Book of Common Prayer
Kuzaliwa kwa Yesu, Masihi
(Lk 2:1-7)
18 Kuzaliwa kwa Yesu Masihi, kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alikuwa amechumbiwa na Yusufu. Kabla hawajaoana, Yusufu aligundua kuwa Mariamu alikuwa mja mzito. (Yeye alipata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.) 19 Kwa kuwa Yusufu alitaka kufanya kile kilichokuwa, alikusudia kumwacha Mariamu kwa siri bila ya kumvunjia heshima.
20 Lakini baada ya Yusufu kuliwazia jambo hili, Malaika wa Bwana alimjia katika ndoto na akamwambia, “Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu awe mke wako. Mimba aliyonayo ameipata kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Atamzaa mwana, nawe utamwita Yesu.[a] Utampa jina hilo Yesu kwa sababu yeye atawaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
22 Haya yote yalitokea ili kutimiza maneno ambayo Bwana aliyasema kupitia kwa nabii aliposema:
23 “Sikiliza! Msichana bikira atapata mimba
na atazaa mtoto wa kiume.
Mtoto huyo ataitwa Emanueli.”(A)
(Yaani “Mungu yu pamoja nasi”.)
24 Yusufu alipoamka alifanya kama alivyoelekezwa na Malaika wa Bwana. Alimuoa Mariamu. 25 Lakini hakukutana naye kimwili mpaka Mariamu alipomzaa mwana. Na Yusufu akamwita Yesu.
Upendo wa Kristo
14 Hivyo ninapiga magoti nikimwomba Baba. 15 Ambaye katika yeye kila familia iliyoko mbinguni na duniani inapewa jina. 16 Ninamwomba Baba kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake awajaze nguvu za ndani kwa nguvu za Roho wake. 17 Ninaomba kwamba Kristo aishi katika mioyo yenu kwa sababu ya imani yenu. Ninaomba maisha yenu yawe na mizizi mirefu na misingi imara katika upendo. 18 Na ninaomba ili ninyi na watakatifu wote wa Mungu muwe na uwezo wa kuuelewa upana, urefu, kimo na kina cha ukuu wa upendo wa Kristo. 19 Upendo wa Kristo ni mkuu kuliko namna ambavyo mtu yeyote anaweza kujua, lakini ninawaombea ili mweze kuujua. Ndipo mtajazwa kwa kila kitu alichonacho Mungu kwa ajili yenu.
20 Tukiwa na nguvu za Mungu zinazotenda kazi ndani yetu, anaweza kufanya zaidi, zaidi ya kila kitu tunachoweza kuomba au kufikiri. 21 Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kila wakati, milele na milele. Amina.
© 2017 Bible League International