Book of Common Prayer
1 Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo.
Kwa makabila Kumi na Mawili[a] ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu!
Imani na Hekima
2 Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi. 3 Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu. 4 Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote.
5 Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima. 6 Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yo yote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa. 7 Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana; 8 yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja.
Utajiri wa Kweli
9 Ndugu aliye maskini na awe na furaha sana kwamba Mungu amemchukulia kuwa mtu wa maana sana. 10 Na waaminio walio matajiri wawe na furaha sana tu pale Mungu anapowashusha chini. Kwani utajiri wao hautawazuia kufa kama maua ya porini. 11 Jua linapochomoza na kuwa kali zaidi, joto lake hukausha mimea na maua huanguka chini na kupukutika na kupoteza urembo wake. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtu tajiri atafifia katika shughuli zake.
Majaribu Hayatoki kwa Mungu
12 Amebarikiwa mtu yule anayestahimili majaribu, maana anapofaulu mitihani atapokea taji yenye uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wanaompenda. 13 Yeyote anayejaribiwa hapaswi kusema, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu maovu hayamjaribu Mungu na hamjaribu mtu yeyote. 14 Bali kila mmoja anajaribiwa na tamaa zake mwenyewe, anapovutwa na kunaswa. 15 Kisha tamaa inapotunga mimba inazaa dhambi, na dhambi ikikomaa kabisa inazaa kifo.
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mt 16:13-19; Mk 8:27-29)
18 Wakati mmoja Yesu alikuwa anaomba akiwa peke yake. Wafuasi wake walimwendea na aliwauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?”
19 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, lakini wengine wanasema wewe ni mmoja wa manabii wa zamani aliyefufuka.”
20 Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ni Masihi kutoka kwa Mungu.”
21 Yesu akawatahadharisha wasimwambie mtu yeyote.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mt 16:21-28; Mk 8:31-9:1)
22 Yesu akasema, “Ni lazima Mwana wa Adamu apate mateso mengi. Nitakataliwa na viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Na nitauawa. Lakini siku ya tatu nitafufuliwa kutoka kwa wafu.”
23 Kisha Yesu akamwambia kila mmoja aliyekuwa pale, “Mtu yeyote miongoni mwenu akitaka kuwa mfuasi wangu ni lazima ajikane yeye mwenyewe na mambo anayopenda. Ni lazima uubebe msalaba unaotolewa kwako kila siku kwa sababu ya kunifuata mimi. 24 Yeyote miongoni mwenu anayetaka kuyaponya maisha yake atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25 Haina thamani kwenu kuupata ulimwengu wote ikiwa ninyi wenyewe mtateketezwa au kupoteza kila kitu. 26 Msione aibu kwa sababu ya kunifuata na kusikiliza mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, Mimi, Mwana wa Adamu, nitawaonea aibu nitakapokuja nikiwa na utukufu wangu, utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu. 27 Niaminini ninaposema kwamba baadhi yenu ninyi mliosimama hapa mtauona Ufalme wa Mungu kabla hamjafa.”
© 2017 Bible League International