M’Cheyne Bible Reading Plan
Mchungaji na Kondoo Wake
10 Yesu akawaambia, “Hakika ninawaambia, mtu anapoingia katika zizi la kondoo, hutumia mlango. Kama akiingia kwa kutumia njia nyingine yoyote, huyo ni mwizi. Anajaribu kuwaiba kondoo. 2 Lakini mtu anayewachunga kondoo hupitia mlangoni. Yeye ndiye mchungaji. 3 Mtu anayelinda mlangoni humfungulia mlango mchungaji. Na kondoo huisikiliza sauti ya mchungaji wao. Naye huwaita kondoo wake mwenyewe kwa majina yao, na huwaongoza kwenda nje. 4 Mchungaji huwatoa nje kondoo wake wote. Kisha huwatangulia mbele na kuwaongoza. Kondoo nao humfuata, kwa sababu wanaifahamu sauti yake. 5 Lakini kamwe kondoo hawatamfuata wasiyemfahamu. Bali watamkimbia, kwa sababu hawaifahamu sauti yake.”
6 Yesu aliwaambia watu habari hii, lakini hawakuelewa ilikuwa ina maana gani.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. 18 Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.”
19 Kwa mara nyingine tena Wayahudi wakagawanyika juu ya yale aliyoyasema Yesu. 20 Wengi wao wakasema, “Pepo mchafu amemwingia na kumfanya awe mwendawazimu. Kwa nini sisi tumsikilize?”
21 Lakini wengine wakasema, “Haya siyo maneno ya mtu anayeendeshwa na pepo mchafu. Pepo mchafu hawezi kuponya macho ya mtu asiyeona.”
Viongozi wa Kiyahudi Wasimama Kinyume na Yesu
22 Ulikuwa ni wakati wa baridi, na wakati wa Sikukuu ya Kuweka Wakfu[b] kule Yerusalemu. 23 Yesu alikuwa katika eneo la Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani. 24 Viongozi wa Kiyahudi wakakusanyika kumzunguka. Wakasema, “Ni mpaka lini utatuacha na mashaka juu yako? Kama wewe ndiwe Masihi, basi tuambie wazi wazi.”
25 Yesu akajibu, “Nilikwisha kuwaambia tayari, lakini hamkuamini. Nafanya miujiza katika jina la Baba yangu. Miujiza hii inaonesha mimi ni nani. 26 Lakini hamuamini, kwa sababu ninyi siyo kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu. Nami nawajua, nao hunifuata. 28 Mimi nawapa kondoo wangu uzima wa milele. Nao hawatakufa kamwe, na tena hakuna atakayemchukua yeyote kutoka mkononi mwangu. 29 Baba yangu ndiye aliyenipa hao, naye ni mkuu kuliko wote.[c] Hakuna anayeweza kuwaiba kondoo wangu kutoka mkononi mwangu. 30 Mimi na Baba tu umoja.”
31 Kwa mara nyingine Wayahudi pale wakaokota mawe ili wamuue Yesu. 32 Lakini Yeye akawaambia, “Mambo mengi mliyoyaona nikiyatenda yanatoka kwa Baba. Ni kwa mambo gani miongoni mwa hayo mazuri mnataka kuniua?”
33 Wakajibu, “Hatukuui kwa ajili ya jambo lo lote zuri ulilofanya. Lakini wewe unasema mambo yanayomkufuru Mungu! Wewe ni mtu tu, lakini unasema uko sawa na Mungu! Ndiyo sababu tunataka kukuua!”
34 Yesu akajibu, “Imeandikwa katika sheria yenu kuwa Mungu alisema, ‘Nilisema ninyi ni miungu.’(A) 35 Maandiko yaliwaita watu hawa miungu; watu waliopokea ujumbe wa Mungu. Na Maandiko siku zote ni ya kweli. 36 Sasa kwa nini mnanilaumu mimi kwa kumkufuru Mungu kwa kusema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’? 37 Lakini kama sitafanya yale anayoyatenda Baba yangu, basi msiamini ninayosema. 38 Lakini kama nafanya anayofanya Baba, mnapaswa kuyaamini ninayoyafanya. Mnaweza msiniamini mimi, lakini muamini yale ninayotenda. Ndipo mtakapofahamu na kuelewa kwamba Baba yumo ndani yangu nami nimo ndani ya Baba.”
