Add parallel Print Page Options

Ukoo wa Yesu

(Lk 3:23-38)

Hii ni historia ya ukoo wa Yesu, Masihi.[a] Alitoka katika ukoo wa Daudi, aliyetoka katika ukoo wa Ibrahimu.

Ibrahimu alikuwa baba yake Isaka.

Isaka alikuwa baba yake Yakobo.

Yakobo alikuwa baba wa Yuda na ndugu zake.

Yuda alikuwa baba wa Peresi na Zera. (Mama yao alikuwa Tamari.)

Peresi alikuwa baba yake Hezroni.

Hezroni alikuwa baba yake Ramu.

Ramu alikuwa baba yake Aminadabu.

Aminadabu alikuwa baba yake Nashoni.

Nashoni alikuwa baba yake Salmoni.

Salmoni alikuwa baba yake Boazi. (Mama yake Boazi alikuwa Rahabu.)

Boazi alikuwa baba yake Obedi. (Mama yake Obedi alikuwa Ruthu.)

Obedi alikuwa baba yake Yese.

Yese alikuwa baba yake Mfalme Daudi.

Daudi alikuwa baba yake Sulemani. (Mama yake Sulemani alikuwa mke wa Uria.)

Sulemani alikuwa baba yake Rehoboamu.

Rehoboamu alikuwa baba yake Abiya.

Abiya alikuwa baba yake Asa.

Asa alikuwa baba yake Yehoshafati.

Yehoshafati alikuwa baba yake Yoramu.

Yoramu alikuwa baba yake Uzia.

Uzia alikuwa baba yake Yothamu.

Yothamu alikuwa baba yake Ahazi.

Ahazi alikuwa baba yake Hezekia.

10 Hezekia alikuwa baba yake Manase.

Manase alikuwa baba yake Amoni.

Amoni alikuwa baba yake Yosia.

11 Yosia alikuwa baba wa Yekonia[b] na ndugu zake.

Walioishi wakati ambao watu walipelekwa utumwani Babeli.

12 Baada ya uhamisho wa Babeli,

Yekonia akawa baba yake Shealtieli.

Shealtieli alikuwa babu wa Zerubabeli.

13 Zerubabeli alikuwa baba yake Abiudi.

Abiudi alikuwa baba yake Eliakimu.

Eliakimu alikuwa baba yake Azori.

14 Azori alikuwa baba yake Sadoki.

Sadoki alikuwa baba yake Akimu.

Akimu alikuwa baba yake Eliudi.

15 Eliudi alikuwa baba yake Eliazari.

Eliazari alikuwa baba yake Matani.

Matani alikuwa baba yake Yakobo.

16 Yakobo alikuwa baba yake Yusufu,

Yusufu alikuwa mume wa Mariamu.

Na Mariamu alimzaa Yesu, anayeitwa Masihi.

17 Kulikuwa na vizazi kumi na nne kuanzia kwa Ibrahimu mpaka kwa Daudi. Na kulikuwa na vizazi kumi na nne kuanzia kwa Daudi mpaka wakati wa uhamisho wa Babeli. Na palikuwa na vizazi kumi na nne tangu uhamisho wa Babeli mpaka wakati alipozaliwa Yesu, Masihi.

Kuzaliwa kwa Yesu, Masihi

(Lk 2:1-7)

18 Kuzaliwa kwa Yesu Masihi, kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alikuwa amechumbiwa na Yusufu. Kabla hawajaoana, Yusufu aligundua kuwa Mariamu alikuwa mja mzito. (Yeye alipata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.) 19 Kwa kuwa Yusufu alitaka kufanya kile kilichokuwa, alikusudia kumwacha Mariamu kwa siri bila ya kumvunjia heshima.

20 Lakini baada ya Yusufu kuliwazia jambo hili, Malaika wa Bwana alimjia katika ndoto na akamwambia, “Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu awe mke wako. Mimba aliyonayo ameipata kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Atamzaa mwana, nawe utamwita Yesu.[c] Utampa jina hilo Yesu kwa sababu yeye atawaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”

22 Haya yote yalitokea ili kutimiza maneno ambayo Bwana aliyasema kupitia kwa nabii aliposema:

23 “Sikiliza! Msichana bikira atapata mimba
    na atazaa mtoto wa kiume.
    Mtoto huyo ataitwa Emanueli.”(A)

(Yaani “Mungu yu pamoja nasi”.)

24 Yusufu alipoamka alifanya kama alivyoelekezwa na Malaika wa Bwana. Alimuoa Mariamu. 25 Lakini hakukutana naye kimwili mpaka Mariamu alipomzaa mwana. Na Yusufu akamwita Yesu.

