M’Cheyne Bible Reading Plan
Utajiri Halisi
16 Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Alikuwepo mtu mmoja tajiri, aliyekuwa na msimamizi wa kuangalia biashara zake. Baadaye akagundua kuwa msimamizi wake alikuwa anapoteza pesa zake. 2 Hivyo, akamwita, akamwambia, ‘Nimesikia mambo mabaya juu yako. Nipe taarifa namna ulivyosimamia pesa zangu. Huwezi kuendelea kuwa msimamizi wangu.’
3 Hivyo msimamizi akawaza moyoni mwaka, ‘Nitafanya nini? Bwana wangu ananiachisha kazi yangu ya usimamizi. Sina nguvu za kulima, kuomba omba naona aibu. 4 Najua nitakalofanya! Nitafanya kitu nipate marafiki. Ili nitakapopoteza kazi yangu, watanikaribisha katika nyumba zao.’
5 Hivyo msimamizi akawaita mmoja mmoja wale waliokuwa wanadaiwa pesa na bwana wake. Akamwuliza wa kwanza, ‘Mkuu wangu anakudai kiasi gani?’ 6 Akamjibu, ‘Ananidai mitungi[a] 100 ya mafuta ya zeituni.’ Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, kaa chini, fanya haraka, badilisha iwe mitungi hamsini.’
7 Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe kiasi gani unadaiwa?’ Akajibu, ‘Vipimo[b] mia moja vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, ibadilishe iwe vipimo themanini.’
8 Baadaye bwana wake akamsifu msimamizi asiye mwaminifu kwa sababu ya kutenda kwa busara. Ndiyo, watu wa ulimwengu huu wana busara katika kufanya biashara kati yao kuliko wana wa Mungu.
9 Ninamaanisha hivi: Vitumieni vitu vya kidunia mlivyonavyo sasa ili muwe na ‘marafiki’ kwa ajili ya siku za baadaye. Ili wakati vitu hivyo vitakapotoweka, mtakaribishwa katika nyumba ya milele. 10 Mtu yeyote anayeweza kuaminiwa kwa mambo madogo anaweza kuaminiwa kwa mambo makubwa pia. Mtu asiye mwaminifu katika jambo dogo hawezi kuwa mwaminifu katika jambo kubwa. 11 Ikiwa huwezi kuaminiwa kwa mali za kidunia, huwezi kuaminiwa kwa mali za mbinguni. 12 Na kama hauwezi kuaminiwa kwa vitu vya mtu mwingine, hautapewa vitu kwa ajili yako wewe mwenyewe.
13 Mtumwa hawezi kuwatumikia mabwana wawili wakati mmoja, hata ninyi hamwezi. Utamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au utakuwa mwaminifu kwa mmoja na hautamjali mwingine. Pia, huwezi kumtumikia Mungu na pesa.”[c]
Sheria Ya Mungu Haiwezi Kubadilishwa
(Mt 11:12-13)
14 Mafarisayo walikuwa wakiyasikiliza mambo haya yote. Walimdhihaki Yesu kwa sababu wote walipenda pesa. 15 Yesu aliwaambia, “Mnajifanya kuwa wenye haki mbele za watu, lakini Mungu anajua hakika kilichomo mioyoni mwenu. Jambo ambalo watu hudhani kuwa la muhimu, kwa Mungu ni chukizo.
16 Kabla ya Yohana Mbatizaji kuja, watu walifundishwa Sheria ya Musa na maandishi ya Manabii. Lakini tangu wakati wa Yohana, Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu inahubiriwa. Na kila mtu anajitahidi sana ili kuingia katika ufalme wa Mungu. 17 Ni rahisi sana kwa mbingu na dunia kutoweka, kuliko sehemu ndogo ya herufi katika Sheria ya Musa kutoweka. 18 Mwanaume yeyote anayemtaliki mkewe na kumwoa mke mwingine anazini. Na mwanaume anayeoa mwanamke aliyetalikiwa anazini pia.”
Tajiri na Lazaro
19 Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja, tajiri ambaye daima alivaa nguo za thamani sana, alikuwa tajiri sana kiasi kwamba alifurahia vitu vizuri kila siku. 20 Alikuwepo pia maskini mmoja aliyeitwa Lazaro ambaye mwili wake ulikuwa umejaa vidonda. Mara nyingi aliwekwa kwenye lango la tajiri. 21 Lazaro alitaka tu kula masalia ya vyakula vilivyokuwa sakafuni vilivyodondoka kutoka mezani kwa tajiri. Na mbwa walikuja na kulamba vidonda vyake.
22 Baadaye Lazaro alikufa. Malaika walimchukua na kumweka kifuani pa Ibrahimu. Tajiri naye alikufa na kuzikwa. 23 Alichukuliwa mpaka mahali pa mauti[d] na akawa katika maumivu makuu. Alimwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro akiwa kifuani pake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie! Mtume Lazaro kwangu ili achovye ncha ya kidole chake kwenye maji na kuupoza ulimi wangu, kwa sababu ninateseka katika moto huu!’
25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, unakumbuka ulipokuwa unaishi? Ulikuwa na mambo yote mazuri katika maisha. Lakini Lazaro hakuwa na chochote ila matatizo. Sasa yeye anafarijiwa hapa, na wewe unateseka. 26 Pia kuna korongo pana na lenye kina kati yetu sisi na ninyi. Hakuna anayeweza kuvuka kuja kukusaidia na hakuna anayeweza kuja huku kutoka huko.’
27 Tajiri akasema, ‘Basi, nakuomba baba, mtume Lazaro nyumbani kwa baba yangu duniani, 28 Nina ndugu watano. Mtume ili akawape tahadhari wasije wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 Lakini Ibrahimu akasema, ‘Wanayo Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kwa ajili ya kuyasoma; wasikilize na kutii.’