39 Walijaribu kumkamata Yesu tena, lakini yeye akawatoroka.
40 Kisha akarejea tena kwa kuvuka Mto Yordani hadi sehemu ambapo Yohana alipoanzia kazi ya kubatizia watu. Yesu akakaa huko, 41 na watu wengi wakaja kwake. Wakasema, “Yohana hakutenda ishara na miujiza yoyote, lakini kila alichosema kuhusu mtu huyu ni kweli!” 42 Na watu wengi huko wakamwamini Yesu.
Tuishi kwa Kusaidiana Sisi kwa Sisi
6 Ndugu zangu, ikiwa mmoja wenu atakosea, ninyi mnaomfuata Roho mnapaswa kumwendea yule anayetenda dhambi. Msaidieni mtu huyo awe mwenye haki tena. Mfanye hivyo kwa njia ya upole, na muwe waangalifu, kwa maana nanyi pia mnaweza kujaribiwa kutenda dhambi. 2 Msaidiane ninyi kwa ninyi katika kubeba mizigo yenu. Mnapofanya hivi, mtakuwa mnatimiza yote ambayo sheria ya Kristo imewaagiza kufanya. 3 Maana mtu akijiona kuwa yeye ni wa muhimu sana na kumbe sio wa muhimu, anajidanganya mwenyewe. 4 Kila mmoja aipime kazi yake mwenyewe kuona ikiwa kuna chochote cha kujivunia. Kama ndivyo, uyatunze hayo moyoni mwako wala usijilinganishe na mtu mwingine yeyote. 5 Maana sisi sote tunawajibika kwa yale tunayofanya.
Msiache Kutenda Mema
6 Yule anayefundishwa neno la Mungu anapaswa kumshirikisha mwalimu wake mambo mema aliyonayo.
7 Ikiwa mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu, mtakuwa mnajidanganya wenyewe. Mtavuna yale mnayopanda. 8 Yule anayepanda kwa kuiridhisha nafsi yake ya dhambi, mavuno yatakayopatikana ni uharibifu kabisa. Lakini mkipanda kwa kuiridhisha Roho, mavuno yenu katika Roho yatakuwa uzima wa milele. 9 Hatupaswi kuchoka katika kutenda mema. Tutapata mavuno yetu kwa wakati sahihi, tusipokata tamaa. 10 Tunapokuwa na nafasi ya kumtendea mema kila mtu, tufanye hivyo. Lakini tuzingatie zaidi kuwatendea mema wale walio wa familia ya waamini.
Paulo Amalizia Barua Yake
11 Huu ni mwandiko wa mkono wangu mwenyewe. Mnaweza kuona jinsi herufi zilivyo kubwa.[a] 12 Watu wale wanaojaribu kuwalazimisha ninyi kutahiriwa wanafanya hivyo ili wawaridhishe Wayahudi wenzao. Wanaogopa wasije wakateswa kwa sababu ya msalaba[b] wa Kristo. 13 Maana hata wale waliotahiriwa hawaitii sheria. Na bado wanawataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujisifu kwa ajili ya yale waliyowatendea ninyi.
14 Mimi nisijisifu kwa ajili ya mambo kama haya. Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo sababu pekee ya kujivuna kwangu. Kupitia kifo cha Yesu msalabani ulimwengu ukafa[c] kwangu, nami nimeufia ulimwengu. 15 Haijalishi kwamba mtu ametahiriwa au hajatahiriwa. Kinachojalisha ni uumbaji mpya wa Mungu katika Kristo.[d] 16 Amani iwe kwa wale wote wanaoifuata njia hii mpya. Na rehema za Mungu ziwe juu ya watu wake Israeli.
17 Kwa hiyo msinitaabishe kwa namna yoyote. Nina makovu mwilini mwangu yanayoonyesha[e] kuwa mimi ni wa Yesu.
18 Ndugu na dada zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.
© 2017 Bible League International