Wenye Hekima Waja Kumwona Yesu

Yesu alizaliwa katika mji wa Bethlehemu ya Uyahudi wakati Herode alipokuwa mfalme. Baada ya Yesu kuzaliwa, baadhi ya wenye hekima kutoka mashariki walikuja Yerusalemu. Walipofika wakawauliza watu, “Yuko wapi mtoto aliyezaliwa ili awe Mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota ilipochomoza na kutuonesha kuwa amezaliwa. Nasi tumekuja ili tumwabudu.”

Mfalme Herode aliposikia haya, yeye pamoja na watu wote wakaao Yerusalemu walikasirika sana. Herode aliitisha mkutano wa wakuu wote wa makuhani wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Akawauliza ni wapi ambapo Masihi angezaliwa. Wakamjibu, “Ni katika mji wa Bethlehemu ya Yuda kama ambavyo nabii aliandika:

‘Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
    wewe ni wa muhimu miongoni mwa watawala wa Yuda.
Ndiyo, mtawala atakayewaongoza
    watu wangu Israeli, atatoka kwako.’”(B)

Kisha Herode akawaita na kufanya mkutano wa siri na wenye hekima kutoka mashariki. Akaelewa kwa usahihi wakati walipoiona nyota. Kisha akawaruhusu waende Bethlehemu. Akawaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto kwa makini na mtakapompata mrudi na kunipa taarifa mahali alipo, ili nami pia niende kumwabudu.”

Wenye hekima walipomsikiliza mfalme, waliondoka. Waliiona tena ile nyota waliyoiona hapo mwanzo na wakaifuata. Nyota ile iliwaongoza mpaka mahali alipokuwa mtoto na kusimama juu ya sehemu hiyo. 10 Wenye hekima walipoona kuwa nyota ile imesimama, walifurahi na kushangilia kwa furaha.

11 Wenye hekima hao kisha waliingia katika nyumba alimokuwamo mtoto Yesu pamoja na Mariamu mama yake. Walisujudu na kumwabudu mtoto. Kisha wakafungua masanduku yenye zawadi walizomletea mtoto. Wakampa hazina za dhahabu, uvumba na manemane. 12 Lakini Mungu aliwaonya wenye hekima hao katika ndoto kuwa wasirudi tena kwa Herode. Hivyo kwa kutii walirudi nchini kwao kwa kupitia njia nyingine.

Yesu Apelekwa Uhamishoni Misri

13 Baada ya wenye hekima kuondoka, malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na kumwambia, “Damka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake ukimbilie Misri kwa sababu Herode amedhamiria kumwua mtoto na sasa atatuma watu kumtafuta. Na mkae Misri mpaka nitakapowaambia mrudi.”

14 Hivyo Yusufu alidamka na kutoka kwenda Misri akiwa na mtoto na mama yake. Nao waliondoka usiku. 15 Yusufu na familia yake walikaa huko Misri mpaka Herode alipofariki. Hili lilitukia ili maneno yaliyosemwa na nabii yatimie: “Nilimwita mwanangu atoke Misri.”(C)

Herode Aua Watoto wa Kiume Katika Mji wa Bethlehemu

16 Herode alipoona kuwa wenye hekima wamemfanya aonekane mjinga, alikasirika sana. Hivyo akatoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili au chini ya miaka hiyo katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake. Herode alifahamu kutoka kwa wenye hekima kwamba walikuwa wameiona nyota miaka miwili kabla. 17 Hili likatimiza yale yaliyosemwa na Mungu kupitia nabii Yeremia aliposema:

18 “Sauti imesikika Rama,
    sauti ya kilio na huzuni kuu.
Raheli akiwalilia watoto wake,
    na amekataa kufarijiwa
    kwa sababu watoto wake hawapo tena.”(D)

Yusufu na Familia Yake Warudi Kutoka Misri

19 Wakati Yusufu na familia yake wakiwa Misri, Herode alifariki. Malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto 20 na akamwambia, “Damka! Mchukue mtoto na mama yake urudi Israeli, kwani waliojaribu kumwua mtoto wamekwisha kufa.”

