini Yesu hakujibu kitu chochote, na Pilato akastaajabu.
Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu
(Mt 27:15-31; Lk 23:13-25; Yh 18:39-19:16)
6 Kila mwaka wakati wa Sherehe ya Pasaka Pilato atamweka huru mfungwa mmoja atakayechaguliwa na watu. 7 Mtu mmoja aliyeitwa Baraba alikuwa gerezani amefungwa pamoja na waasi. Watu hawa walifanya mauaji wakati wa fujo.
8 Watu walikuja Kwa Pilato na kumwomba amweke huru mfungwa kama alivyofanya siku zote. 9 Yeye akawauliza, “Je, mnataka nimwache huru mfalme wa Wayahudi?” 10 Pilato alilisema hili kwa sababu alijua kuwa viongozi wa makuhani walimleta kwake kwa ajili ya wivu tu. 11 Lakini wale viongozi wa makuhani walimchochea amwache Baraba badala ya Yesu.
12 Lakini Pilato akawauliza watu tena, “Kwa hiyo nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”
13 Wakapiga kelele “Muue kwenye msalaba.”
14 Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini? Je, amefanya kosa gani?”
Lakini wote wakapiga kelele zaidi, “Muue kwenye msalaba!”
15 Pilato alitaka kuwaridhisha watu, kwa hiyo alimweka huru Baraba kwa ajili yao. Akaamuru maaskari wampige Yesu viboko na kisha akamtoa kwao ili akauawe kwenye msalaba.
16 Maaskari wakamwongoza Yesu hadi ndani ya baraza la jumba la gavana (lililojulikana kama Praitorio). Huko wakakiita pamoja kikosi cha maaskari. 17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau na wakafuma taji ya miiba na kumvisha kichwani. 18 Kisha wakaanza kumpigia saluti wakisema: “Heshima kwa Mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga tena na tena kichwani kwa fimbo na wakamtemea mate. Kisha wakapiga magoti mbele yake na kujifanya wanampa heshima kama mfalme. 20 Walipomaliza kumkejeli walimvua joho lile la kizambarau, na kumvisha mavazi yake mwenyewe. Baada ya hapo wakamtoa nje ili waweze kumsulubisha.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mt 27:32-44; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)
21 Wakiwa njiani walikutana na mtu kutoka Kirenio aliyeitwa Simoni, akitoka vijijini kuja mjini. Yeye alikuwa baba yake Iskanda na Rufo. Wale wanajeshi wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 22 Wakamleta Yesu hadi mahali palipoitwa Golgotha (Yaani Mahali pa Fuvu la Kichwa) 23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na siki, lakini yeye alikataa kuinywa. 24 Pale wakampigilia kwa misumari msalabani. Wakagawana mavazi yake miongoni mwao nao wakayapigia kura ili kuona kila mtu atapata nini.
25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipompigilia kwa misumari msalabani. 26 Ilani ya mashtaka dhidi yake ilikuwa na maandishi haya juu yake: “Mfalme wa Wayahudi.” 27 Hapo waliwapigilia msalabani wahalifu wawili pembeni mwa Yesu, mmoja kushoto kwake na mwingine kuume kwake. 28 [a]
29 Watu waliopita mahali pale walimtukana. Walitikisa vichwa vyao na kusema, “Haya! Wewe ndiye yule awezaye kuliharibu hekalu na kulijenga tena kwa siku tatu. 30 Hebu shuka msalabani na uyaokoe maisha yako.”
31 Kwa njia hiyo hiyo, viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria walimfanyia dhihaka na wakasema wao kwa wao, “Aliwaokoa wengine lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 Ikiwa yeye kweli ni Masihi Mfalme wa Israeli, iinampasa ashuke sasa toka msalabani, tukiliona hilo nasi tutamwamini.” Wale wahalifu waliokuwa katika misalaba ile mingine pembeni waliosulubiwa pamoja naye nao walimtukana.
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)
33 Ilipofika saa sita mchana giza ilifunika nchi yote. Giza liliendelea hadi saa tisa. 34 Mnamo saa tisa Yesu alipiga kelele kwa sauti na kusema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”(A)
35 Na baadhi ya wale waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hivi, walisema, “sikilizeni anamwita Eliya.”[b]
36 Mtu mmoja alikimbia na kujaza sifongo kwenye siki, akaliweka kwenye ufito, na akampa Yesu anywe akisema, “Subiri! Tuone ikiwa Eliya atashuka na kumshusha chini.”
