Book of Common Prayer
12 Watu walio na sheria na wote ambao hawajawahi kuisikia sheria, wote wako sawa wanapotenda dhambi. Watu wasio na sheria na ni watenda dhambi wataangamizwa. Vivyo hivyo, wale walio na sheria na ni watenda dhambi watahukumiwa kuwa na hatia kwa kutumia sheria. 13 Kuisikia sheria hakuwafanyi watu wawe wenye haki kwa Mungu. Wanakuwa wenye haki mbele zake, pale wanapotekeleza kile kinachoagizwa na sheria.
14 Fikirini kuhusu wasio Wahayudi ambao hawakukua wakiwa na sheria. Wanapotenda kama sheria inavyoamuru,[a] wanakuwa kielelezo cha sheria, ijapokuwa hawana sheria iliyoandikwa. 15 Wanaonesha kuwa wanafahamu kilicho sahihi na kibaya, kama sheria inavyoamuru na dhamiri zao zinakubali. Lakini wakati mwingine mawazo yao huwaambia kuwa wamekosea au wamefanya sahihi. 16 Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu kupitia Yesu Kristo, sawasawa na Habari Njema ninayoihubiri.
Wayahudi na Sheria
17 Wewe unajiita Myahudi, na unajiona upo salama kwa kuwa tu una sheria. Kwa majivuno unadai kuwa wewe ni mmoja wa wateule wa Mungu. 18 Unajua yale ambayo Mungu anataka ufanye. Na unajua yaliyo muhimu, kwa sababu umejifunza sheria. 19 Unadhani kuwa wewe ni kiongozi wa watu wasioweza kuiona njia sahihi, na nuru kwa wale walio gizani. 20 Unafikiri unaweza kuwaonesha wajinga kilicho sahihi. Na unadhani kuwa wewe ni mwalimu wa wanaoanza kujifunza. Unayo sheria, na hivyo unadhani unajua kila kitu na una kweli yote. 21 Unawafundisha wengine, sasa kwa nini usijifundishe wewe wenyewe? Unawaambia usiibe, lakini wewe mwenyewe unaiba. 22 Unasema wasizini, lakini wewe mwenyewe una hatia ya dhambi hiyo. Unachukia sanamu, lakini unaziiba sanamu katika mahekalu yao. 23 Unajivuna sana kwamba una sheria ya Mungu, lakini unamletea Mungu aibu kwa kuivunja sheria yake. 24 Kama Maandiko yanavyosema, “Watu wa mataifa mengine wanamtukana Mungu kwa sababu yako.”[b]
Yesu Anayo Mamlaka ya Mungu
19 Lakini Yesu akajibu, “Hakika nawaambieni kuwa Mwana hawezi kufanya chochote peke yake. Bali hufanya tu yale anayoona Baba yake anayafanya. Kwa maana Mwana hufanya mambo ambayo Baba huyafanya. 20 Baba anampenda Mwana na humwonesha kila kitu anachofanya. Pia Baba atamwonesha Mwana mambo makuu ya kufanya kuliko hili. Kisha nyote mtashangazwa. 21 Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima. Kwa njia hiyo hiyo, Mwana pia huwapa uzima wale anaowataka.”
22 “Vile vile, Baba hamhukumu mtu. Bali amempa Mwana nguvu ya kufanya hukumu zote. 23 Mungu alifanya hivi ili watu wote waweze kumheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Mtu yeyote asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba. Kwani Baba ndiye aliyemtuma Mwana.
24 Kwa hakika nawaambia, yeyote anayesikia ninayosema na kumwamini yule aliyenituma anao uzima wa milele. Hawa hawatahukumiwa kuwa na hatia. Kwani tayari wameshaivuka mauti na kuingia ndani ya uzima. 25 Mniamini, wakati muhimu sana unakuja. Wakati huo tayari upo ambapo watu waliokufa wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu. Na hao watakaoisikia watafufuka na kuwa hai. 26 Uzima huja kutoka kwa Baba mwenyewe. Na pia Baba amemruhusu Mwana kutoa uzima. 27 Na Baba amempa Mwana mamlaka ya kuwahukumu watu wote kwa sababu yeye ndiye Mwana wa Adamu.
28 Ninyi msishangazwe na hili. Wakati unakuja ambapo watu wote waliokufa na kuwamo makaburini mwao wataisikia sauti yake. 29 Kisha watatoka nje ya makaburi yao. Wale waliotenda mema watafufuka na kupata uzima wa milele. Lakini wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa kwa kuwa na hatia.
© 2017 Bible League International