21 Hivyo Yusufu alidamka na kumchukua mtoto Yesu na mama yake na kurudi Israeli. 22 Lakini Yusufu aliposikia kuwa Arkelao alikuwa mfalme wa Yuda baada ya baba yake kufa, aliogopa kwenda huko. Lakini baada ya kuonywa na Mungu katika ndoto, Yusufu aliondoka pamoja na familia yake akaenda sehemu za Galilaya. 23 Alikwenda katika mji wa Nazareti na kukaa huko. Hii ilitokea ili kutimiza maneno yale yaliyosemwa na manabii. Mungu alisema Masihi angeitwa Mnazareti.[d]

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mk 1:1-8; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)

Baadaye, kabla ya miaka mingi kupita, Yohana Mbatizaji alianza kuwahubiri watu ujumbe uliotoka kwa Mungu. Naye alihubiri kutokea maeneo ya nyikani huko Uyahudi. Yohana alisema, “Tubuni na kuibadili mioyo yenu, kwa sababu ufalme wa Mungu umekaribia.” Nabii Isaya alisema kuhusu habari za Yohana Mbatizaji pale aliposema,

“Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.’”(E)

Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi. Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi na wale kutoka maeneo yote yaliyo kando ya Mto Yordani walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.

Mafarisayo na Masadukayo wengi walikwenda kwa Yohana ili wabatizwe. Yohana alipowaona, akasema, “Enyi ninyi nyoka! Ni nani amewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Muibadili mioyo yenu! Na muoneshe kwa vitendo kuwa mmebadilika. Ninajua mnachofikiri. Mnataka akasema kuwa, ‘lakini Ibrahimu ni baba yetu!’ Hiyo haijalishi. Ninawaambia Mungu anaweza kumzalia Ibrahimu watoto kutoka katika mawe haya. 10 Shoka limewekwa tayari kukata shina la mti katika mizizi yake. Kila mti[e] usiozaa matunda mazuri utakatwa vivyo hivyo na kutupwa motoni.

11 Mimi ninawabatiza kwa maji kuonesha kuwa mmebadilika mioyoni mwenu na pia maishani mwenu. Lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12 Naye atakuja akiwa tayari kwa ajili ya kuisafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri kutoka kwenye makapi,[f] na kisha ataiweka nafaka nzuri kwenye ghala yake. Kisha atayachoma makapi kwa moto usiozimika.”

Yohana Ambatiza Yesu

(Mk 1:9-11; Lk 3:21-22)

13 Ndipo Yesu alitoka Galilaya na kwenda Mto Yordani. Alikwenda kwa Yohana, akitaka kubatizwa. 14 Lakini Yohana alijaribu kumzuia. Yohana akamwambia Yesu, “Kwa nini unakuja kwangu ili nikubatize? Mimi ndiye ninayepaswa kubatizwa na wewe!”

15 Yesu akajibu, “Acha iwe hivyo kwa sasa. Tunapaswa kuyatimiza mapenzi ya Mungu.” Ndipo Yohana akakubali.

16 Hivyo Yesu akabatizwa. Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, mbingu zilifunguka na akamwona Roho Mtakatifu akishuka kutoka mbinguni kama hua[g] na kutua juu yake. 17 Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu, nimpendaye. Ninapendezwa naye.”

Yesu Ajaribiwa na Shetani

(Mk 1:12-13; Lk 4:1-13)

Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza Yesu hadi nyikani ili akajaribiwe na Shetani. Baada ya Yesu kufunga kwa siku arobaini mchana na usiku, akaumwa njaa sana. Mjaribu[h] akamwendea na akasema, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, basi yaamuru mawe haya yawe mikate.”

Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Mungu.’”(F)

Kisha Shetani alimwongoza Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na akamweka juu ya mnara wa Hekalu. Akamwambia Yesu, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe mpaka chini! Kwani Maandiko yanasema,

‘Mungu atawaamuru malaika zake wakusaidie,
na mikono yao itakupokea,
    ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’”(G)

Yesu akamjibu, “Pia, Maandiko yanasema, ‘usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(H)

Kisha Shetani akamwongoza Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima ulio mrefu sana na kumwonyesha falme zote za ulimwengu na vitu vya kupendeza vilivyomo ndani. Shetani akamwambia Yesu, “Ukiinama na kuniabudu, nitakupa vitu hivi vyote.”

