Book of Common Prayer
Mungu na Wayahudi
9 Nazungumza nayi sasa kama mmojawapo niliye wa Kristo. Hivyo mnaweza kuwa na uhakika kuwa sisemi uongo. Dhamiri yangu, inayotawaliwa na Roho Mtakatifu, inakubali kwamba ninayowaambia sasa ni kweli. 2 Nimejawa na huzuni na maumivu ya moyoni yasiyokwisha 3 kwa ajili ya watu wangu. Wao ni kaka na dada zangu katika mwili. Natamani ningeweza kuwasaidia. Ningekuwa tayari pia kuomba kupokea laana ya kutengwa na Kristo kama hiyo itaweza kuwasaidia. 4 Ni Waisraeli, watoto waliochaguliwa na Mungu. Wameushuhudia utukufu wa Mungu na wanashiriki maagano aliyofanya Mungu na watu wake. Mungu aliwapa Sheria ya Musa, ibada ya Hekalu, na ahadi zake. 5 Ni wazaliwa wa mababa zetu wakuu, na ni familia ya kidunia ya Masihi,[a] ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote. Yeye asifiwe milele![b] Amina.
6 Sina maana kuwa Mungu alishindwa kutimiza ahadi yake kwa Wayahudi. Lakini kwa hakika ni baadhi tu ya Waisraeli ndiyo watu wa Mungu[c]. 7 Na hivyo ni baadhi tu ya watoto wa Ibrahimu ndiyo wazaliwa wake halisi. Hivi ndivyo Mungu alimwambia Ibrahimu: “Wazaliwa wako halisi watakuwa wale waliotoka kwa Isaka.”(A) 8 Hii ina maana kuwa si watoto wote wa Ibrahimu walio watoto halisi wa Mungu. Wazaliwa halisi wa Ibrahamu ni wale wanaofanyika watoto wa Mungu kwa sababu ya agano ambalo Mungu alililiweka na Ibrahamu. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyosema katika agano hilo: “Wakati kama huu mwaka ujao nitakujia tena, na Sara mke wako atazaa mwana.”(B)
10 Na si hivyo tu. Kitu kama hicho kilimtokea Rebeka ambaye baada ya kupata mimba ya wana wawili mapacha waliotokana na baba mmoja, baba yetu Isaka. 11-12 Ndiyo, kabla ya kuzaliwa wana hao mapacha, Mungu alimwambia Rebeka, “Mwana mkubwa atamtumikia mdogo.”(C) Hii ilikuwa kabla wavulana hawa hawajatenda jambo lolote jema au baya. Mungu alisema hivi kabla hawajazaliwa ili kwamba mvulana ambaye Mungu alimtaka atachaguliwa kutokana na mpango wa Mungu mwenyewe. Mvulana huyu alichaguliwa kwa sababu ndiye ambaye Mungu alitaka kumwita, si kwa sababu ya jambo lolote walilofanya wavulana hao. 13 Kama Maandiko yanavyosema, “Nilimpenda Yakobo lakini nilimchukia Esau.”(D)
14 Namsikia mtu akiuliza, “Hivyo hii ina maana gani? Je, Mungu si mwenye haki?” Hapana! 15 Mungu alimwambia Musa, “Nitampa rehema yeyote ninayetaka kumpa rehema. Nitamhurumia yeyote ninayemchagua.”(E) 16 Hivyo Mungu atamchagua yeyote anayeamua kumpa rehema pasipo kujali watu wanataka nini ama kwa jinsi gani wanapiga mbio. 17 Katika Maandiko Mungu anamwambia Farao: “Nilikuweka uwe mfalme kwa kusudi hili hasa: kuonesha nguvu zangu kupitia kwako. Nilitaka jina langu litangazwe ulimwenguni kote”(F) 18 Hivyo Mungu huwarehemu wale anaotaka kuwarehemu na huwafanya jeuri wale anaotaka wawe jeuri.
Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu
60 Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?”
61 Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je, fundisho hili ni tatizo kwenu? 62 Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? 63 Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” 64 Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) 65 Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’”
66 Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata.
67 Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. 69 Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.”
70 Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” 71 Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake.
© 2017 Bible League International