Book of Common Prayer
15 Wafanya biashara wataogopa mateso yake na watakaa mbali naye. Hawa ni wale waliotajirika kwa kumwuzia vitu hivyo. Watalia na kuhuzunika. 16 Watasema:
“Inatisha! Inatisha kwa mji mkuu!
Alivalishwa kitani safi;
alivaa zambarau na nguo nyekundu.
Alikuwa anang'aa kwa sababu ya dhahabu, vito na lulu!
17 Utajiri wote huu umeteketezwa kwa saa moja!”
Kila nahodha, wote ambao husafiri katika meli, mabaharia na wote ambao hupata pesa kutokana na bahari walisimama mbali na Babeli. 18 Waliuona moshi wa kuungua kwake. Walilia kwa sauti, “Hakukuwa na mji kama mji huu mkuu!” 19 Walirusha mavumbi juu ya vichwa vyao na kulia kwa sauti kuu kuonesha huzuni kuu waliyokuwa nayo. Walisema:
“Inatisha! Inatisha sana kwa mji mkuu!
Wote waliokuwa na meli baharini walitajirika kwa sababu ya utajiri wake!
Lakini umeteketezwa katika saa moja!
20 Ufurahi kwa sababu ya hili, Ee mbingu!
Furahini, watakatifu wa Mungu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu kwa sababu ya kile alichowatendea ninyi.”
21 Kisha malaika mwenye nguvu akainua jiwe kubwa. Jiwe hili lilikuwa kubwa kama jiwe kubwa la kusagia. Malaika akalitupia jiwe baharini na kusema:
“Hivyo ndivyo mji mkuu Babeli utakavyotupwa chini.
Hautaonekana tena.
22 Ee Babeli, muziki wa wapigao vinanda na ala zingine waimbaji na tarumbeta,
hautasikika tena ndani yako.
Hakuna mfanyakazi afanyaye kazi atakayeonekana ndani yako tena.
Sauti ya jiwe la kusagia haitasikika ndani yako tena.
23 Mwanga wa taa hautang'aa ndani yako tena.
Sauti za maarusi hazitasikika ndani yako tena.
Wafanyabiashara wako walikuwa watu wakuu wa ulimwengu.
Mataifa yote yalidanganyika kwa uchawi wako.
24 Una hatia ya vifo vya manabii, na watakatifu wa Mungu,
na vya wote waliouawa duniani.”
Utazawadiwa
12 Kisha Yesu akamwambia Farisayo aliyemwalika, “Unapoandaa chakula, usiwaalike rafiki zako tu, au ndugu zako, au jamaa zako, wala jirani zako matajiri. Kwa sababu wao pia watakualika, na kwa kufanya hivyo watakuwa wanakulipa. 13 Lakini ufanyapo sherehe waalike maskini, waliolemaa, walemavu wa miguu, na wasiyeona. 14 Utabarikiwa, kwa sababu watu hawa hawana kitu cha kukulipa. Lakini Mungu atakupa thawabu wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
Mfano Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Chakula
(Mt 22:1-10)
15 Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.”
16 Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. 17 Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ 18 Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ 19 Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ 20 Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’
21 Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’
22 Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ 23 Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! 24 Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’”
© 2017 Bible League International