Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: 1Chr for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
1 Petro 4

Maisha Mapya

Kristo aliteseka alipokuwa katika mwili wake. Hivyo mjitayarishe kwa fikra ile ile aliyokuwa nayo Kristo. Yeyote anayekubali kuteseka katika maisha haya hakika ameamua kuacha kutenda dhambi. Jiimarishe wenyewe ili mweze kuishi maisha yenu yaliyosalia hapa duniani kwa kutenda yale anayotaka Mungu, siyo maovu ambayo watu wanataka kufanya. Huko nyuma mmepoteza muda mwingi mkitenda yale ambayo wasiyomjua Mungu wanapenda kutenda. Mliishi kwa kutojali maadili, mkitenda maovu mliyotaka kutenda. Daima mlikuwa mnalewa, mlifanya sherehe mbaya za ulevi, na mlitenda mambo ya aibu katika ibada zenu za sanamu.

Na sasa “marafiki” zenu wa zamani wanaona ni ajabu kwamba ninyi hamshirikiani nao katika njia za maisha zilizo mbaya na zisizofaa wanazozifuata. Na hivyo wanasema mabaya juu yenu. Lakini itawalazimu kukutana na Mungu na kutoa maelezo juu ya yale waliyoyatenda. Yeye ndiye atakaye hukumu watu wote muda si mrefu, walio hai sasa na wale waliokwisha kufa. Walikosolewa na wengine katika maisha yao hapa duniani. Lakini ulikuwa mpango wa Mungu kwamba wasikie Habari Njema kabla hawajafa ili wawe na maisha mapya katika Roho.

Vitumieni vizuri vipawa vya Mungu

Wakati wa kila kitu kufikia mwisho wake umekaribia. Hivyo iweni waangalifu katika akili zenu na mjizuie kwa kila jambo. Hii itawasaidia katika maombi yenu. Jambo lililo muhimu kuliko yote, daima mpendane ninyi kwa ninyi kikamilifu, kwa sababu upendo huwawezesha kusamehe dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi katika nyumba zenu na kushiriki chakula kwa pamoja pasipo manunguniko. 10 Mungu amewapa neema yake kwa namna nyingi mbalimbali. Hivyo muwe watumishi wema na kila mmoja wenu atumie kipawa chochote alichopewa kwa njia iliyo bora katika kuhudumiana ninyi kwa ninyi. 11 Ikiwa kipawa chako ni kuhubiri, maneno yako yawe kama yanayotoka kwa Mungu. Ikiwa kipawa chako ni kuhudumu, unatakiwa kuhudumu kwa nguvu anazokupa Mungu. Ndipo Mungu atakaposifiwa kwa kila jambo katika Yesu Kristo. Uwezo na utukufu ni wake milele na milele. Amina.

Kuteseka kama mfuasi wa Kristo

12 Rafiki zangu, msishangae kwa sababu ya mateso mnayoyapata sasa, mateso hayo yanaijaribu imani yenu. Msidhani kuwa linalotokea kwenu ni jambo la ajabu. 13 Lakini mnapaswa kufurahi kwa kuwa mnayashiriki mateso ya Kristo. Mtafurahi na kujawa na raha wakati uweza wake mkuu utapodhihirishwa kwa ulimwengu. 14 Mhesabu kuwa ni heshima watu wanapowanenea mabaya kwa sababu mnamwakilisha Kristo. Linapotokea hilo inaonesha kuwa Roho wa Mungu, aliye Roho wa utukufu, yupo pamoja nanyi. 15 Mnaweza kupata mateso; lakini msiteseke kwa sababu mmeua, mmeiba, mmesababisha ghasia, au mmejaribu kutawala maisha ya watu wengine. 16 Lakini endapo utateswa kwa kuwa ni “Mkristo” basi usione haya. Bali umshukuru Mungu kwa kuwa unalibeba jina hilo. 17 Wakati wa kuanza hukumu umewadia. Hukumu hiyo itaanza na familia ya Mungu. Ikiwa itaanzia kwetu, nini kitawatokea wale wasioikubali Habari Njema ya Mungu?

