Book of Common Prayer
7 Yesu alipoishi duniani alimwomba Mungu, akiusihi msaada kutoka kwa yule anayeweza kumwokoa kutoka mauti. Alimwomba Mungu kwa sauti kuu na kwa machozi. Na Mungu alizisikia sala zake kwa sababu ya heshima yake kuu kwa Mungu. 8 Yesu alikuwa mwana wa Mungu, lakini aliteseka, na kwa njia ya mateso yake alijifunza kutii chochote alichosema Mungu. 9 Hili lilimfanya yeye awe kuhani mkuu mkamilifu, anayetoa njia kwa ajili ya kila mmoja anayemtii ili kuokolewa milele. 10 Mungu alimfanya yeye kuhani mkuu, kama alivyokuwa Melkizedeki.
Tahadhari Kuhusu Kuanguka
11 Tunayo mambo mengi ya kuwaeleza kuhusu hili. Lakini ni vigumu kufafanua kwa sababu mmeoteza shauku ya kusikiliza. 12 Mmekuwa na muda wa kutosha ambapo sasa mngepaswa kuwa walimu. Lakini mnahitaji mtu awafundishe tena mafundisho ya Mungu ya mwanzo. Bado mnahitaji mafundisho ambayo yako kama maziwa. Hamjafikia kiwango cha chakula kigumu. 13 Yeyote anayeishi kwa kutegemea maziwa tu bado ni mtoto mchanga, hayupo tayari kuelewa zaidi kuhusu kuishi kwa haki. 14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu ambao wamekua. Kutokana na uzoefu wao wamejifunza kuona tofauti baina ya jema na ovu.
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-18; Mk 9:14-27)
37 Siku iliyofuata, Yesu, Petro, Yohana na Yakobo walitelemka kutoka mlimani. Kundi kubwa la watu likaenda kukutana naye. 38 Mtu mmoja katika umati huo alimwita Yesu akisema, “Mwalimu, tafadhali njoo umwonee mwanangu. Ni mtoto pekee niliye naye. 39 Pepo mchafu humvaa na hupiga kelele, humtia kifafa na kumtoa povu mdomoni. Huendelea kumwumiza na hamwachi kirahisi. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyu mchafu lakini wameshindwa.”
41 Yesu akajibu, “Enyi watu msio na imani. Maisha yenu ni mabaya. Nitakaa na kuchukuliana nanyi mpaka lini?” Ndipo Yesu akamwambia yule mtu, “Mlete kijana wako hapa.”
42 Kijana alipokuwa anakwenda kwa Yesu, pepo mchafu akamwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamwamuru atoke. Kijana akaponywa, na Yesu akampeleka kwa baba yake. 43 Watu wote wakaushangaa ukuu wa nguvu ya Mungu.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Mk 9:30-32)
Watu walipokuwa bado wanayashangaa mambo yote aliyofanya Yesu. Akawaambia wanafunzi wake, 44 “Msiyasahau nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu yu karibu kukamatwa na kuwekwa katika mikono ya watu wengine.” 45 Lakini wanafunzi hawakuelewa alichomaanisha. Maana ilifichwa kwao ili wasitambue. Lakini waliogopa kumwuliza Yesu kuhusiana na alilosema.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Mk 9:33-37)
46 Wafuasi wa Yesu walianza kubishana wakiulizana nani ni mkuu kuliko wote miongoni mwao. 47 Yesu alijua walichokuwa wanafikiri, hivyo akamchukua mtoto mdogo na kumsimamisha karibu yake. 48 Kisha akawaambia, “Yeyote anayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu kwa jina langu ananikaribisha mimi. Na yeyote anayenikaribisha mimi anamkaribisha yule aliyenituma. Aliye mnyenyekevu zaidi miongoni mwenu, ndiye mkuu.”
Asiye Kinyume Nanyi ni Mmoja Wenu
(Mk 9:38-40)
49 Yohana akajibu; “Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kutoka kwa watu akitumia jina lako. Tulimwambia aache kwa sababu hayuko katika kundi letu.”
50 Yesu akamwambia, “Msimkataze. Asiye kinyume nanyi yu pamoja nanyi.”
© 2017 Bible League International