37 Yesu akalia kwa sauti kubwa na kisha akafa.
38 Hapo pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini. 39 Yule afisa wa jeshi aliyekuwa amesimama pale mbele na kuona jinsi Yesu alivyokufa. Afisa huyu alisema, “mtu huyu hakika alikuwa mwana wa Mungu!”
40 Baadhi ya wanawake walikuwa wakiangalia mambo haya toka mbali. Miongoni mwao alikuwapo Maria Magdalena, Salome, na Maria mama yake Yakobo na Yose. 41 Wanawake hawa ni wale waliomfuata Yesu huko Galilaya na kumhudumia. Wanawake wengi wengine waliofuatana naye kuja Yerusalemu walikuwapo pale pia.
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)
42 Siku hii ilikuwa ni Siku ya Maandalizi ya Sabato. (Maana yake siku kabla ya Siku ya Sabato.) Jua lilikuwa bado halijazama. 43 Yusufu wa Arimathea alifika. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Kiyahudi aliyeheshimiwa, ambaye pia alikuwa anautazamia ufalme wa Mungu unaokuja. Kwa ujasiri mkubwa aliingia kwa Pilato na kuuomba mwili wa Yesu.
44 Pilato alishangaa Yesu angekuwa amekufa kwa haraka namna hii, hivyo alimwita yule akida na kumwuliza kama Yesu alikuwa tayari amekufa. 45 Aliposikia taarifa kutoka kwa yule afisa wa jeshi, ndipo alipoutoa mwili wa Yesu na kumpa Yusufu wa Arimathea.
46 Hivyo Yusufu alinunua mavazi kadhaa ya hariri, na akamshusha Yesu toka msalabani, akauzungushia mwili wake na hariri hiyo, na kumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika mwamba. Kisha alivingirisha jiwe kubwa na kuliweka mlangoni mwa kaburi. 47 Mariamu Magdalena na Maria mama yake Yose aliona pale alipolazwa Yesu.
15 Baadhi yetu hatuna matatizo na mambo haya. Hivyo tunapaswa kuwa wastahimilivu kwa wale wasio imara na wenye mashaka. Hatupaswi kufanya yanayotupendeza sisi 2 bali tufanye yale yanayowapendeza wao na kwa faida yao. Tufanye chochote kinachoweza kumsaidia kila mtu kujengeka katika imani. 3 Hata Kristo hakuishi ili kijaribu kujifurahisha yeye mwenyewe. Kama Maandiko yanavyosema, “Matusi ambayo watu waliyatoa dhidi yako pia yalinifanya niteseke.”(A) 4 Chochote kilichoandikwa zamani kiliandikwa ili kitufundishe sisi. Maandiko haya yaliandikwa ili yatupe matumaini yanayokuja kwa njia ya subira na kutia moyo kunakoletwa nayo. 5 Subira na kuhimiza kote hutoka kwa Mungu. Na ninawaombea ili Mungu awasaidie muwe na nia ile ile ninyi kwa ninyi, kama ilivyo nia ya Kristo Yesu. 6 Kisha ninyi nyote, kwa sauti moja, mtamtukuza Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. 7 Kristo aliwakaribisha ninyi, hivyo nanyi mkaribishane ninyi kwa ninyi. Hili litaleta heshima[a] kwa Mungu. 8 Ndiyo, haya ndiyo maneno yangu kwenu kwamba Kristo alifanyika mtumishi wa Wayahudi ili kuonesha kuwa Mungu amefanya yale aliyowaahidi baba zao wakuu. 9 Na pia alifanya hivi ili wale wasio Wayahudi waweze kumsifu Mungu kwa rehema anazowapa. Maandiko yanasema,
“Hivyo nitakushukuru wewe katikati ya watu wa mataifa mengine;
Nitaliimbia sifa jina lako.”(B)
10 Na Maandiko yanasema,
“Ninyi watu wa mataifa mengine furahini pamoja na watu wa Mungu.”(C)
11 Pia Maandiko yanasema,
“Msifuni Bwana ninyi watu wote wa mataifa mengine;
watu wote na wamsifu Bwana.”(D)
12 Na Isaya anasema,
“Mtu mmoja atakuja kutoka katika ukoo wa Yese.[b]
Atainuka na kutawala juu ya mataifa,
na wataweka matumaini yao kwake.”(E)
13 Naomba kwamba Mungu aletaye matumaini awajaze furaha na amani kadri mnavyomwamini yeye. Na hii isababishe tumaini lenu liongezeke hadi lifurike kabisa ndani yenu kwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Paulo Azungumzia Kazi Yake
