Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Lev for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yohana 20

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Lk 24:1-12)

20 Asubuhi na mapema siku ya Jumapili, wakati bado lilikuwepo giza, Mariamu Magdalena akaenda kwenye kaburi la Yesu. Naye akaona kuwa lile jiwe kubwa lilikuwa limeondolewa kutoka mlangoni. Hivyo akakimbia kwenda kwa Simoni Petro na kwa mfuasi mwingine (yule ambaye Yesu alimpenda sana). Akasema, “Wamemwondoa Bwana kutoka kaburini na hatujui wamemweka wapi.”

Kwa hiyo Petro na yule mfuasi mwingine wakaanza kuelekea kwenye kaburi. Wote walikuwa wakikimbia, lakini yule mfuasi mwingine alikimbia kwa kasi zaidi kuliko Petro na kuwasili wa kwanza kaburini. Alipofika akainama chini na kuchungulia ndani ya kaburi. Humo akaviona vipande vya nguo za kitani vikiwa pale chini, lakini hakuingia ndani.

Hatimaye Simoni Petro akafika kaburini na kuingia ndani. Naye aliviona vipande vile vya nguo za kitani vikiwa chini mle ndani. Pia aliiona nguo iliyokuwa imezungushwa kichwani kwa Yesu. Hii ilikuwa imekunjwa na kuwekwa upande mwingine tofauti na pale zilipokuwepo nguo za kitani. Kisha mfuasi mwingine, yule aliyefika kwanza kaburini, akaingia ndani. Yeye aliona yaliyotokea na akaamini. (Wafuasi hawa walikuwa bado hawajayaelewa yale Maandiko kwamba Yesu alipaswa kufufuka kutoka wafu.)

Yesu Amtokea Mariamu Magdalena

(Mk 16:9-11)

10 Kisha wafuasi wakarudi nyumbani. 11 Lakini Mariamu akabaki amesimama nje ya kaburi, akilia. Aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi alipokuwa akilia. 12 Mle ndani akawaona malaika wawili waliovaa nguo nyeupe na wameketi mahali ulipokuwa mwili wa Yesu. Mmoja amekaa sehemu kilipolazwa kichwa na mwingine aliketi sehemu miguu ilipokuwa imewekwa.

13 Malaika wakamwuliza Mariamu, “Mwanamke, kwa nini unalia?”

Mariamu akajibu, “Wameuondoa mwili wa Bwana wangu, na sijui wameuweka wapi.” 14 Wakati Mariamu aliposema hivi, akageuka nyuma na kumwona Yesu amesimama pale. Lakini hakujua kuwa huyo alikuwa ni Yesu.

15 Akamwuliza, “Mwanamke, kwa nini unalia? Je, unamtafuta nani?”

Yeye alifikiri kuwa huyu alikuwa ni mtunzaji wa bustani. Hivyo akamwambia, “Je, ulimwondoa Bwana? Niambie umemweka wapi. Nami nitaenda kumchukua.” 16 Yesu akamwita, “Mariamu.”

Mariamu akamgeukia na kumwambia kwa Kiaramu, “Raboni”, (hii ikiwa na maana “Mwalimu”).

17 Yesu akamwambia, “Hupaswi kunishika! Kwani bado sijapaa kwenda huko juu kwa Baba yangu. Lakini nenda ukawaambie wafuasi wangu[a] maneno haya: ‘Ninarudi kwa Baba yangu ambaye pia ni Baba yenu. Ninarudi kwa Mungu wangu ambaye pia ni Mungu wenu.’”

18 Mariamu Magdalena akaenda kwa wafuasi na kuwaambia, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaeleza yale Yesu aliyomwambia.

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Lk 24:36-49)

19 Ilikuwa siku ya Jumapili, na jioni ile wafuasi walikuwa pamoja. Nao walikuwa wamefunga milango kwa kuwa waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Ghafla, Yesu akawa amesimama pale katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 Mara baada ya kusema haya, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Wafuasi walipomwona Bwana, walifurahi sana.

21 Kisha Yesu akasema tena, “Amani iwe nanyi. Kama vile Baba alivyonituma, nami sasa nawatuma ninyi vivyo hivyo.” 22 Kisha akawapumulia pumzi na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkisamehe dhambi zake mtu yeyote, dhambi zake hizo zitasamehewa. Kama kuna mtu yeyote ambaye hamtamsamehe dhambi zake, dhambi zake huyo hazitasamehewa.”

Yesu Amtokea Tomaso

24 Tomaso (aliyeitwa Pacha) alikuwa ni mmoja wa wale kumi na mbili, lakini hakuwapo pamoja na wafuasi wengine Yesu alipokuja. 25 Wakamwambia, “Tulimwona Bwana.” Tomaso akasema, “Hiyo ni ngumu kuamini. Ninahitaji kuona makovu ya misumari katika mikono yake, niweke vidole vyangu ubavuni. Ndipo tu nitakapoamini.” 26 Juma moja baadaye wafuasi walikuwemo katika nyumba ile tena, na Tomaso alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja na kusimama katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa. Iangalie mikono yangu. Weka mkono wako hapa ubavuni mwangu. Acha kuwa na mashaka na uamini.”

