Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Exod for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yohana 8

Usiku ule Yesu akaenda katika mlima wa Mizeituni. Mapema asubuhi akarudi katika eneo la Hekalu. Watu wengi wakaja kwake, naye akakaa pamoja nao na kuwafundisha.

Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta kwake mwanamke waliyemfumania akizini. Wakamlazimisha asimame mbele ya watu. Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa akifanya zinaa. Sheria ya Musa inatuagiza kumponda kwa mawe mpaka afe mwanamke wa jinsi hiyo. Je, Unasema tufanye nini?”

Watu hao waliyasema haya ili kumtega Yesu. Walitaka kumkamata akisema mambo tofauti ili wapate mashtaka ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama chini na kuanza kuandika kwenye udongo kwa kidole chake. Viongozi wa Kiyahudi waliendelea kumuuliza swali lao hilo. Naye akainuka na kusema, “Yeyote hapa ambaye hajawahi kutenda dhambi awe wa kwanza kumponda jiwe mwanamke huyu.” Kisha Yesu akainama chini tena na kuendelea kuandika katika udongo.

Waliposikia hayo, wale watu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wanaume wazee wakitangulia kwanza, na kisha wengine wakifuata. Wakamwacha Yesu peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10 Kisha Yesu akainua uso wake tena na kumwambia, “Wameenda wapi hao wote? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa una hatia?” 11 Mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja aliyenihukumu, Bwana.”[a]

Kisha Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda sasa, lakini usifanye dhambi tena.”

Yesu ni Nuru ya Ulimwengu

12 Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”

13 Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”

14 Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15 Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18 Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”

19 Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”

Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”

20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa anafundisha katika eneo la Hekalu, karibu na chumba ambamo sadaka za Hekaluni zilitunzwa. Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyemkamata, kwa sababu wakati sahihi wa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika.

Baadhi ya Wayahudi Hawamwelewi Yesu

21 Kwa mara nyingine, Yesu akawaambia watu, “Mimi nitawaacha. Nanyi mtanitafuta, lakini pamoja na hayo mtakufa katika dhambi zenu. Kwani hamuwezi kuja kule niendako.”

22 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakaulizana wenyewe, “Je, atajiua mwenyewe? Je, ndiyo maana alisema, ‘Hamuwezi kuja kule niendako’?”

23 Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi watu ni wa hapa chini, lakini mimi ni wa kule juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, lakini mimi si wa ulimwengu huu. 24 Niliwaambia kwamba mnaweza kufa katika dhambi zenu. Ndiyo, kama hamtaamini kuwa MIMI NDIYE,[b] mtakufa katika dhambi zenu.”

25 Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani?”

Yesu akajibu, “Mimi ni yule niliyekwisha kuwaambia tangu mwanzo kuwa ni nani. 26 Ninayo mengi zaidi ya kusema na ya kuwahukumu. Lakini nawaambia watu yale tu niliyosikia kutoka kwake aliyenituma, naye daima husema kweli.”

27 Wale watu hawakuelewa alikuwa anazungumza habari za nani. Kwani Yeye alikuwa anawaambia habari za Baba. 28 Naye akawaambia, “Mtamwinua juu[c] Mwana wa Adamu. Ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE. Mtajua kuwa lo lote nilifanyalo silifanyi kwa mamlaka yangu. Mtajua kuwa nayasema tu yale Baba yangu aliyonifundisha. 29 Yeye aliyenituma yuko pamoja nami. Siku zote nafanya yale yanayompendeza. Naye hajawahi kuniacha peke yangu.” 30 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, watu wengi wakamwamini.

Yesu Azungumzia Uhuru kutokana na Dhambi

31 Hivyo Yesu akawaambia Wayahudi waliomwamini, “Kama mtaendelea kuyakubali na kuyatii mafundisho yangu, mtakuwa wafuasi wangu wa kweli. 32 Mtaijua kweli, na kweli hiyo itawafanya muwe huru.”

33 Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”

34 Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36 Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. 37 Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. 38 Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.”

39 Wakasema, “Baba yetu ni Ibrahimu.”

Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Ibrahimu kweli, mngefanya yale aliyofanya Ibrahimu. 40 Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Ibrahimu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. 41 Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.”

Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.”

42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. 43 Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. 44 Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo.

45 Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. 46 Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.”

Yesu Azungumza Juu yake na Ibrahimu

48 Wayahudi wakajibu, “Sisi tunasema kuwa wewe ni Msamaria na pepo anakufanya uwe mwendawazimu! Je, hatuko sahihi kusema hivyo?”

49 Yesu akajibu, “Sina pepo ndani yangu. Nampa heshima Baba yangu, lakini ninyi hamnipi heshima. 50 Sijaribu kujitukuza mimi mwenyewe. Yupo mmoja anayetaka kunitukuza. Ndiye hakimu. 51 Nawaahidi, yeyote anayeendelea kutii mafundisho yangu, hatakufa milele.”

52 Wayahudi wakamwambia Yesu, “Sasa tunatambua kuwa una pepo ndani yako! Hata Ibrahimu na manabii walikufa. Lakini unasema, ‘Yeyote anayetii mafundisho yangu, hatakufa kamwe.’ 53 Wewe si mkuu zaidi ya baba yetu Ibrahimu! Yeye alikufa na manabii nao walikufa. Unadhani wewe ni nani?”

54 Yesu akajibu, “Kama ningejipa heshima mwenyewe, heshima hiyo isingelifaa kwa namna yoyote ile. Yule anayenipa mimi heshima ni Baba yangu. Ninyi mnasema kuwa ndiye Mungu wenu. 55 Lakini kwa hakika hamumjui yeye. Mimi namjua. Kama ningesema simjui, basi ningekuwa mwongo kama ninyi. Lakini namjua, na kuyatii anayosema. 56 Baba yenu Ibrahimu alifurahi sana kwamba angeiona siku nilipokuja duniani. Hakika aliiona na akafurahi sana.”

