Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: 1Chr for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yakobo 1

Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo.

Kwa makabila Kumi na Mawili[a] ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu!

Imani na Hekima

Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi. Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu. Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote.

Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima. Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yo yote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa. Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana; yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja.

Utajiri wa Kweli

Ndugu aliye maskini na awe na furaha sana kwamba Mungu amemchukulia kuwa mtu wa maana sana. 10 Na waaminio walio matajiri wawe na furaha sana tu pale Mungu anapowashusha chini. Kwani utajiri wao hautawazuia kufa kama maua ya porini. 11 Jua linapochomoza na kuwa kali zaidi, joto lake hukausha mimea na maua huanguka chini na kupukutika na kupoteza urembo wake. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtu tajiri atafifia katika shughuli zake.

Majaribu Hayatoki kwa Mungu

12 Amebarikiwa mtu yule anayestahimili majaribu, maana anapofaulu mitihani atapokea taji yenye uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wanaompenda. 13 Yeyote anayejaribiwa hapaswi kusema, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu maovu hayamjaribu Mungu na hamjaribu mtu yeyote. 14 Bali kila mmoja anajaribiwa na tamaa zake mwenyewe, anapovutwa na kunaswa. 15 Kisha tamaa inapotunga mimba inazaa dhambi, na dhambi ikikomaa kabisa inazaa kifo.

16 Kaka zangu na dada zangu wapendwa msikubali kudanganywa, 17 Kila karama njema na kila tuzo kamilifu hutoka juu; hushuka chini kutoka kwa Baba aliyeumba nuru zote zilizoko mawinguni ambamo kwake yeye hakuna mabadiliko kama vile vivuli vinavyosababishwa na mzunguko wa sayari. 18 Kwa uamuzi wake mwenyewe Mungu alituzaa sisi na kuwa watoto wake kwa njia ya ujumbe wa kweli ili tuwe mazao ya kwanza[b] yenye heshima ya pekee miongoni mwa vyote alivyoviumba.

Kusikiliza na Kutii

19 Kumbukeni hili ndugu zangu wapendwa: Kila mtu awe mwepesi wa kusikia lakini awe mzito wa kusema, na mzito kukasirika, 20 kwa sababu hasira ya mwanadamu haitoi haki inayohitajiwa na Mungu toka kwetu. 21 Hivyo acheni matendo yote machafu na kila uovu uliokaa karibu yenu, na mpokee kwa unyenyekevu mafundisho yaliyopandwa ndani ya mioyo yenu. Neno hilo, lina uwezo wa kuleta wokovu wa roho zenu.

22 Usisikilize tu kile ambacho mafundisho ya Mungu yanakisema; bali fanya yale inayosema! Ikiwa utasikiliza tu, utajidanganya mwenyewe. 23 Kwani kama mtu atasikiliza mafundisho ya Mungu, lakini asitende yanayosemwa, yuko kama mtu anayeutazama uso wake kwenye kioo. 24 Anajiangalia mwenyewe kwa haraka na anapoondoka tu husahau anavyoonekana. 25 Lakini anayetazama kwa makini katika sheria kamilifu ya Mungu, inayowaletea watu uhuru, na akaendelea kufanya hivyo asiwe msikilizaji anayesahau, bali huyatunza mafundisho katika matendo, mtu huyo atakuwa na baraka katika kila analofanya.

Njia Sahihi ya Kumwabudu Mungu

26 Kama kuna anayedhani kuwa ni mshika dini, lakini bado hauzuii ulimi wake anajidanganya mwenyewe. Dini yake mtu huyu haina manufaa. 27 Dini safi na isiyo na lawama mbele za Mungu Baba, inahusisha haya: kuwatunza yatima na wajane katika mazingira mgumu na kujilinda asichafuliwe na ulimwengu.

Error: Book name not found: Amos for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka 3

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Yh 1:19-28)

Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo:

Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi;

Herode alikuwa mtawala wa Galilaya;

Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti;

na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene.

Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema,

“Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.
Kila bonde litajazwa,
    na kila mlima na kilima vitasawazishwa.
Barabara zilizopinda zitanyooshwa,
    na barabara zenye mashimo zitasawazishwa.
Na kila mtu ataona
    jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’”(A)

Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! Na sasa shoka liko tayari kukata miti,[a] kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

10 Watu wakamwuliza Yohana, “Tufanye nini?”

11 Akajibu, “Ukiwa na mashati mawili mpe moja asiyekuwa na shati. Kama una chakula, kigawe pia.”

12 Hata watoza ushuru walikuja kwa Yohana. Walitaka wabatizwe. Walimwambia, “Mwalimu, tufanye nini sisi?”

13 Akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi kuliko kiwango kilichoamriwa.”

14 Askari wakamwuliza, “Vipi kuhusu sisi? Tufanye nini?”

Akawaambia, “Msitumie nguvu au kutengeneza mashtaka ya uongo ili watu wawape pesa. Mtosheke na mishahara mnayopata.”

