Book of Common Prayer
18 Hivyo mfumo wa sheria za zamani zilizowekwa sasa zinaisha kwa sababu zilikuwa dhaifu na hazikuweza kutusaidia. 19 Sheria ya Musa haikuweza kukamilisha kitu chochote. Lakini sasa tumaini bora zaidi limeletwa kwetu. Na kwa tumaini hilo tunaweza kumkaribia Mungu.
20 Vile vile, ni muhimu kwamba Mungu aliweka ahadi kwa kiapo alipomfanya Yesu kuwa kuhani mkuu. Watu hawa wengine walipofanyika makuhani, hapakuwepo kiapo. 21 Lakini Yesu akafanyika kuhani kwa kiapo cha Mungu. Mungu alimwambia:
“Bwana anaweka ahadi kwa kiapo
naye hatabadili mawazo yake:
‘Wewe ni kuhani milele.’”(A)
22 Hivyo hii inamaanisha kwamba Yesu ni uhakika wa agano zuri zaidi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake.
23 Pia, mmoja wa hawa makuhani wengine alipofariki, asingeendelea kuwa kuhani. Hivyo walikuwepo makuhani wengi wa jinsi hii. 24 Lakini Yesu anaishi milele. Hatakoma kufanya kazi kama kuhani. 25 Hivyo anaweza kuwaokoa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake. Yesu anaweza kufanya hivi milele, kwa sababu anaishi siku zote na yuko tayari kuwasaidia watu wanapomjia Mungu.
26 Hivyo Yesu ni aina ya kuhani mkuu tunayemhitaji. Yeye ni mkamilifu. Hana dhambi ndani yake. Hana kasoro na havutwi na watenda dhambi. Naye amepandishwa juu ya mbingu. 27 Hayuko sawa na hawa makuhani wengine. Walitakiwa kutoa sadaka kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Lakini Yesu hahitaji kufanya hivyo. Alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya nyakati zote. Alijitoa mwenyewe. 28 Sheria huchagua makuhani wakuu ambao ni watu na wanao udhaifu ule ule ambao watu wote wanao. Lakini baada ya sheria, Mungu alisema kiapo ambacho kilimfanya Mwana awe kuhani mkuu. Na Mwana huyo, aliyekamilishwa kwa njia ya mateso, atatumika kama kuhani mkuu milele yote.
Simulizi Kuhusu Msamaria Mwema
25 Kisha mwanasheria mmoja alisimama ili amjaribu Yesu. Akasema, “Mwalimu, ninatakiwa nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26 Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Unaielewaje?”
27 Yule mwana sheria akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.’(A) Pia ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(B)
28 Yesu akasema, “Jibu lako ni sahihi. Fanya hivi nawe utaupata uzima wa milele.”
29 Lakini mwanasheria alitaka kuonesha kuwa alikuwa mwenye haki na aliishi kwa usahihi. Hivyo akamwuliza Yesu, “Lakini si kila mtu aliye jirani yangu, au unasemaje?”
30 Katika kujibu swali hili, Yesu akasema, “Mtu mmoja alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani alivamiwa na majambazi, wakamchania nguo na kumpiga. Kisha wakamwacha amelala chini akiwa katika hali ya kufa.
31 Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa anasafiri kupitia njia hiyo hiyo. Alipomwona, hakusimama ili amsaidie, alikwenda zake. 32 Kisha Mlawi[a] alipokaribia na kumwona yule mtu, alipita upande mwingine. Hakusimama ili amsaidie, Alikwenda zake.
33 Ndipo Msamaria[b] mmoja aliyekuwa anasafiri kupitia njia ile ile, alipofika mahali ambapo mtu aliyejeruhiwa alikuwa amelala, alipomwona alimhurumia. 34 Alimkaribia ili amsaidie, akamsafisha majeraha kwa mafuta ya zeituni na divai,[c] kisha akayafunga majeraha yake. Msamaria alikuwa na punda. Akampandisha juu ya punda wake na kumpeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni. Akamhudumia huko. 35 Siku iliyofuata, Msamaria alitoa sarafu mbili za fedha na kumpa mtunza nyumba ya wageni, akamwambia, ‘Mtunze mtu huyu aliyejeruhiwa. Ukitumia pesa nyingi zaidi kwa kumhudumia, nitakulipa nitakapokuja tena.’”
36 Kisha Yesu akasema, “Ni yupi kati ya hawa watu watatu unadhani hakika alikuwa jirani wa yule mtu aliyepigwa na majambazi?”
37 Mwanasheria akajibu, “Ni yule aliyemsaidia.”
Yesu akasema, “Basi nenda ukafanye kama alivyofanya.”
© 2017 Bible League International