Book of Common Prayer
28 Tunajua kwamba katika kila kitu Mungu[a] hufanya kazi ili kuwapa mema wale wanaompenda. Hawa ni watu aliowachagua Mungu, kwa sababu huo ndiyo ulikuwa mpango wake. 29 Mungu aliwajua kabla hajauumba ulimwengu. Na aliamua hao wangekuwa kama Mwanaye. Na Yesu angekuwa mzaliwa wa kwanza wa watoto wake wengi. 30 Mungu aliwakusudia wao wawe kama Mwanaye. Aliwachagua na kuwahesabia haki pamoja na Mungu. Na alipowahesabia haki, akawapa utukufu wake.
Mungu Huonesha Pendo lake Kupitia Yesu
31 Hivyo tuseme nini juu ya hili? Ikiwa Mungu yuko kwa ajili yetu, hakuna anayeweza kuwa kinyume nasi. 32 Naye alimwacha mwanae ateswe kwa ajili yetu. Mungu alimtoa Mwanaye kwa ajili yetu sisi sote. Sasa kwa kuwa tu wa Kristo, hakika Mungu atatupa mambo mengine yote. 33 Nani atakayewashitaki watu waliochaguliwa na Mungu? Hayupo! Mungu ndiye hutuhesabia haki. 34 Ni nani anaweza kuwahukumu watu wa Mungu kuwa wana hatia? Hayupo! Kristo Yesu alikufa kwa ajili yetu na alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu na anazungumza na Mungu kwa ajili yetu. 35 Je, kuna kitu chochote kinachoweza kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni matatizo au shida au mateso? Ikiwa hatuna chakula au mavazi au tunakabiliwa na hatari au kifo, je mambo hayo yatatutenga sisi kutoka katika upendo wake? 36 Kama Maandiko yanavyosema,
“Kwa ajili yako, tunakabiliana na kifo wakati wote.
Watu wanadhani hatuna thamani kama kondoo wanaowachinja.”(A)
37 Lakini katika shida zote hizo tuna ushindi kamili kupitia Mungu, aliyetuonyesha upendo wake. 38-39 Ndiyo, nina uhakika kuwa hakuna kitu kinachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu, si kifo, maisha, malaika, wala roho zinazotawala. Nina uhakika kuwa hakuna wakati huu, hakuna wakati ujao; hakuna mamlaka, hakuna kilicho juu yetu au chini yetu, hakuna katika ulimwengu wote ulioumbwa, kitakachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu ulioonyeshwa kwetu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
52 Kisha Wayahudi hawa wakaanza kubishana wao kwa wao. Wakasema, “Yawezekanaje mtu huyu akatupa mwili wake tuule?”
53 Yesu akasema, “Mniamini ninaposema kwamba mnapaswa kuula mwili wa Mwana wa Adamu, na mnapaswa kuinywa damu yake. Msipofanya hivyo, hamtakuwa na uzima wa kweli. 54 Wale wanaoula mwili wangu na kuinywa damu yangu wanao uzima wa milele. Nitawafufua siku ya mwisho. 55 Mwili wangu ni chakula halisi, na damu yangu ni kinywaji halisi. 56 Wale waulao[a] mwili wangu na kuinywa damu yangu wanaishi ndani yangu, nami naishi ndani yao.
57 Baba alinituma. Yeye anaishi, nami naishi kwa sababu yake. Hivyo kila anayenila mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Mimi siyo kama ule mkate walioula baba zenu. Wao waliula mkate huo, lakini bado walikufa baadaye. Mimi ni mkate uliotoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele.”
59 Yesu aliyasema haya yote alipokuwa akifundisha kwenye Sinagogi katika mji wa Kapernaumu.
© 2017 Bible League International