Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Exod for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka 8

Yesu Akiwa Galilaya

Siku iliyofuata, Yesu alisafiri kupitia katika baadhi ya miji na vijiji. Yesu aliwahubiri watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Mitume kumi na wawili walikuwa pamoja naye. Walikuwepo pia baadhi ya wanawake ambao Yesu aliwaponya magonjwa na pepo wabaya. Mmoja wao alikuwa Mariamu aitwaye Magdalena ambaye alitokwa na pepo saba; Pia pamoja na wanawake hawa alikuwepo Yoana mke wa Kuza (msimamizi wa mali za Herode), Susana, na wanawake wengine wengi. Wanawake hawa walitumia fedha zao kuwahudumia Yesu na mitume wake.

Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu

(Mt 13:1-17; Mk 4:1-12)

Kundi kubwa la watu lilikusanyika. Watu walimjia Yesu kutoka katika kila mji, naye Yesu akawaambia fumbo hili:

“Mkulima alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akizitawanya, baadhi zilianguka kandokando ya njia. Watu wakazikanyaga, na ndege wa angani wakazila. Zingine zikaanguka kwenye udongo wenye mawe. Zilipoanza kukua zikafa kwa sababu ya kukosa maji. Mbegu zingine ziliangukia kwenye miiba. Miiba ikakua pamoja nazo, miiba ikazisongasonga na hazikukua. Zilizosalia ziliangukia kwenye udongo mzuri wenye rutuba. Mbegu hizi zikaota na kuzaa kila moja mia.”

Yesu akamalizia fumbo. Kisha akapaza sauti, akasema, “Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!”

Wafuasi wake wakamwuliza, “Fumbo hili linamaanisha nini?”

10 Akasema, “Mmechaguliwa kujua kweli za siri kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini ninatumia mafumbo kuzungungumza na watu wengine. Ninafanya hivi ili,

‘Watazame,
    lakini wasiweze kuona.
Wasikia,
    lakini wasielewe.’(A)

Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu

(Mt 13:18-23; Mk 4:13-20)

11 Hii ndiyo maana ya fumbo hili: Mbegu ni Neno la Mungu. 12 Watu wengine ni kama mbegu zilizoanguka njiani. Husikia mafundisho ya Mungu, lakini Shetani huja na kuwafanya waache kuyatafakari. Hii huwafanya kutoamini na kuokoka. 13 Wengine wanafanana na mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye mawe. Ni watu ambao huyasikia mafundisho ya Mungu na kuyapokea kwa furaha, lakini kwa kuwa hawana mizizi yenye kina, huamini kwa muda mfupi. Majaribu yanapokuja, humwacha Mungu.

14 Zilizoanguka katika miiba, zinafanana na watu wanaoyasikia Mafundisho ya Mungu, lakini wanaruhusu wasiwasi, mali na anasa za maisha haya kuwasimamisha na hawaendelei kukua. Hivyo mafundisho hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao.[a] 15 Na zile zilizoangukia katika udongo mzuri, ni wale ambao huyasikia mafundisho ya Mungu kwa moyo safi na mnyoofu. Huyatii na kwa uvumilivu wao huzaa mazao mazuri.

Zingatieni Nuru

(Mk 4:21-25)

16 Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa bakuli au kuificha uvunguni mwa kitanda. Badala yake huiweka kwenye kinara cha taa mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani wapate nuru ya kuwawezesha kuona. 17 Kila jambo lililofichwa litawekwa wazi na kila siri itajulikana na kila mtu ataiona. 18 Hivyo yatafakarini kwa umakini yale mnayosikia. Watu wenye uelewa kiasi watapokea zaidi. Lakini wale wasio na uelewa watapoteza hata ule wanaodhani kuwa wanao.”

Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi

(Mt 12:46-50; Mk 3:31-35)

19 Mama yake Yesu na wadogo zake wakaenda kumwona, lakini walishindwa kumfikia kwa sababu walikuwepo watu wengi sana. 20 Mtu mmoja akamwambia Yesu, “Mama yako na wadogo zako wamesimama nje. Wanataka kukuona.”

