Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Exod for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yohana 9

Yesu Amponya Aliyezaliwa Pasipo Kuwa na Uwezo wa Kuona

Yesu alipokuwa anatembea, alimwona mtu asiyeona tangu alipozaliwa. Wafuasi wake wakamwuliza, “Mwalimu, kwa nini mtu huyu alizaliwa asiyeona? Dhambi ya nani ilifanya hili litokee? Ilikuwa ni dhambi yake mwenyewe au ya wazazi wake?” Yesu akajibu, “Si dhambi yoyote ya huyo mtu wala ya wazazi wake iliyosababisha awe asiyeona. Alizaliwa asiyeona ili aweze kutumiwa kuonesha mambo makuu ambayo Mungu anaweza kufanya. Kukiwa bado ni mchana, tunapaswa kuendelea kuzifanya kazi zake Yeye aliyenituma. Usiku unakuja, na hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi wakati wa usiku. Nikiwa bado nipo ulimwenguni, mimi ndiye nuru ya ulimwengu.”

Yesu aliposema haya, akatema mate chini kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka yule asiyeona katika macho yake. Yesu akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni “Aliyetumwa”.) Hivyo mtu yule akaenda katika bwawa lile, akanawa na kurudi akiwa mwenye kuona.

Majirani zake na wengine waliomwona akiomba omba wakasema, “Angalieni! Hivi huyu ndiye mtu yule aliyekaa siku zote na kuomba omba?”

Wengine wakasema, “Ndiyo! Yeye ndiye.” Lakini wengine wakasema, “Hapana, hawezi kuwa yeye. Huyo anafanana naye tu.”

Kisha yule mtu akasema, “Mimi ndiye mtu huyo.”

10 Wakamwuliza, “Kulitokea nini? Uliwezaje kupata kuona?”

11 Akawajibu, “Mtu yule wanayemwita Yesu alitengeneza tope akayapaka macho yangu. Kisha akaniambia ‘Nenda kanawe kwenye bwawa la Siloamu.’ Hivyo nikaenda kule na kunawa, na ndipo nikaweza kuona.”

12 Wakamwuliza, “Yuko wapi mtu huyo?”

Akajibu, “Mimi sijui aliko.”

Baadhi ya Mafarisayo Wana Maswali

13 Kisha watu wakampeleka huyo mtu kwa Mafarisayo. 14 Siku Yesu alipotengeneza yale matope na kuyaponya macho ya mtu huyo ilikuwa ni Sabato. 15 Hivyo Mafarisayo wakamwuliza huyo mtu, “Uliwezaje kuona?”

Akawajibu, “Alipaka matope katika macho yangu. Nikaenda kunawa, na sasa naweza kuona.”

16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyo mtu hatii sheria inayohusu siku ya Sabato. Kwa hiyo hatoki kwa Mungu.”

Wengine wakasema, “Lakini mtu aliye mtenda dhambi hawezi kufanya ishara kama hizi?” Hivyo hawakuelewana wao kwa wao. 17 Wakamuuliza tena huyo mtu, “Kwa vile aliponya macho yako, unasemaje juu ya mtu huyo?”

Akajibu, “Yeye ni nabii.” 18 Viongozi wa Kiyahudi walikuwa bado hawaamini kwamba haya yalimtokea mtu huyo; kwamba alikuwa haoni na sasa ameponywa. Lakini baadaye wakawaita wazazi wake. 19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mwana wenu? Mnasema alizaliwa akiwa haoni. Sasa amewezaje kuona?”

20 Wazazi wake wakajibu, “Tunafahamu kwamba mtu huyu ni mwana wetu. Na tunajua kuwa alizaliwa akiwa asiyeona. 21 Lakini hatujui kwa nini sasa anaweza kuona. Hatumjui aliyeyaponya macho yake. Muulizeni mwenyewe. Yeye ni mtu mzima anaweza kujibu mwenyewe.” 22 Walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Kiyahudi. Viongozi walikwisha azimia kwamba, wangemwadhibu mtu yeyote ambaye angesema Yesu alikuwa Masihi. Wangewazuia hao wasije tena kwenye sinagogi. 23 Ndiyo maana wazazi wake walisema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni yeye!”

