Book of Common Prayer
Kuyamudu Mambo Tunayosema
3 Kaka na dada zangu, msiwe walimu wengi miongoni mwenu. Mnajua kuwa sisi tulio walimu tutahukumiwa zaidi tena kwa umakini kweli.
2 Ninawatahadharisha kwa sababu sote tunakosa mara kwa mara. Na kama kuna mtu asiyekosa kwa maneno yake, huyo ni mkamilifu, huyo anaweza kuumudu mwili wake wote. 3 Tunawaweka lijamu katika midomo ya farasi, ili waweze kututii sisi. Kwa lijamu hizo tunaweza kuidhibiti miili yao. 4 Au tuchukue meli kama mfano: Hata kama ni kubwa mno na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana na kwenda po pote alikokusudia nahodha kuipeleka. 5 Kwa jinsi hiyo hiyo, ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini unaweza kujivuna kuwa umetenda mambo makubwa sana.
Fikiri jinsi ambavyo msitu mkubwa unaweza kuwashwa moto kwa mwali mdogo tu! 6 Ndiyo, ulimi ni mwali wa moto. Ulimi unawakilisha ulimwengu wa uovu miongoni mwa viungo vya mwili wetu. Ulimi huo huo huuchafua mwili wote, na unaweza kuwasha moto maisha yote ya mtu. Nao unapata moto wake kutoka Jehanamu.
7 Aina zote za wanyama na ndege, mijusi na viumbe vya baharini wanaweza kufugwa na wanadamu wamekuwa wanawafuga. 8 Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia na umejaa sumu ya kuua. 9 Kwa ulimi huo tunambariki Bwana na Baba, na kwa huo huo tunawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu! 10 Kutoka katika kinywa hicho hicho hutoka baraka na laana. Kaka na dada zangu, haipaswi kuwa hivyo. 11 Chemichemi ya maji haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu kutoka katika tundu moja, je inawezekana? 12 Ndugu zangu, je mtini unaweza kuzaa zeituni? Au mzabibu waweza kuzaa tini? Kwa hakika haiwezekani! Wala chemichemi ya maji chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
Dhambi na Msamaha
(Mt 18:6-7,21-22; Mk 9:42)
17 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi yatatokea hakika. Lakini ole wake mtu anayesababisha hili litokee. 2 Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama jiwe la kusagia lingefungwa shingoni mwake, na akatupwa baharini, kuliko kusababisha mmojawapo wa wanyenyekevu hawa kutenda dhambi. 3 Hivyo iweni waangalifu!
Ikiwa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akikukosea, umwonye. Akitubu, msamehe. 4 Hata kama akikukosea mara saba katika siku moja, lakini akakuomba msamaha kila anapokukosea, msamehe.”
Imani Yako Ni Kubwa Kiasi Gani?
5 Kisha mitume wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
6 Bwana akasema, “Imani yenu ingekuwa kubwa kama mbegu ya haradali, mngeuambia mforosadi huu, ‘Ng'oka, ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.
Iweni Watumishi Wema
7 Chukulia mmoja wenu ana mtumishi ambaye amekuwa shambani akilima au akichunga kondoo shambani. Akirudi kutoka shambani au machungani, utamwambia nini? Je, utamwambia, ‘Njoo ndani, keti, ule chakula’? 8 Hapana! Utamwambia mtumishi wako, ‘Nitayarishie chakula nile. Jitayarishe na unihudumie. Nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula.’ 9 Mtumishi asipewe shukrani maalumu kwa kufanya kazi yake. Anafanya kile alichoagizwa na mkuu wake. 10 Vivyo hivyo nanyi. Mkimaliza kufanya yote mliyoamriwa kufanya, mseme, ‘Sisi ni watumwa, hatustahili shukrani yoyote maalumu. Tumefanya kazi tunayotakiwa kufanya.’”
© 2017 Bible League International