Book of Common Prayer
13 Ikiwa unajaribu kwa bidii kutenda mema, ni nani atakayetaka kukudhuru? 14 Lakini hata ukiteseka kwa sababu kutenda yaliyo haki, unazo Baraka za Mungu. “Msimwogope mtu yeyote, wala msiruhusu watu wawasumbue.”(A) 15 Lakini mjitoe kikamilifu kwa Kristo ambaye ni Bwana wenu pekee. Na daima iweni tayari kumjibu mtu yeyote anayetaka ufafanuzi kuhusu tumaini linaloyaongoza maisha yenu.[a] 16 Lakini wajibuni kwa upole na heshima kwa ajili ya Mungu, mkizitunza dhamiri zenu mbele zake. Ndipo watu watakapoona namna njema mnayoishi kama wafuasi wa Kristo. Na wataaibika kwa kuwanenea mabaya.
17 Ni afadhali kuteseka kwa kutenda mema kuliko kutenda mabaya. Ndiyo, ni bora ikiwa hivyo ndivyo Mungu anavyotaka.
18 Kristo mwenyewe aliteseka alipokufa kwa ajili yenu,
na kwa kifo hicho kimoja alilipa fidia kwa ajili ya dhambi.
Hakuwa na hatia,
lakini alikufa kwa ajili ya watu waliokuwa na hatia.
Alifanya hivyo ili awalete ninyi nyote kwa Mungu.
Kama mwanadamu, aliuawa,
lakini uhai wake ulifanywa hai na Roho.[b]
19 Na kwa Roho alikwenda akazihubiri roho zilizo kifungoni. 20 Hizo ndizo roho zilizokataa kumtii Mungu hapo zamani wakati wa Nuhu. Mungu alisubiri kwa uvumilivu Nuhu alipokuwa anaunda safina. Na watu wachache tu, yaani wanane kwa jumla ndiyo walioingia katika safina na kuokolewa kwa kuvushwa salama katika gharika hiyo. 21 Na maji yale ni kama ubatizo, unaowaokoa ninyi sasa kupitia ufufuo wa Yesu Kristo kutoka katika wafu na siyo kuondoa uchafu mwilini kwa kuoga. Ni ahadi ya dhati ya kuishi kwa kumcha Mungu. 22 Sasa yupo mbinguni upande wa kuume wa Mungu, na anatawala juu ya malaika, mamlaka na nguvu.
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)
21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. 2 Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[a] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. 3 Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”
4 Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:
5 “Waambie watu wa Sayuni,[b]
‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(A)
6 Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. 7 Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. 8 Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. 9 Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:
“Msifuni[c] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
ajaye katika jina la Bwana!’(B)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”
10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”
11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mk 11:15-19; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)
12 Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. 13 Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’(C) Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’.(D)”
© 2017 Bible League International