M’Cheyne Bible Reading Plan
Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli
(Mk 12:41-44)
21 Yesu alitazama na kuwaona matajiri wakimtolea Mungu sadaka zao katika sanduku la sadaka ndani ya Hekalu. 2 Kisha akamwona mjane maskini akiweka sarafu mbili za shaba kwenye sanduku. 3 Akasema, “Mjane huyu maskini ametoa sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kuwa, ametoa zaidi ya hao matajiri wote. 4 Wale wanavyo vingi, na wametoa vile ambavyo hawavihitaji. Lakini mwanamke huyu ni maskini sana, lakini ametoa vyote alivyokuwa akitegemea ili aishi.”
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mt 24:1-14; Mk 13:1-13)
5 Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao.
6 Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.”
7 Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?”
8 Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. 9 Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.”
10 Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. 11 Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu.
12 Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. 13 Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. 14 Msihofu namna mtakavyojitetea, 15 Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. 16 Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na marafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. 17 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. 18 Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 19 Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote.
Kuharibiwa Kwa Mji wa Yerusalemu
(Mt 24:15-21; Mk 13:14-19)
20 Mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu, ndipo mtajua kuwa wakati wa kuharibiwa kwake umefika. 21 Watu walioko katika Uyahudi wakati huo wakimbilie milimani. Mtu yeyote atakaye kuwa Yerusalemu wakati huo aondoke haraka. Ikiwa utakuwa karibu na mji, usiingie mjini! 22 Manabii waliandika mambo mengi kuhusu wakati ambao Mungu atawaadhibu watu wake. Wakati ninaouzungumzia ni wakati ambao mambo haya yote lazima yatokee. 23 Wakati huu utakuwa mgumu kwa wanawake wenye mimba au wanaonyonyesha watoto wadogo, kwa sababu mambo mabaya yatakuja katika nchi hii. Mungu atawaadhibu watu wake kwa sababu wamemkasirisha. 24 Baadhi ya watu watauawa, wengine watafanywa watumwa na kuchukuliwa katika nchi mbalimbali. Mji mtakatifu wa Yerusalemu utatekwa na kuwekwa chini ya utawala wa wageni mpaka wakati ulioruhusiwa wao kufanya hivi utakapokwisha.
Msiogope
(Mt 24:29-31; Mk 13:24-27)
25 Mambo ya kushangaza yatatokea kwenye jua, mwezi na nyota na watu katika dunia yote wataogopa na kuchanganyikiwa kutokana na kelele za bahari na mawimbi yake. 26 Watazimia kwa hofu na kuogopa watakapoona mambo yanayoupata ulimwengu. Kila kitu katika anga kitabadilishwa. 27 Kisha watu watamwona Mwana wa Adamu akija katika wingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28 Mambo haya yakianza kutokea, simameni imara na msiogope. Jueni kuwa wakati wa Mungu kuwaweka huru umekaribia!”
Maneno Yangu Yataishi Milele
(Mt 24:32-35; Mk 13:28-31)
29 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. 30 Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. 31 Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja.
32 Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. 33 Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele.
Kuweni Tayari Wakati Wote
34 Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. 35 Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. 36 Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.”
37 Wakati wa mchana Yesu aliwafundisha watu katika eneo la Hekalu. Usiku alitoka nje ya mji na kukaa usiku kucha kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. 38 Kila asubuhi watu wote waliamka mapema kwenda kumsikiliza Yesu katika Hekalu.
6 Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu. Hivyo tunawasihi: Neema mliyoipokea kutoka kwa Mungu iwe na manufaa kwenu. 2 Mungu anasema,
“Nilikusikia kwa wakati sahihi,
na nikakusaidia siku ya wokovu.”(A)
Ninawaambia kwamba “wakati uliokubalika” ni huu sasa. Na “Siku ya wokovu” ni leo.
3 Hatutaki watu waone makosa katika kazi yetu. Hivyo hatutendi jambo lolote litakalokuwa kikwazo kwa wengine. 4 Lakini kwa kila njia tunaonesha kuwa sisi ni watumishi wa Mungu. Hatukati tamaa, ingawa tunakutana na matatizo, mambo magumu na matatizo ya kila namna. 5 Tumepigwa na kutupwa gerezani. Watu wameanzisha fujo dhidi yetu. Tumefanya kazi kwa bidii, mara nyingi pasipo kula ama kulala. 6 Tunadhihirisha kuwa sisi tu watumishi wa Mungu kutokana na maisha yetu safi, kwa ufahamu wetu, kwa subira yetu na kwa upole wetu. Tunadhihirisha hilo kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo wetu wa kweli, 7 kwa kusema iliyo kweli, na kwa kuzitegemea nguvu za Mungu. Njia hii iliyo sahihi ya kuishi imetuandaa kujitetea wenyewe kinyume na kila aina ya shambulizi.
8 Baadhi ya watu wanatuheshimu, lakini wengine wanatudhihaki. Wengine wanasema mema juu yetu, lakini wengine wasema mabaya juu yetu. Wengine wanatusema kuwa tu waongo, lakini tunasema kweli. 9 Kwa wengine hatufahamiki, lakini twajulikana sana. Tunaonekana kama watu wanaostahili kufa, lakini angalia! Twadumu kuishi. Tunaadhibiwa, lakini hatuuawi. 10 Tuna huzuni nyingi, lakini tunafuraha kila siku. Tu maskini, lakini tunawafanya watu wengi kuwa matajiri katika imani. Hatuna kitu, lakini tunakila kitu.
11 Tumesema kwa uhuru kwenu ninyi watu wa Korintho. Tumefungua mioyo yetu kwenu. 12 Upendo wetu kwenu haujakoma. Ninyi ndiyo mliouzuia upendo wenu kwetu. 13 Ninawaambia kama watoto wangu. Fanyeni vivyo hivyo kama sisi tulivyotenda kwenu; fungueni mioyo yenu pia.
Sisi ni Hekalu la Mungu
14 Ninyi hamko sawa na wale wasioamini. Hivyo msifungwe nira pamoja nao. Wema na ubaya havikai pamoja. Nuru na giza haviwezi kukaa pamoja katika chumba kimoja. 15 Itawezekanaje kuwe na mapatano kati ya Kristo na beliali?[a] Je, mwamini anashirika gani na asiye amini? 16 Hekalu la Mungu halina mapatano yoyote na sanamu, na sisi tu hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu anavyosema,
© 2017 Bible League International