Book of Common Prayer
Uwe Mstahimilivu
7 Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli.[a] 8 Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. 9 Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani.
10 Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia. 11 Na tunatoa heshima kubwa sana kwa wale wote waliostahimili mateso. Mmesikia juu ya uvumilivu wa Ayubu,[b] na mnayajua ya kuwa baada ya yote hayo Bwana alimsaidia. Hii basi inaonesha ya kuwa Bwana ni mwenye wingi wa rehema na huruma.
Uwe Makini na Unayosema
12 Juu ya mambo yote kaka zangu na dada zangu, usitumie kiapo unapotoa ahadi, Usiape kwa mbingu wala kwa dunia, ama kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo halisi”, na “Hapana” yenu na iwe “Hapana halisi”, ili msije mkaingia katika hukumu ya Mungu.
Mungu Atawajibu Watu Wake
18 Kisha Yesu akawafundisha wafuasi wake kwamba wanapaswa kuomba daima bila kupoteza tumaini. Akatumia simulizi hii kuwafundisha. 2 Akasema, “Kulikuwa na mwamuzi katika mji fulani. Hakumcha Mungu wala hakujali watu walikuwa wanamfikiriaje. 3 Na katika mji huo huo alikuwepo mwanamke mjane. Huyu alimjia mwamuzi huyu mara nyingi akimwambia, ‘Kuna mtu anayenitendea mambo mabaya. Nipe haki yangu!’ 4 Mwanzoni mwamuzi hakutaka kumsaidia yule mwanamke. Lakini baada ya muda kupita, akawaza moyoni mwake yeye mwenyewe, ‘Simchi Mungu. Na sijali watu wananifikiriaje. 5 Lakini mwanamke huyu ananisumbua. Nikimpa haki yake ataacha kunisumbua. Nisipomsaidia, ataendelea kunijia na anaweza kunishambulia.’”
6 Bwana akasema, “Sikilizeni, maneno aliyosema mwamuzi mbaya yana mafundisho kwa ajili yenu. 7 Daima Mungu atawapa mahitaji yao wateule wanaomwomba usiku na mchana. Hatachelewa kuwajibu. 8 Ninawaambia, Mungu atawapa haki yao watu wake haraka. Lakini Mwana wa Adamu atakaporudi, atawakuta duniani watu ambao bado wanamwamini?”
© 2017 Bible League International