15 Kila mtu alitarajia kuja kwa Masihi,[b] na walijiuliza wakisema, “Labda Yohana ndiye Masihi.”

16 Yohana aliwajibu watu wote, akasema, “Ninawabatiza ninyi katika maji, lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Yuko tayari sasa kuja kusafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri na makapi, na kuiweka katika ghala yake kisha ataichoma ile isiyofaa katika moto usiozimika.” 18 Hivi ndivyo ambavyo Yohana aliwahubiri watu Habari Njema. Aliwaonya sana kuwa wanatakiwa kubadili njia zao.

Kazi ya Yohana Ilivyomalizika Baadaye

19 Yohana alimkosoa Herode kwa sababu ya mambo mabaya aliyokuwa ameyafanya na Herodia, mkewe kaka yake Herode, na pia kwa mambo mengine mabaya aliyokuwa ameyafanya. 20 Hivyo Herode aliongeza jambo jingine baya katika matendo yake maovu. Alimfunga Yohana gerezani.

Yohana Ambatiza Yesu

(Mt 3:13-17; Mk 1:9-11)

21 Watu wote walipokuwa wakibatizwa, Yesu alikuja naye akabatizwa. Na alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka, 22 na Roho Mtakatifu aliyekuwa katika umbo la njiwa akashuka juu yake. Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.”

Ukoo wa Yesu

(Mt 1:1-17)

23 Yesu alipoanza kufundisha, alikuwa na umri kama wa miaka thelathini. Watu walidhani kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Yusufu.

Yusufu alikuwa mwana wa Eli.

24 Eli alikuwa mwana wa Mathati.

Mathati alikuwa mwana wa Lawi.

Lawi alikuwa mwana wa Melki.

Melki alikuwa mwana wa Yana.

Yana alikuwa mwana wa Yusufu.

25 Yusufu alikuwa mwana wa Matathia.

Matathia alikuwa mwana wa Amosi.

Amosi alikuwa mwana wa Nahumu.

Nahumu alikuwa mwana wa Esli.

Esli alikuwa mwana wa Nagai.

26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi.

Maathi alikuwa mwana wa Matathia.

Matathia alikuwa mwana wa Semei.

Semei alikuwa mwana wa Yusufu.

Yusufu alikuwa mwana wa Yoda.

27 Yoda alikuwa mwana wa Yoana.

Yoana alikuwa mwana wa Resa.

Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli.

Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli.

Shealtieli alikuwa mwana wa Neri.

28 Neri alikuwa mwana wa Melki.

Melki alikuwa mwana wa Adi.

Adi alikuwa mwana wa Kosamu.

Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu,

Elmadamu alikuwa mwana wa Eri.

29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua.

Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri.

Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu.

Yorimu alikuwa mwana wa Mathati.

Mathati alikuwa mwana wa Lawi.

30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni.

Simeoni alikuwa mwana wa Yuda.

Yuda alikuwa mwana wa Yusufu.

Yusufu alikuwa mwana wa Yonamu.

Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu.

31 Eliakimu alikuwa mwana wa Melea.

Melea alikuwa mwana wa Mena.

Mena alikuwa mwana wa Matatha.

Matatha alikuwa mwana wa Nathani.

Nathani alikuwa mwana wa Daudi.

32 Daudi alikuwa mwana wa Yese.

Yese alikuwa mwana wa Obedi.

Obedi alikuwa mwana wa Boazi.

Boazi alikuwa mwana wa Salmoni.[c]

Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni.

33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu.

Aminadabu alikuwa mwana wa Admini,

Admini alikuwa mwana wa Aramu.[d]

Aramu alikuwa mwana wa Hesroni.

Hesroni alikuwa mwana wa Peresi.

Peresi alikuwa mwana wa Yuda.

34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo.

Yakobo alikuwa mwana wa Isaka.

Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu.

Ibrahimu alikuwa mwana wa Tera.

Tera alikuwa mwana wa Nahori.

35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi,

Serugi alikuwa mwana wa Ragau.

Ragau alikuwa mwana wa Pelegi.

Pelegi alikuwa mwana wa Eberi,

Eberi alikuwa mwana wa Sala.

36 Sala alikuwa mwana wa Kenani.

Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi.

Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu.

Shemu alikuwa mwana wa Nuhu.

Nuhu alikuwa mwana wa Lameki.

37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela.

Methusela alikuwa mwana wa Henoko.

Henoko alikuwa mwana wa Yaredi.

Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli.

Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani.

38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi.

Enoshi alikuwa mwana wa Sethi.

Sethi alikuwa mwana wa Adamu.

Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International