24 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakamwita yule aliyekuwa haoni. Wakamwambia aingie ndani tena. Wakasema, “Unapaswa kumheshimu Mungu na kutuambia ukweli. Tunamjua mtu huyu kuwa ni mtenda dhambi.”

25 Yule mtu akajibu, “Mimi sielewi kama yeye ni mtenda dhambi. Lakini nafahamu hili: Nilikuwa sioni, na sasa naweza kuona!”

26 Wakawuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyaponyaje macho yako?”

27 Akajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia hayo. Lakini hamkutaka kunisikiliza. Kwa nini mnataka kusikia tena? Mnataka kuwa wafuasi wake pia?”

28 Kwa hili wakampigia makelele na kumtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake, siyo sisi! Sisi ni wafuasi wa Musa. 29 Tunafahamu kwamba Mungu alisema na Musa. Lakini wala hatujui huyu mtu anatoka wapi!”

30 Yule mtu akajibu, “Hili linashangaza kweli! Hamjui anakotoka, lakini aliyaponya macho yangu. 31 Wote tunajua kuwa Mungu hawasikilizi watenda dhambi, bali atamsikiliza yeyote anayemwabudu na kumtii. 32 Hii ni mara ya kwanza kuwahi kusikia kwamba mtu ameponya macho ya mtu aliyezaliwa asiyeona. 33 Hivyo lazima anatoka kwa Mungu. Kama asingetoka kwa Mungu, asingefanya jambo lolote kama hili.”

34 Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ulizaliwa ukiwa umejaa dhambi. Unataka kutufundisha sisi?” Kisha wakamwambia atoke ndani ya sinagogi na kukaa nje.

Kutoona Kiroho

35 Yesu aliposikia kuwa walimlazimisha huyo mtu kuondoka, alikutana naye na kumuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”

36 Yule mtu akajibu, “Niambie ni nani huyo, bwana, ili nimwamini.” 37 Yesu akamwambia, “Umekwisha kumwona tayari. Mwana wa Adamu ndiye anayesema nawe sasa.”

38 Yule mtu akajibu, “Ndiyo, ninaamini, Bwana!” Kisha akainama na kumwabudu Yesu.

39 Yesu akasema, “Nilikuja ulimwenguni ili ulimwengu uweze kuhukumiwa. Nilikuja ili wale wasiyeona waweze kuona. Kisha nilikuja ili wale wanaofikiri wanaona waweze kuwa wasiyeona.”

40 Baadhi ya Mafarisayo walikuwa karibu na Yesu. Wakamsikia akisema haya. Wakamwuliza, “Nini? Unasema sisi pia ni wale wasiyeona?”

41 Yesu akasema, “Kama mngekuwa wasiyeona hakika, msingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini kwa kuwa mnasema mnaona, basi bado mngali na hatia.”

Error: Book name not found: Prov for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Wagalatia 5

Utunzeni Uhuru Wenu

Sasa tuko huru, kwa sababu Kristo alituweka huru ili tuweze kuishi tukiufurahia uhuru huo. Hivyo muwe imara katika uhuru huo. Msimruhusu mtu yeyote awaingize utumwani tena. Sikilizeni! Mimi Paulo nawaambia kwamba ikiwa mtakubali kutahiriwa, basi Kristo hatakuwa na manufaa kwenu. Tena, ninamwonya kila mtu atakayeruhusu atahiriwe, kwamba akifanya hivyo itampasa aifuate sheria yote. Ikiwa utajaribu kufanyika mwenye haki mbele za Mungu kwa njia ya sheria, maisha yako na Kristo yamepotea, kwani umeiacha neema ya Mungu. Ninasema hivi kwa sababu tumaini letu la kufanywa wenye haki mbele za Mungu huja kwa imani. Na kwa nguvu ya Roho kwa njia ya imani, tunangoja kwa utulivu na kwa matumaini yenye ujasiri hukumu ya Mungu inayotuweka huru. Mtu anapokuwa wa Kristo Yesu, vyote kutahiriwa ama kutotahiriwa havina nguvu ya kuleta manufaa yoyote. Lakini kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu imani inatenda kazi kupitia upendo.