30 Tajiri akasema, ‘Hapana Baba Ibrahimu! Lakini ikiwa mtu kutoka kwa wafu akiwaendea ndipo wataamua kutubu na kubadili maisha yao.’
31 Lakini Ibrahimu akamwambia, ‘Ikiwa ndugu zako hawatawasikiliza Musa na manabii, hawataweza kumsikiliza mtu yeyote kutoka kwa wafu.’”
1 Salamu kutoka kwa Paulo, Mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alitaka. Na Timotheo ndugu yetu katika Kristo.
Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho na kwa watakatifu wote wa Mungu walio jimbo lote la Akaya.
2 Neema na Amani iwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Paulo Anamshukuru Mungu
3 Sifa na zimwendee Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni baba aliyejaa rehema, Mungu aliye mwingi wa faraja. 4 Hutufariji kila wakati tunapokuwa katika hali ya matatizo ili wengine wawapo katika matatizo, tuweze kuwafariji kwa namna ile ile ambayo Mungu ametufariji sisi. 5 Twashiriki katika mateso mengi ya Kristo. Na kwa namna hiyo hiyo, faraja nyingi hutujia kwa njia ya Kristo. 6 Ikiwa tuko katika mateso, tuko kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na ikiwa tunafarijika, ni kwa sababu tuweze kuwafariji ninyi. Hili huwasaidia katika kuyakubali mateso yale yale tunayopata kwa uvumilivu. 7 Tumaini letu kwenu liko imara. Tunafahamu kuwa mnashiriki katika mateso yetu. Hivyo tunafahamu pia kuwa mnashiriki katika faraja yetu pia.
8 Ndugu zangu, tunapenda mfahamu juu ya mateso tuliyoyapata hapa Asia. Tulikuwa na mzigo sana huko, ulikuwa mzito kuliko hata nguvu zetu. Hata tulipoteza tumaini la kuishi. 9 Ukweli ni kuwa, ilionekana kana kwamba Mungu alikuwa anatuambia kuwa tunakwenda kufa. Lakini haya yalitokea ili tusizitumainie nguvu zetu bali tumtumainie Mungu, ambaye huwainua watu toka mautini. 10 Yeye alituokoa toka katika hatari hizi kubwa za mauti, na ataendelea kutuokoa. Twajisikia kuwa na hakika kuwa ataendelea kutuokoa. 11 Nanyi mnaweza kutusaidia kwa njia ya maombi. Ndipo watu wengi wataweza kumshukuru Mungu kwa ajili yetu; kwamba Mungu alitubariki kutokana na maombi yao mengi.
Mabadiliko katika Mipango ya Paulo
12 Hili ndilo tunalojivunia, na naweza kusema kwa dhamiri safi kwamba ni kweli: Katika kila kitu tulichofanya duniani, Mungu ametuwezesha kukifanya kwa moyo safi. Na hili ni kweli zaidi katika yale tuliyowatendea ninyi. Tulifanya hivyo kwa neema ya Mungu, si kwa hekima ambayo ulimwengu unayo. 13 Tunawaandikia mambo mnayoweza kusoma na kuyaelewa. Na nina matumaini kuwa mtayaelewa inavyopasa 14 kama ambavyo tayari mmekwisha kuyafahamu mambo mengi kuhusu sisi. Natumaini mtaelewa kuwa mnaweza kuona fahari juu yetu, kama nasi tutakavyoona fahari juu yenu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja.
15 Nilikuwa na uhakika sana juu ya haya yote. Ndiyo maana niliweka mpango wa kuwatembelea kwanza. Kisha mngebarakikwa mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nilipokuwa nikienda Makedonia na nilipokuwa ninarudi. Na nilipanga kuwaomba mniletee kutoka huko hadi Yudea chochote ambacho nilihitaji kwa ajili ya safari yangu. 17 Je! Mnadhani nilipanga mipango hii bila kufikiri? Au mnadhani ninafanya mipango kama vile dunia inavyofanya, lugha yetu kwenu si ndiyo na hapana kwa wakati mmoja.
18 Kama ambavyo kwa hakika mnaweza kumwamini Mungu, basi mnaweza kuamini kuwa lile tunalowaambia kamwe haliwezi kuwa ndiyo na hapana kwa pamoja. 19 Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, Yeye ambaye Sila, Timotheo, na mimi tuliwaeleza habari zake, hakutokea kuwa ni ndiyo na hapana kwa ahadi za Mungu. Kinyume chake ndiyo ya Mungu imethibitika daima katika Kristo kuwa ni ndiyo. 20 Ndiyo kwa ahadi zote za Mungu katika Kristo. Na hii ndiyo maana twasema “Amina” Katika Kristo kwa utukufu wa Mungu. 21 Na Mungu ndiye anayewafanya ninyi na sisi kuwa imara katika Kristo. Mungu pia ndiye aliyetuchagua kwa ajili ya kazi yake.[b] 22 Aliweka alama yake juu yetu ili kuonesha kuwa tu mali yake. Ndiyo, amemweka roho wake ndani ya mioyo yetu kama malipo ya awali yanayotuhakikishia mambo yote atakayotupa.
23 Ninawaambia hili, na ninamwomba Mungu awe shahidi wangu kuwa ni la kweli: Sababu iliyonifanya nisirudi tena Korintho ni kuwa nilitaka niepuke kuwapa karipio lenye nguvu. 24 Sina maana ya kuwa tunataka kuitawala imani yenu. Ninyi mpo imara katika imani. Lakini tunatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu wenyewe.
© 2017 Bible League International