57 Wayahudi wakamwambia Yesu, “Ati nini? Wawezaje kusema ulimwona Ibrahimu? Wewe bado hujafikisha hata umri wa miaka hamsini!”

58 Yesu akajibu, “Ukweli ni kwamba, kabla Ibrahimu hajazaliwa MIMI NIPO.” 59 Aliposema haya, wakachukua mawe ili wamponde. Lakini Yesu akajificha, na kisha akaondoka katika eneo la Hekalu.

Error: Book name not found: Prov for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Wagalatia 4

Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu[a] zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili[b] sisi kama watoto wake.

Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba,[c] yaani Baba.” Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.

Upendo wa Paulo kwa Waamini wa Galatia

Zamani hamkumjua Mungu. Mlikuwa watumwa wa miungu isiyokuwa halisi. Lakini sasa mnamjua Mungu wa kweli. Hakika, Mungu ndiye anayewajua ninyi. Hivyo kwa nini sasa mnavigeukia vikosi dhaifu na visivyo na manufuaa yoyote mlivyovifuata hapo mwanzo? Mnataka kuwa watumwa wa mambo haya tena? 10-11 Inanipa wasiwasi kwa kuwa mnaadhimisha siku, miezi, misimu na miaka. Nina hofu ya kuwa nimefanya kwa bidii kazi bure kwa ajili yenu.

12 Ndugu zangu, naomba mniige mimi kama ambavyo mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunikosea kwa jambo lololote. 13 Mnajua kuwa nilikuja kwenu mara ya kwanza kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Ndipo nilipowaeleza ninyi Habari Njema. 14 Ugonjwa wangu uliwaelemea. Hata hivyo hamkunikataa kutokana na fadhaa ama hofu. Bali, mlinikaribisha kama vile nilikuwa malaika kutoka kwa Bwana. Mlinipokea kama vile nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe! 15 Mlikuwa na furaha sana wakati huo. Nini kimetokea kwa imani yenu ya awali kwamba mimi nilikuwa mtu niliyebarikiwa kipekee na Mungu? Naweza kusema bila shaka yoyote kwamba mngeliweza kufanya kitu chochote kunisaidia. Kama ingeliwezekana, mngeliyang'oa hata macho yenu na kunipa mimi. 16 Je, nimekuwa sasa adui yenu kwa sababu nawaambia ukweli?

17 Watu hawa[d] wanajitahidi sana kuonesha kuvutiwa nanyi,[e] lakini hiyo siyo nzuri kwenu. Wanataka kuwashawishi ninyi ili mtugeuke sisi na kuambatana nao. 18 Inapendeza daima kuwa na mtu anayevutiwa nawe katika jambo lililo jema. Hivyo ndivyo nilivyofanya nilipokuwa pamoja nanyi. Siku zote inapendeza, na si pale tu mimi nikiwapo. 19 Watoto wangu wadogo, nasikia uchungu tena kwa ajili yenu, kama mama anayejifungua. Nitaendelea kusikia uchungu huu mpaka watu watakapofikia kumwona Kristo wawatazamapo ninyi. 20 Natamani ningekuwa nanyi sasa. Ndipo labda ninapoweza kubadilisha namna ninavyoongea nanyi. Sasa sielewi nifanye nini juu yenu.

Mfano wa Hajiri na Sara

21 Baadhi yenu mnataka kuwa chini ya sheria. Niambieni, mnajua sheria inavyosema? 22 Maandiko yanasema kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili. Mama wa mwana mmoja alikuwa ni mjakazi, na mama wa mwana mwingine alikuwa wa mwanamke aliye huru. 23 Mwana wa Ibrahimu kutoka kwa mjakazi alizaliwa kwa namna ya kawaida ya kibinadamu. Lakini mwana kutoka kwa mwanamke aliyekuwa huru alizaliwa kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.

24 Habari hii ina maana nyingine kwenu. Wanawake wawili ni sawa na maagano mawili baina ya Mungu na watu wake. Agano moja ni sheria ambayo Mungu aliifanya katika Mlima Sinai, inayowafanya watu wawe watumwa. Mwanamke aliyeitwa Hajiri yuko kama agano la kwanza. 25 Hivyo Hajiri anauwakilisha Mlima Sinai uliopo Arabia. Na anafanana na Yerusalemu wa sasa, kwa sababu mji huu uko utumwani pamoja na watu wake. 26 Lakini Yerusalemu ya mbinguni ulio juu uko kama mwanamke aliye huru, ambaye ndiye mama yetu. 27 Maandiko yanasema,

“Ufurahi mwanamke, wewe uliye tasa.
    Ufurahi kwani hukuwahi kuzaa.
Piga kelele na ulie kwa furaha!
    Hukupata uchungu wa kuzaa.
Mwanamke aliye peke yake atapata watoto zaidi
    zaidi ya mwanamke aliye na mume.”(A)

28 Ndugu zangu, ninyi ni watoto mliozaliwa kwa sababu ya ahadi ya Mungu, kama Isaka alivyozaliwa. 29 Lakini mwana mwingine wa Ibrahimu, aliyezaliwa kwa njia ya kawaida, alisababisha matatizo kwa yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho. Ndivyo ilivyo leo. 30 Lakini Maandiko yanasemaje? “Mfukuze mjakazi na mwanawe! Mwana wa mwanamke aliye huru atapokea kila kitu alicho nacho baba yake, lakini mwana wa mjakazi hatapokea kitu.”(B) 31 Hivyo, kaka na dada zangu, sisi si watoto wa mjakazi. Ni watoto wa mwanamke aliye huru.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International