Book of Common Prayer
Msiwakosoe Wengine
14 Iweni tayari kuwakubali wenye mashaka kuhusu yale ambayo waamini wanaweza kufanya. Tena msibishane nao kuhusu mawazo yao tofauti. 2 Baadhi ya watu wanaamini kuwa wanaweza kula aina yoyote ya chakula,[a] lakini wale walio na mashaka wanakula mboga za majani tu. 3 Wale wanaojua kuwa wanaweza kula chakula cha aina yoyote hawapaswi kujisikia kuwa ni bora kuliko wale wanaokula mboga za majani tu. Na wale wanaokula mboga za majani tu hawapaswi kuamua kuwa wale wanaokula vyakula vyote wanakosea. Mungu amewakubali. 4 Huwezi kuwahukumu watumishi wa mtu mwingine. Hilo linamhusu bwana wao mwenyewe ikiwa watafaulu au watashindwa. Na watakubaliwa, kwa sababu Bwana yuko tayari kuwafanya wafaulu.
5 Watu wengine wanaweza kuamini kuwa siku moja ni ya muhimu zaidi kuliko nyingine. Na wengine wanaweza kuwa na uhakika kuwa siku zote ziko sawa. Kila mtu anapaswa kujihakikisha juu ya imani yake katika akili zake wenyewe. 6 Wale wanaofikiri kuwa siku moja ni ya muhimu kuliko siku zingine wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Na wale wanaokula vyakula vya aina zote wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Ndiyo, wanamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Na wale wanaokataa kula vyakula fulani wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Nao pia wanamshukuru Mungu.
7 Hatuishi au kufa kwa ajili yetu sisi wenyewe tu. 8 Kama tukiishi, tunaishi kwa ajili ya Bwana. Na kama tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Hivyo kuishi au kufa, sisi ni mali ya Bwana. 9 Ndiyo sababu Kristo alikufa na kuishi tena ili awe Bwana juu ya wote waliokufa na wanaoishi.
10 Hivyo kwa nini unamhukumu kaka au dada yako katika familia ya Mungu? Au kwa nini unafikiri kuwa wewe ni bora kuliko wao? Sote tutasimama mbele za Mungu, naye atatuhukumu sisi sote. 11 Ndiyo, Maandiko yanasema,
“‘Hakika kama niishivyo’, asema Bwana,
‘kila mtu atapiga magoti mbele zangu,
na kila mtu atasema kuwa mimi ni Mungu.’”(A)
12 Hivyo kila mmoja wetu ataeleza kuhusu matendo yake mbele za Mungu.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Mk 5:1-20)
26 Yesu na wafuasi wake wakasafiri mpaka katika nchi walimoishi Wagerasi[a] iliyokuwa ng'ambo ya ziwa Galilaya. 27 Yesu alipotoka katika mashua, mwanaume mmoja kutoka katika mji ule alimwendea. Mtu huyu alikuwa na mapepo ndani yake. Kwa muda mrefu hakuwahi kuvaa nguo na aliishi makaburini.
28-29 Pepo aliyekuwa ndani yake alikuwa akimpagaa mara nyingi na alikuwa akifungwa gerezani, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo. Lakini kila mara aliivunja. Pepo ndani yake alikuwa anamlazimisha kwenda nje ya mji mahali pasipoishi watu. Yesu alimwamuru kumtoka mtu yule. Alipomwona Yesu, alianguka mbele yake huku akipiga kelele kwa sauti, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu Aliye Juu? Tafadhali usiniadhibu!”
30 Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?”
Mtu yule akajibu, “Jeshi.”[b] (Alisema jina lake ni “Jeshi” kwa sababu pepo wengi walikuwa wamemwingia.) 31 Pepo wale wakamsihi Yesu asiwaamuru kwenda shimoni.[c] 32 Katika kilima kile, kulikuwa kundi kubwa la nguruwe wakichungwa. Pepo wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie wale nguruwe. Hivyo Yesu akawaruhusu. 33 Pepo wakamtoka yule mtu, na kuwaingia nguruwe. Kundi lote la wale nguruwe likakimbia kutelemkia ziwani kwa kasi, nguruwe wakazama na kufia humo.
34 Wachungaji wa nguruwe walipoona lililotokea, walikimbia, wakaenda kutoa taarifa mjini na mashambani. 35 Watu wakaenda kuona lililotokea. Walipofika alipokuwa Yesu wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, akiwa na akili zake timamu; pepo walikuwa wamemtoka. Jambo hili likawaogopesha watu. 36 Wale walioona mambo haya yalivyotokea waliwaambia wengine namna Yesu alivyomponya yule mtu. 37 Watu wote waliokuwa wakiishi eneo lote la Gerasi wakamtaka Yesu aondoke kwa sababu waliogopa.
Hivyo Yesu akapanda mashua na kurudi Galilaya. 38 Mtu aliyeponywa alimsihi amfuate Yesu. Lakini Yesu akamtuma, akamwambia, 39 “Rudi nyumbani, ukawaeleze watu mambo ambayo Mungu amekutendea.”
Hivyo mtu yule alikwenda sehemu zote za mji akieleza mambo ambayo Yesu amemtendea.
© 2017 Bible League International