21 Yesu akawajibu “Mama yangu na wadogo zangu ni wale wanaolisikia na kulitii Neno la Mungu.”

Yesu Atuliza Dhoruba

(Mt 8:23-27; Mk 4:35-41)

22 Siku moja Yesu na wafuasi wake walipanda mashua. Akawaambia, “Tuvuke mpaka upande mwingine wa ziwa.” Wakaanza safari kuvuka ziwa. 23 Walipokuwa wanasafiri, Yesu alisinzia. Tufani kubwa ikalikumba ziwa na mashua ikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. 24 Wafuasi wakamwendea, wakamwamsha, wakasema, “Mkuu, mkuu, tutazama!”

Yesu akasimama, akaukemea upepo na mawimbi ya maji. Upepo ukakoma na ziwa likatulia. 25 Ndipo Yesu akawaambia wafuasi wake, “Imani yenu iko wapi?”

Lakini wao waliogopa na kustaajabu, wakanong'onezana, “Huyu ni mtu wa namna gani? Anaamuru upepo na maji, na vinamtii?”

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu

(Mt 8:28-34; Mk 5:1-20)

26 Yesu na wafuasi wake wakasafiri mpaka katika nchi walimoishi Wagerasi[b] iliyokuwa ng'ambo ya ziwa Galilaya. 27 Yesu alipotoka katika mashua, mwanaume mmoja kutoka katika mji ule alimwendea. Mtu huyu alikuwa na mapepo ndani yake. Kwa muda mrefu hakuwahi kuvaa nguo na aliishi makaburini.

28-29 Pepo aliyekuwa ndani yake alikuwa akimpagaa mara nyingi na alikuwa akifungwa gerezani, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo. Lakini kila mara aliivunja. Pepo ndani yake alikuwa anamlazimisha kwenda nje ya mji mahali pasipoishi watu. Yesu alimwamuru kumtoka mtu yule. Alipomwona Yesu, alianguka mbele yake huku akipiga kelele kwa sauti, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu Aliye Juu? Tafadhali usiniadhibu!”

30 Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?”

Mtu yule akajibu, “Jeshi.”[c] (Alisema jina lake ni “Jeshi” kwa sababu pepo wengi walikuwa wamemwingia.) 31 Pepo wale wakamsihi Yesu asiwaamuru kwenda shimoni.[d] 32 Katika kilima kile, kulikuwa kundi kubwa la nguruwe wakichungwa. Pepo wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie wale nguruwe. Hivyo Yesu akawaruhusu. 33 Pepo wakamtoka yule mtu, na kuwaingia nguruwe. Kundi lote la wale nguruwe likakimbia kutelemkia ziwani kwa kasi, nguruwe wakazama na kufia humo.

34 Wachungaji wa nguruwe walipoona lililotokea, walikimbia, wakaenda kutoa taarifa mjini na mashambani. 35 Watu wakaenda kuona lililotokea. Walipofika alipokuwa Yesu wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, akiwa na akili zake timamu; pepo walikuwa wamemtoka. Jambo hili likawaogopesha watu. 36 Wale walioona mambo haya yalivyotokea waliwaambia wengine namna Yesu alivyomponya yule mtu. 37 Watu wote waliokuwa wakiishi eneo lote la Gerasi wakamtaka Yesu aondoke kwa sababu waliogopa.

Hivyo Yesu akapanda mashua na kurudi Galilaya. 38 Mtu aliyeponywa alimsihi amfuate Yesu. Lakini Yesu akamtuma, akamwambia, 39 “Rudi nyumbani, ukawaeleze watu mambo ambayo Mungu amekutendea.”

Hivyo mtu yule alikwenda sehemu zote za mji akieleza mambo ambayo Yesu amemtendea.

Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa

(Mt 9:18-26; Mk 5:21-43)

40 Yesu aliporudi Galilaya, watu walimkaribisha. Kila mtu alikuwa anamsubiri. 41-42 Mtu mmoja jina lake Yairo, aliyekuwa mkuu wa sinagogi alimwendea. Alikuwa na binti mmoja tu mwenye umri wa miaka kumi na mbili na alikuwa mgonjwa sana katika hali ya kufa. Hivyo Yairo alisujudu miguuni pa Yesu na akamsihi aende nyumbani kwake.

Yesu alipokuwa akienda nyumbani kwa Yairo, watu walimzonga kila upande. 43 Mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili alikuwepo katika umati huo. Alikuwa ametumia mali zake zote kwa madaktari,[e] lakini hakuna daktari aliyeweza kumponya. 44 Alikwenda nyuma ya Yesu na kugusa pembe ya vazi lake. Wakati huo huo damu ikaacha kumtoka. 45 Ndipo Yesu akasema, “Nani amenigusa?”

Kila mtu alikataa kuwa hajamgusa, Petro akasema, “Mkuu, watu wamekuzunguka na wanakuzongazonga kila upande.”

46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu amenigusa. Nimesikia nguvu ikinitoka.” 47 Yule mwanamke alipoona ya kwamba hataweza kujificha akajitokeza akitetemeka. Akasujudu mbele ya Yesu. Huku kila mmoja akisikia, akaeleza sababu iliyomfanya amguse, na kwamba alipona wakati ule ule alipomgusa. 48 Yesu alimwambia, “Binti yangu umeponywa kwa sababu uliamini. Nenda kwa amani.”

49 Yesu alipokuwa bado anaongea, mtu mmoja kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi alikuja na akasema, “Binti yako amekwisha kufa! Hakuna haja ya kuendelea kumsumbua Mwalimu.”

50 Yesu aliposikia maneno hayo, alimwambia Yairo, “Usiogope! Amini tu na binti yako ataponywa.”

51 Yesu akaenda nyumbani, alipofika akaruhusu Petro, Yohana, Yakobo pamoja na baba na mama wa yule mtoto tu kuingia ndani pamoja naye. 52 Kila mtu alikuwa akilia na kusikia huzuni kwa sababu msichana alikuwa amekufa. Lakini Yesu akasema, “Msilie. Hajafa. Amelala usingizi tu.”

53 Watu wakamcheka, kwa sababu walijua kuwa amekwisha kufa. 54 Lakini Yesu akamshika mkono na kumwambia, “Mtoto inuka!” 55 Roho yake ikamrudia, akasimama hapo hapo. Yesu akasema, “Mpeni chakula.” 56 Wazazi wa yule binti wakashangaa. Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote lililotokea.

Error: Book name not found: Job for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
1 Wakorintho 9

Haki Ambazo Paulo Hajazitumia

Mnajua kuwa mimi ni mtu niliye huru. Mnajua kuwa mimi ni mtume na kwamba nilimwona Yesu Bwana wetu. Na ninyi ni kielelezo cha kazi yangu katika Bwana. Wengine wanaweza wasikubali kuwa mimi ni mtume, lakini hakika ninyi mnakubali. Ninyi ni uthibitisho kuwa mimi ni mtume wa Bwana.

Ninataka kuwajibu baadhi ya watu wanaotaka kunichunguza. Je, hatuna haki ya kula na kunywa? Je, hatuna haki ya kusafiri pamoja na mke aliye mwamini? Mitume wengine wote, wadogo zake Bwana na Petro hufanya hivi. Na je, ni mimi na Barnaba tu ndiyo ambao ni lazima tufanya kazi ili tupate kipato cha kutuwezesha kuishi? Ni askari gani aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi la kondoo na hanywi maziwa?

