Book of Common Prayer
Ahadi ya Mungu Hupokelewa kwa Imani
13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu na wazaliwa wake ya kuwapa ulimwengu wote. Lakini kwa nini Mungu aliweka ahadi hii? Haikuwa kwa sababu Ibrahimu aliifuata sheria. Ni kwa sababu aliiweka imani yake katika Mungu na akakubaliwa kuwa mwenye haki. 14 Watu wa Mungu watarithi yote ambayo Mungu alimwahidi Ibrahimu, lakini si kwa sababu wanaifuata sheria. Ikiwa ni lazima tuitii sheria ili tupate kile alichoahidi Mungu, badi imani ya Ibrahimu haina maana yoyote na ahadi ya Mungu haina manufaa. 15 Ninasema hivi kwa sababu sheria ndiyo huleta hasira ya Mungu kwa wale wasioitii. Lakini ikiwa sheria haipo, basi hakuna hatia ya kutoitii.
16 Hivyo watu hupokea ahadi ya Mungu kwa imani. Hili hutokea ili ahadi hiyo iwe kipawa cha bure. Na ikiwa ahadi ni kipawa cha bure, basi watu wote wa Ibrahimu watapata ahadi hiyo. Ahadi hii si tu kwa ajili ya wale wanaoishi chini ya Sheria ya Musa. Bali ni kwa ajili ya wote wanaoishi kwa kuweka imani yao kwa Mungu kama Ibrahimu alivyofanya. Ni baba yetu sote. 17 Kama Maandiko yanavyosema, “Nimekufanya uwe baba wa mataifa mengi.”(A) Ibrahimu aliposikia ahadi hii, aliiweka imani yake kwa Mungu. Mungu ndiye awapaye uhai waliokufa na kwa amri yake huumba kisichokuwepo.
18 Halikuwepo tumaini kwamba Ibrahimu angepata watoto, lakini alimwamini Mungu na akaendelea kutumaini. Na ndiyo sababu akafanyika kuwa baba wa mataifa mengi. Kama Mungu alivyomwambia kuwa, “Utakuwa na wazaliwa wengi.”(B) 19 Ibrahimu alikuwa na umri uliokaribia miaka 100, hivyo alikuwa amevuka umri wa kupata watoto. Pia, Sara hakuweza kuwa na watoto. Ibrahimu alilijua hili vizuri, lakini imani yake kwa Mungu haikudhoofika. 20 Hakutilia shaka kuwa Mungu angetenda kile alichoahidi. Hakuacha kuamini. Kwa hakika, aliendelea kuimarika katika imani yake. Alitukuza Mungu 21 na alikuwa na uhakika kuwa Mungu anaweza kutenda alichoahidi. 22 Ndiyo sababu “Mungu alimkubali kuwa ni mwenye haki”. 23 Maneno haya, “alikubaliwa”, yaliandikwa siyo tu kwa ajili ya Ibrahimu. 24 Pia yaliandikwa kwa ajili yetu. Mungu atatukubali sisi pia kwa sababu tunaamini. Tunamwamini yule aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Yesu alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, na akafufuliwa kutoka kifo ili Mungu atuhesabie haki.
Yesu Azungumza Juu ya Roho Mtakatifu
37 Siku ya mwisho ya kusherehekea sikukuu ikafika. Nayo Ilikuwa siku muhimu zaidi. Katika siku hiyo Yesu alisimama na kusema kwa sauti kubwa, “Yeyote aliye na kiu aje kwangu anywe. 38 Kama mtu ataniamini, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka ndani ya moyo wake. Ndivyo Maandiko yanavyosema.” 39 Yesu alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu ambaye alikuwa hajatolewa kwa watu bado, kwa sababu Yesu naye alikuwa bado hajatukuzwa. Ingawa baadaye, wale waliomwamini Yesu wangempokea huyo Roho.
Watu Wanabishana Juu ya Yesu
40 Watu waliposikia maneno aliyosema Yesu, baadhi yao wakasema, “Hakika mtu huyu ni nabii.”[a]
41 Wengine wakasema, “Huyu ni Masihi.”
Na wengine wakasema, “Masihi hawezi kutoka Galilaya. 42 Maandiko yanasema kwamba Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi. Na wanasema kwamba atatoka Bethlehemu, mji alimoishi Daudi.” 43 Kwa jinsi hiyo watu hawakukubaliana wao kwa wao kuhusu Yesu. 44 Baadhi yao wakataka kumkamata. Lakini hakuna aliyejaribu kufanya hivyo.
Baadhi ya Viongozi wa Kiyahudi Wakataa Kuamini
45 Walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Makuhani na Mafarisayo wakawauliza, “Kwa nini hamjamleta Yesu?”
46 Walinzi wa Hekalu wakajibu, “Hatujawahi kumsikia mtu akisema mambo ya ajabu kiasi hicho!”
47 Mafarisayo wakajibu, “Kwa hiyo Yesu amewadanganya hata ninyi? 48 Hamuoni kuwa hakuna kiongozi yeyote wala sisi Mafarisayo anayemwamini? 49 Lakini watu hao walio nje wasiojua sheria wamo katika laana ya Mungu.”
50 Lakini Nikodemu alikuwa katika kundi lile. Naye ndiye yule aliyekwenda kumwona Yesu pale mwanzo.[b] Naye akasema, 51 “Sheria yetu haitaturuhusu kumhukumu mtu na kumtia hatiani kabla ya kumsikiliza kwanza na kuyaona aliyotenda?”
52 Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Wewe nawe utakuwa umetoka Galilaya. Jifunze Maandiko. Hutapata lolote kuhusu nabii[c] anayetoka Galilaya.”
© 2017 Bible League International