Book of Common Prayer
Mpanda Farasi Juu ya Farasi Mweupe
11 Kisha nikaona mbingu zimefunguka, na nikamwona farasi mweupe. Mpanda farasi aliitwa Mwaminifu na Kweli, kwa sababu ni wa haki katika maamuzi yake na kufanya vita. 12 Macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Alikuwa na taji nyingi kichwani mwake. Jina lilikuwa limeandikwa juu yake, lakini yeye peke yake ndiye aliyejua maana ya jina hilo. 13 Alivaa vazi lililochovywa katika damu, na aliitwa Neno la Mungu. 14 Majeshi ya mbinguni yalikuwa yanamfuata mpanda farasi mweupe. Walikuwa wanaendesha farasi weupe pia. Walikuwa wamevaa kitani nzuri, nyeupe na safi. 15 Upanga mkali ulikuwa unatoka kwenye kinywa chake, upanga ambao angeutumia kuyashinda mataifa. Na atayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Atazikanyaga zabibu katika shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenye Nguvu. 16 Kwenye vazi lake na kwenye mguu wake alikuwa ameandikwa jina lake:
mfalme wa wafalme na bwana wa mabwana.
17 Kisha nikaona malaika amesimama katika jua. Kwa sauti kuu malaika akawaambia ndege wote wanaoruka angani, “Kusanyikeni kwa ajili ya karamu kuu ya Mungu. 18 Kusanyikeni mle miili ya watawala, majemadari na watu maarufu. Njooni mle miili ya farasi na wanaowapanda na miili ya watu wote, walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”
19 Kisha nikamwona mnyama na watawala wa dunia. Majeshi yao yalikusanyika pamoja ili kufanya vita kupigana na mpanda farasi mweupe na jeshi lake. 20 Lakini mnyama na nabii wa uongo walikamatwa. Nabii wa uongo ndiye aliyefanya miujiza[a] kwa ajili ya mnyama. Alitumia miujiza hii kuwahadaa wale waliokuwa na alama ya mnyama na walioabudu sanamu yake. Nabii wa uongo na mnyama walitupwa kwenye ziwa la moto linalowaka kwa baruti. 21 Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kwenye kinywa cha mpanda farasi. Ndege wote walikula miili hii mpaka wakashiba.
Furaha Mbinguni
(Mt 18:12-14)
15 Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. 2 Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu[a] huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!”
3 Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, 4 “Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. 5 Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako 6 mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ 7 Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika.
8 Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha,[b] lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. 9 Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ 10 Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.”
© 2017 Bible League International