Lakini nina mifano mingi kutoka katika maisha ya kila siku inayosisitiza hoja yangu. Sheria ya Mungu inasema vivyo hivyo pia. Ndiyo, imeandikwa katika Sheria ya Musa kuwa; “Mnyama wa kazi anapotumika kupura nafaka, usimzuie kula nafaka.”(A) Je, Mungu aliposema hivi, alikuwa anawawazia wanyama pekee? Hapana. 10 Hakika Mungu alizungumza kuhusu sisi. Ndiyo, iliandikwa kwa ajili yetu. Wote wawili, anayelima na anayepura nafaka, wana haki ya kupata nafaka kutokana na kazi yao. 11 Ikiwa tulipanda mbegu ya kiroho mioyoni mwenu, je, hatustahili kupata vitu kwa ajili ya maisha haya kutoka kwenu? 12 Ikiwa wengine wana haki ya kupata vitu kutoka kwenu, hakika hata sisi tuna haki pia. Lakini hatuitumii haki hii. Tunavumilia katika hali zote ili tusimfanye mtu yeyote akaacha kuitii Habari Njema ya Kristo. 13 Hakika mnajua ya kuwa wanaotumika Hekaluni hula chakula kutoka Hekaluni. Na wale wanaotumika madhabahuni hupata sehemu ya yale yanayotolewa madhabahuni. 14 Vivyo hivyo kwa wale wenye kazi ya kuhubiri Injili. Bwana ameamuru kuwa nao wataishi kutokana na kazi hiyo.

15 Lakini sijatumia haki hizi, na si kwamba ninataka kitu chochote kutoka kwenu. Ijapokuwa ninaandika hivi hilo si lengo langu. Ni bora nife kuliko mtu yeyote kuchukua kutoka kwangu kitu ninachojivunia. 16 Sijivuni kwa sababu ya kazi yangu ya kuhubiri Habari Njema kwa sababu ni wajibu wangu ambao ni lazima nifanye; ole wangu nisipowahubiri watu Habari Njema. 17 Ikiwa ningehubiri kwa sababu ya utashi kwangu, ningestahili kulipwa. Lakini sikuchagua kufanya kazi hii. Ni lazima nihubiri Habari Njema. Hivyo ninafanya kazi niliyokabidhiwa. 18 Sasa, kwa kufanya kazi hii ninapata nini? Thawabu yangu, ni kuwa ninapowahubiri watu Habari Njema, ninawapa bure na sizitumii haki zinazoambatana na kufanya kazi hii.

19 Niko huru. Similikiwi na mtu yeyote, lakini ninakuwa mtumwa ili watu wengi waokoke. 20 Kwa Wayahudi nilienenda kama Myahudi ili nisaidie Wayahudi wengi waokolewe. Sitawaliwi na sheria, lakini kwa wanaotawaliwa na sheria nilikuwa kama ninayetawaliwa na sheria. Nilifanya hivi kuwasaidia wanaotawaliwa na sheria, ili waokoke. 21 Kwa wasio na sheria nilikuwa kama nisiye na sheria, ili niwasaidie wasio na sheria kuokoka. Mimi si kama mtu asiye na Sheria ya Mungu, ninatawaliwa na sheria ya Kristo. 22 Kwa waliodhaifu, nilikuwa dhaifu ili niwasaidie kuokoka. Nilifanyika kila kitu kwa watu wote ili nifanye kila kinachowezekana niweze kuwasaidia watu waokolewe. 23 Ninafanya kila ninachoweza ili Habari Njema ijulikane na niweze kushiriki katika Habari zake.

24 Mnajua kuwa katika riadha, wanariadha wengi hukimbia, lakini mmoja tu hupata zawadi. Hivyo kimbieni hivyo. Kimbieni ili mshinde! 25 Wote wanaoshiriki katika mchezo hufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kushinda na kupata zawadi. Lakini zawadi wanazopata hazidumu milele. Lakini zawadi yetu ni ile inayodumu milele. 26 Hivyo ninakimbia kama mtu mwenye malengo. Ninapigana ngumi kama mpiganaji anayepiga kitu, si kama anayepiga hewa. 27 Ninaudhibiti mwili wangu kikamilifu na kuufanya unitiii kwa kila jambo ninalotaka kutenda. Ninafanya hivi ili mimi binafsi nisiikose thawabu baada ya kuwahubiri wengine Habari Njema.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International