18 “Iwapo ni vigumu hata kwa mtu mwema kuokolewa,
    nini kitatokea kwa yule aliye kinyume na Mungu na amejaa dhambi?”(A)

19 Hivyo kama mnateseka kwa sababu ya kutii mapenzi ya Mungu, yakabidhini maisha yenu kwake maana Yeye ndiye aliyewaumba, na hivyo mnapaswa kumwamini. Na anastahili kuthaminiwa na kuaminiwa.

Error: Book name not found: Mic for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka 11

Yesu Afundisha Kuhusu Maombi

(Mt 6:9-15)

11 Siku moja Yesu alitoka akaenda mahali fulani kuomba. Alipomaliza, mmoja wa wafuasi wake akamwambia, “Yohana aliwafundisha wafuasi wake namna ya kuomba. Bwana, tufundishe nasi pia.”

Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivi ndivyo mnapaswa kuomba:

‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe daima.
    Tunaomba Ufalme wako uje.
Utupe chakula tunachohitaji kila siku.
Utusamehe dhambi zetu,
    kama tunavyomsamehe kila mtu anayetukosea.
Na usiruhusu tukajaribiwa.’”

Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji

(Mt 7:7-11)

5-6 Kisha Yesu akawaambia, “Chukulia mmoja wenu angekwenda kwa rafiki yake usiku na kumwambia, ‘Rafiki yangu aliyekuja mjini amekuja kunitembelea. Lakini sina chakula cha kumpa ili ale. Tafadhali nipe mikate mitatu.’ Rafiki yako ndani ya nyumba akajibu, ‘Nenda zako! Usinisumbue! Mlango umefungwa. Mimi na watoto wangu tumeshapanda kitandani kulala. Siwezi kuamka ili nikupe kitu chochote kwa sasa.’ Ninawaambia, urafiki unaweza usimfanye aamke akupe kitu chochote. Lakini hakika ataamka ili akupe unachohitaji ikiwa utaendelea kumwomba. Hivyo ninawaambia, Endeleeni kuomba na Mungu atawapa. Endeleeni kutafuta na mtapata. Endeleeni kubisha milangoni, na milango itafunguliwa kwa ajili yenu. 10 Ndiyo, kila atakayeendelea kuomba atapokea. Kila atakayeendelea kutafuta atapata. Na kila atakayeendelea kubisha mlangoni, mlango utafunguliwa kwa ajili yake. 11 Je, kuna mmoja wenu aliye na mwana? Utafanya nini ikiwa mwanao atakuomba samaki? Je, kuna baba yeyote anayeweza kumpa nyoka? 12 Au akiomba yai, utampa nge? Hakika hakuna baba wa namna hivyo. 13 Ikiwa ninyi waovu mnajua namna ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Vivyo hivo, hakika Baba yenu aliye mbinguni anajua namna ya kuwapa Roho Mtakatifu wale wanao mwomba?”

Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu

(Mt 12:22-30; Mk 3:20-27)

14 Wakati mmoja Yesu alikuwa akitoa pepo aliyemfanya mtu ashindwe kuzungumza. Ikawa, pepo alipotoka, yule mtu akaanza kuongea, umati wa watu walishangaa. 15 Lakini baadhi ya watu walisema, “Anatumia nguvu za Shetani kuwatoa pepo. Shetani[a] ni mtawala wa pepo wachafu.”

16 Baadhi ya watu wengine waliokuwa pale walitaka kumjaribu Yesu, walimwomba afanye muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. 17 Lakini alijua walichokuwa wanafikiria, hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe huteketezwa; na familia yenye magomvi husambaratika. 18 Hivyo, ikiwa Shetani anapigana yeye mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Ninawauliza hivi kwa kuwa mnasema kwamba ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani. 19 Lakini ikiwa ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani, watu wenu wanatumia nguvu gani wanapotoa pepo? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa ninyi ni waovu. 20 Lakini, ninatumia nguvu za Mungu kutoa pepo. Hii inaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu sasa.