28 Tomaso akamwambia Yesu, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

29 Yesu akamwambia, “Unaamini kwa sababu umeniona. Wana baraka nyingi watu wale wanaoniamini bila kuniona!”

Kwa Nini Yohana Aliandika Kitabu hiki

30 Yesu alifanya ishara nyingine nyingi za miujiza ambazo wafuasi wake waliziona, na ambazo hazikuandikwa kwenye kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili muweze kuamini kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu. Kisha, kwa kuamini, mpate uzima kupitia jina lake.

Error: Book name not found: Prov for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Wafilipi 4

Maagizo ya Mwisho

Kaka na dada zangu wapenzi, ninawapenda na ninataka kuwaona. Mnanifurahisha na ninajivuna kwa sababu yenu. Endeleeni kuwa imara kumfuata Bwana kama nilivyowaambia.

Ninawasihi Euodia na Sintike, ninyi nyote wawili ni wa Bwana, hivyo muwe na mtazamo mmoja. Kwa ajili ya hili ninamwomba rafiki yangu aliyetumika pamoja nami kwa uaminifu: Wasaidieni wanawake hawa. Waliwahubiri watu Habari Njema kwa bidii kama watendaji wenzangu tukiwa pamoja na Klementi na wengine waliofanya kazi pamoja nami. Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.[a]

Furahini katika Bwana daima. Ninasema tena, furahini.

Kila mtu auone wema na uvumilivu wenu. Bwana yu karibu kuja. Msisumbuke kitu chochote, lakini salini na kumwomba Mungu kwa mahitaji yenu. Mshukuruni Mungu wakati mnapomwomba yale mnayohitaji. Na kwa kuwa ninyi ni milki ya Kristo Yesu, amani ya Mungu itailinda mioyo na mawazo yenu isipate wasiwasi. Amani yake inaweza kutenda haya zaidi ya akili za kibinadamu.[b]

Na sasa, mwisho kabisa, kaka na dada zangu, fikirini kuhusu yale yaliyo ya kweli, ya kuheshimiwa, ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, na yanayosemwa vema. Yatendeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu, niliyowaambia na yale mliyoyaona nikitenda. Na Mungu atoaye amani atakuwa pamoja nanyi.

Paulo Apokea Zawadi Kwa Furaha

10 Nimefurahi sana katika Bwana kwa sababu mmeonesha tena kuwa mnanijali. Mmeendelea kujali juu yangu, lakini haikuwepo njia ya kuonesha hili. 11 Ninawaambia hili, si kwa sababu ninahitaji msaada kutoka kwa yeyote. Nimejifunza kuridhika na kile nilichonacho na chochote kinachotokea. 12 Ninajua namna ya kuishi ninapokuwa na vichache na ninapokuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuishi katika hali zote, ninapokuwa na vyakula vingi au ninapokuwa na njaa, ninapokuwa na vingi zaidi ya ninavyohitaji au ninapokuwa sina kitu. 13 Kristo ndiye anayenitia nguvu kuyakabili mazingira yote katika maisha.

14 Lakini mlifanya vyema mliposhiriki nami katika kipindi changu kigumu. 15 Enyi watu wa Filipi kumbukeni nilipokuja mara ya kwanza kuwahubiri Habari Njema watu wa Makedonia. Nilipoondoka huko, ninyi ndiyo kanisa pekee ambalo lilishirikiana nami katika uhusiano ulioendelea wa kutoa na kupokea. 16 Ukweli ni kuwa hata nilipokuwa Thesalonike, zaidi ya mara moja mlinitumia kila kitu nilichohitaji. 17 Si kwamba natafuta msaada wa kifedha kutoka kwenu. Bali ninataka ninyi mpokee manufaa yanayozidi kukua yanayotokana na kutoa. 18 Nina kila kitu ninachohitaji. Nina zaidi ya hata ninavyohitaji kwa sababu Epafrodito ameniletea kila kitu mlichompa aniletee. Zawadi zenu ni kama sadaka yenye harufu nzuri inayotolewa kwa Mungu. Ni sadaka anayoikubali, na inampendeza. 19 Mungu wangu atatumia utajiri wake wenye utukufu kuwapa ninyi kila kitu mnachohitaji kupitia Kristo Yesu. 20 Utukufu kwa Mungu na Baba yetu milele na milele. Amina.

21 Wasalimuni watakatifu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Wale walio katika familia ya Mungu walio pamoja nami wanawasalimu. 22 Na watu wote wa Mungu walio hapa wanawasalimu, hasa wale walio katika utumishi wa Kaisari.

23 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na utu wenu wa ndani.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International