Mlikuwa mnapiga mbio vizuri sana. Ni nani aliyewafanya mkaacha kuitii kweli? Hakika hakuwa yule aliyewachagua. Mjihadhari! “Chachu ndogo tu hufanya mkate wote mzima uumuke.”[a] 10 Nimeridhika moyoni mbele za Bwana kuwa hamtafikiri vinginevyo. Mtu yule anayewasumbua atahukumiwa hata angekuwa nani?

11 Kaka na dada zangu, sifundishi kuwa ni lazima mwanaume atahiriwe. Kama nitaendelea kuwafundisha wanaume watahiriwe, kwa nini watu bado wanaendelea kunitesa? Ikiwa bado nafundisha tohara, basi ujumbe wangu kuhusu msalaba hautaendelea kuwa tatizo. 12 Natamani watu hao wanaowasumbua wangeongeza na kuhasi[b] juu ya tohara yao.

13 Ndugu na dada zangu, Mungu aliwaita ili muwe huru. Lakini msiutumie uhuru wenu kama udhuru wa kutimiza yale yote mnayoyapenda, badala yake, msaidiane ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Sheria yote imepewa muhtasari katika amri hii moja tu, “Mpende jirani yako[c] kama unavyojipenda mwenyewe.”(A) 15 Ikiwa mtaendelea kuumizana na kuraruana, muwe waangalifu, vinginevyo mtaangamizana ninyi kwa ninyi.

Roho na Asili ya Kibinadamu

16 Hivyo ninawaambieni, ishini kama Roho anavyowaongoza. Hapo hamtatenda dhambi kutokana na tamaa zenu mbaya. 17 Utu wenu wa dhambi unapenda yale yaliyo kinyume cha Roho, na Roho anataka yale yaliyo kinyume na utu wa dhambi. Hao siku zote hushindana wao kwa wao. Kwa jinsi hiyo ninyi hamko huru kufanya chochote mnachotaka kufanya. 18 Lakini mkimruhusu Roho awaongoze, hamtakuwa chini ya sheria.[d]

19 Mambo mabaya yanayofanywa na mwili wa dhambi ni dhahiri: uasherati, tabia chafu, kufanya mambo yenye kuleta aibu, 20 kuabudu miungu wa uongo, kushiriki mambo ya uchawi, kuwachukia watu, kuanzisha mafarakano, kuwa na wivu, hasira ama choyo, kusababisha mabishano na kujigawa kimakundi na kuwatenga wengine, 21 kujawa na husuda, kulewa pombe, kushiriki karamu zenye ulafi na uasi mwingi na kufanya mambo yanayofanana na hayo. Ninawatahadharisha mapema kama nilivyowatahadharisha mwanzo: Watu wanaofanya mambo hayo hawatahesabiwa kama watoto watakaourithi ufalme wa Mungu. 22 Lakini tunda linalozaliwa na Roho katika maisha ya mtu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, na kiasi. Hakuna sheria juu ya mambo kama haya. 24 Wale walio wa Kristo Yesu wameusulubisha udhaifu wao wa kibinadamu pamoja na tamaa zake za dhambi na zile za mwili. Wameachana na utu wao wa kale wenye hisia za ubinafsi na uliotaka kufanya mambo maovu. 25 Tunayapata maisha yetu mapya kutoka kwa Roho, hivyo tunapaswa kuufuata uongozi wa Roho. 26 Tusijivune na kujisifu juu yetu wenyewe. Hatupaswi kuchokozana kwa mashindano baina yetu ama kuoneana wivu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International