14 Kaka na dada zangu, najua pasipo mashaka kuwa mmejaa wema na mnayo maarifa yote mnayohitaji. Hivyo kwa hakika mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi. 15 Lakini nimewaandikia ninyi kwa ujasiri wote kuhusu mambo fulani niliyotaka mkumbuke. Nilifanya hivi kwa sababu Mungu alinipa karama hii maalumu: 16 kuwa mtumishi wa Kristo Yesu kwa ajili ya wasio Wayahudi. Natumika kama kuhani ambaye kazi yake ni kuhubiri Habari Njema kutoka kwa Mungu. Alinipa mimi jukumu hili ili ninyi msio Wayahudi mweze kuwa sadaka atakayoikubali, sadaka iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Na hii ndiyo sababu najisikia vizuri kuhusu yale yote yaliyofanyika kwa ajili ya Mungu kwa kuwa mimi ni mali ya Kristo Yesu. 18 Sitazungumzia chochote nilichofanya mwenyewe. Nitazungumza tu kuhusu yale Kristo aliyofanya akinitumia mimi katika kuwaongoza wale wasiokuwa Wayahudi katika kutii. Ni yeye aliyetenda kazi katika yale niliyosema na kufanya. 19 Alitenda kazi kwa ishara za miujiza kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Matokeo yake ni kuwa nimewahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo kuanzia Yerusalemu na kuzunguka kote mpaka Iliriko. Na hivyo nimemaliza sehemu hiyo ya wajibu wangu. 20 Imekuwa shabaha yangu daima kuzihubiri Habari Njema katika sehemu ambako watu hawajawahi kusikia juu ya Kristo. Nafanya hivi kwa sababu sitaki kujenga katika kazi ambayo tayari mtu mwingine amekwisha kuianza. 21 Kama Maandiko yanavyosema,
“Wale ambao hawakuambiwa kuhusu yeye wataona,
na wale ambao hawajasikia juu yake wataelewa.”(F)
Mpango wa Paulo Kwenda Rumi
22 Kazi hiyo imenifanya niwe na shughuli nyingi sana na mara nyingi imenizuia kuja kuwaona.
23 Kwa miaka mingi nimetamani kuwatembelea, na sasa nimekamilisha kazi yangu katika maeneo haya. 24 Hivyo nitawatembelea nitakapoenda Hispania. Ndiyo, napanga kusafiri kwenda Hispania na natumaini kuwatembelea nikiwa njiani. Nitakaa kwa muda na kufurahi pamoja nanyi. Kisha natumaini mtanisaidia kuendelea na safari yangu.
25 Sasa ninakwenda Yerusalemu kuwasaidia watu wa Mungu huko. 26 Baadhi yao ni maskini, na waamini kule Makedonia na Akaya walitaka kuwasaidia. Hivyo walikusanya kiasi cha fedha ili wawatumie. 27 Walifurahia kufanya hivi. Na ilikuwa kama kulipa kitu fulani walichokuwa wakidaiwa, kwa sababu kama watu wasiokuwa Wayahudi walikuwa wamebarikiwa kiroho na Wayahudi. Hivyo nao wanapaswa kutumia baraka za vitu walivyonavyo kwa ajili ya kuwasaidia Wayahudi. 28 Naelekea Yerusalemu kuhakikisha kuwa maskini wanapokea fedha hizi zilizotolewa kwa ajili yao.
Nitakapokuwa nimekamilisha hilo, nitaondoka kuelekea Hispania na nikiwa njiani nitasimama ili niwaone. 29 Na ninajua kwamba nitakapowatembelea, nitakuja na baraka zote anazotoa Kristo.
30 Kaka na dada zangu, nawaomba mnisaidie katika kazi hii kwa kuniombea kwa Mungu. Fanyeni hivi kwa sababu ya Bwana wetu Yesu Kristo na pendo ambalo Roho anatupa. 31 Niombeeni ili niokolewe kutokana na wale walioko Yudea wanaokataa kuupokea ujumbe wetu. Pia ombeni kwamba msaada huu ninaoupeleka Yerusalemu utakubalika kwa watu wa Mungu huko. 32 Kisha, nitakuwa na furaha wakati nitakapokuja kuwaona, Mungu akipenda. Na ndipo tutaweza kufurahia muda wa kujengana sisi kwa sisi. 33 Mungu anayetoa amani awe pamoja nanyi nyote. Amina.
© 2017 Bible League International