Book of Common Prayer
Bakuli Zilizojazwa Ghadhabu ya Mungu
16 Kisha nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni. Ikiwaambia malaika saba, “Nendeni mkazimimine bakuli saba zenye ghadhabu ya Mungu juu ya dunia.”
2 Malaika wa kwanza akaondoka. Akaimimina bakuli yake duniani. Ndipo wale wote waliokuwa na alama ya mnyama na walioiabudu sanamu yake wakapata majipu mabaya yenye maumivu makali.
3 Malaika wa pili akaimimina bakuli yake baharini. Bahari ikawa kama damu ya mtu aliyekufa. Kila kitu kinachoishi baharini kikafa.
4 Malaika wa tatu akaimimina bakuli yake juu ya mito na chemichemi za maji. Mito na chemichemi za maji zikawa damu. 5 Ndipo nikasikia malaika wa maji akimwambia Mungu:
“Wewe ni yule uliyepo na uliyekuwepo daima.
Wewe ni Mtakatifu.
Uko sahihi kwa hukumu hizi ulizofanya.
6 Watu walimwaga damu za
watakatifu na manabii wako.
Sasa umewapa watu hao damu ili wanywe.
Hiki ndicho wanachostahili.”
7 Pia nikasikia madhabahu ikisema:
“Ndiyo, Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
hukumu zako ni za kweli na za haki.”
8 Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto. 9 Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.
10 Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu. 11 Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda.
Yesu Amponya Mwanamke Siku ya Sabato
10 Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi moja siku ya Sabato. 11 Alikuwepo mwanamke mmoja ndani ya sinagogi aliyekuwa na pepo mchafu aliyemlemaza kwa muda wa miaka kumi na nane. Mgongo wake ulikuwa umepinda na hakuweza kusimama akiwa amenyooka. 12 Yesu alipomwona alimwita na kumwambia, “Mama, umefunguliwa kutoka katika ugonjwa wako!” 13 Akaweka mikono yake juu yake na saa hiyo hiyo akaweza kusimama akiwa amenyooka. Akaanza kumsifu Mungu.
14 Kiongozi wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu aliponya siku ya Sabato. Akawaambia watu, “Kuna siku sita za kufanya kazi. Hivyo njooni ili mponywe katika moja ya siku hizo, msije siku ya Sabato kutafuta uponyaji.”
15 Yesu akamjibu kwa kusema, “Ninyi watu ni wanafiki! Ninyi nyote huwafungulia punda au ng'ombe wenu wa kulimia kutoka zizini na kuwapeleka kunywa maji kila siku, hata siku ya Sabato. 16 Mwanamke huyu niliyemponya ni mzaliwa halisi wa Ibrahimu.[a] Lakini Shetani alikuwa amemfunga kwa miaka kumi na nane. Hakika si kosa yeye kuponywa ugonjwa wake siku ya Sabato!” 17 Yesu aliposema haya, watu wote waliokuwa wanampinga walidhalilika. Kundi lote likafurahi kwa sababu ya mambo makuu aliyatenda.
© 2017 Bible League International