21 Mwenye nguvu aliye na silaha nyingi anapoilinda nyumba yake, vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake huwa salama. 22 Lakini chukulia kuwa mwenye nguvu zaidi kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yule mwenye nguvu zaidi humnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea kuilinda nyumba yake. Ndipo mwenye nguvu zaidi atavitumia vitu vya yule mtu wa kwanza kadri anavyotaka.

23 Mtu yeyote asiye pamoja nami, yuko kinyume nami. Na mtu yeyote asiyefanya kazi pamoja nami anafanya kinyume nami.

Hatari ya Kuwa Mtupu

(Mt 12:43-45)

24 Mtu anapotokwa na roho chafu, roho hiyo husafiri sehemu zilizo kavu, ikitafuta mahali ili ipumzike. Lakini hukosa mahali pa kupumzika. Hivyo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba nilikotoka.’ 25 Inaporudi hukuta nyumba imesafishwa na kupangwa vizuri. 26 Ndipo roho hiyo chafu huenda ikachukua roho wengine saba, walio waovu kuliko yenyewe. Na kwa pamoja roho zote hizo huingia na kuishi ndani ya mtu huyo, na mtu huyo hupata matatizo mengi kuliko ya kwanza.”

Watu Wanaobarikiwa na Mungu

27 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, mwanamke mmoja katika kundi la watu akapaza sauti akamwambia “Amebarikiwa na Mungu mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!”

28 Lakini Yesu akasema, “Wamebarikiwa zaidi wanaosikia na kuyatii mafundisho ya Mungu.”

Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu

(Mt 12:38-42; Mk 8:12)

29 Baada ya kundi la watu kuongezeka na kumzunguka, Yesu alisema, “Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu. Mnaomba muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia jambo lolote. Ishara pekee mtakayopata ni kile kilichompata Yona.[b] 30 Yona alikuwa ishara kwa watu walioishi katika mji wa Ninawi. Ni sawasawa na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa watu wa wakati huu.

31 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa, mtalinganishwa na Malkia wa Kusini,[c] naye pia, atakuwa shahidi atakayeonyesha namna mlivyo waovu. Kwa nini ninasema haya? Kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana ili ayasikilize mafundisho yenye hekima ya Suleimani. Na ninawaambia mkuu[d] kuliko Suleimani yupo hapa, lakini hamnisikilizi!

32 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa mtafananishwa pia na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha makosa yenu. Ninasema hivi kwa sababu Yona alipowahubiri, walibadili mioyo na maisha yao. Na sasa mnamsikia mtu aliye mkuu kuliko Yona, Lakini hamtaki kubadilika!

Iweni Mwanga kwa Ajili ya Ulimwengu

(Mt 5:15; 6:22-23)

33 Hakuna mtu anayechukua taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunika. Badala yake huiweka mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani waweze kuiona nuru yake. 34 Namna unavyowatazama watu inaonesha kwa hakika jinsi ulivyo. Unapowatazama watu katika hali isiyo ya ubinafsi, inaonesha wazi kuwa umejaa nuru. Lakini unapowatazama watu katika namna ya uchoyo, ni wazi kuwa umejaa giza.[e] 35 Hivyo iweni waangalifu ili nuru iliyo ndani yenu usiwe giza! 36 Ikiwa umejaa nuru na hakuna sehemu yenye giza ndani yako, basi utang'aa, kama nuru ya kwenye taa.”

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)

37 Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38 Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa[f] mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39 Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40 Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41 Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.

42 Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani[g] zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.

43 Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44 Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”

45 Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.[h] Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47 Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48 Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49 Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume[i] kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’

50 Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51 Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,[j] aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.

52 Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”

53 Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54 ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International