10 Yesu akamjibu Shetani akamwambia, “Ondoka kwangu Shetani! Kwani Maandiko yanasema, ‘Umwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake!’”(I)

11 Baada ya hayo, Shetani akamwacha. Ndipo malaika wakaja kumhudumia.

Yesu Aanza Kazi yake Galilaya

(Mk 1:14-15; Lk 4:14-15)

12 Yesu aliposikia kuwa Yohana alikuwa amefungwa gerezani, alirudi katika wilaya ya Galilaya. 13 Lakini aliondoka Nazareti. Alikwenda kuishi Kapernaumu, mji ulio kando kando ya Ziwa Galilaya katika eneo la Zabuloni na Naftali. 14 Hili lilitokea ili kutimiza maneno aliyosema nabii Isaya:

15 “Sikilizeni, enyi nchi ya Zabuloni na Naftali,
    nchi iliyo kando ya barabara iendayo baharini,
    ng'ambo ya Mto Yordani!
    Galilaya, wanapokaa Mataifa.
16 Watu wanaoishi katika giza ya kiroho,
    nao wameiona nuru iliyo kuu.
Nuru hiyo imeangaza kwa ajili yao wale
    wanaoishi katika nchi yenye giza kama kaburi.”(J)

17 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaambia watu ujumbe wake unaosema, “Mbadili mioyo yenu na maisha yenu pia, kwa sababu Ufalme wa Mungu umewafikia.”

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mk 1:16-20; Lk 5:1-11)

18 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni, aitwaye Petro na nduguye aitwaye Andrea. Ndugu hawa walikuwa wavuvi na walikuwa wanavua samaki kwa nyavu zao. 19 Yesu akawaambia, “Njooni, mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine. Nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 20 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata Yesu papo hapo.

21 Yesu akaendelea kutembea kutoka pale. Akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo. Walikuwa kwenye mashua pamoja na Zebedayo baba yao. Walikuwa wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. Yesu akawaita wamfuate. 22 Mara moja wakaiacha mashua pamoja na baba yao na wakamfuata Yesu.

Yesu Afundisha na Kuponya Watu

(Lk 6:17-19)

23 Yesu alikwenda sehemu zote za Galilaya, akifundisha na akihubiri Habari Njema katika masinagogi kuhusu Ufalme wa Mungu. Aliponya magonjwa yote na madhaifu mengi ya watu. 24 Habari kuhusu Yesu zilienea katika nchi yote ya Shamu, na watu waliwaleta wale wote wenye kuteswa na magonjwa na maumivu mbalimbali. Baadhi yao walikuwa na mashetani, wengine walikuwa na kifafa na wengine walikuwa wamepooza. Yesu akawaponya wote. 25 Makundi makubwa ya watu walimfuata; watu kutoka Galilaya, na jimbo lililoitwa Miji Kumi,[i] Yerusalemu, Yuda na maeneo ng'ambo ya Mto Yordani.

Mafundisho ya Yesu Mlimani

(Lk 6:20-23)

Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda kwenye kilima na kukaa chini. Wanafunzi wake walimjia Yesu. Kisha Yesu akaanza kuwafundisha watu kwa akasema:

“Heri[j] kwa walio maskini na wenye kujua kwamba wanamhitaji Mungu.[k]
    Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao.
Heri kwa wenye huzuni sasa.
    Kwa kuwa watafarijiwa na Mungu.
Heri kwa walio wapole.
    Kwa kuwa watairithi nchi.[l]
Heri kwa wenye kiu na njaa ya kutenda haki.[m]
    Kwa kuwa Mungu ataikidhi kiu na njaa yao.
Heri kwa wanaowahurumia wengine.
    Kwa kuwa watahurumiwa pia.
Heri kwa wenye moyo safi,[n]
    Kwa kuwa watamwona Mungu.
Heri kwa wanaotafuta amani.[o]
    Kwa kuwa wataitwa watoto wa Mungu.
10 Heri kwa wanaoteswa kwa sababu ya kutenda haki.
    Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao.

11 Heri kwenu ninyi pale watu watakapowatukana na kuwatesa. Watakapodanganya na akasema kila neno baya juu yenu kwa kuwa mnanifuata mimi. 12 Furahini na kushangilia kwa sababu thawabu kuu inawasubiri mbinguni. Furahini kwa kuwa ninyi ni kama manabii walioishi zamani. Watu waliwatendea wao mambo mabaya kama haya pia.

Ninyi ni Kama Chumvi na Nuru

(Mk 9:50; 4:21; Lk 14:34-35; 8:16)

13 Mnahitajika kama chumvi inavyohitajiwa na wale waliopo duniani. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, haiwezi kufanywa chumvi tena. Haina manufaa yo yote isipokuwa hutupwa nje na kukanyagwa na watu.

14 Ninyi ni nuru inayong'aa ili ulimwengu uweze kuiona. Ni kama mji uliojengwa juu ya kilima unavyoonekana wazi. 15 Watu hawawashi taa na kuificha kwenye chungu. Bali huiweka kwenye kinara cha taa ili nuru iangaze kwa kila mtu. 16 Kwa namna hiyo hiyo mnapaswa kuwa nuru kwa ajili ya watu wengine. Hivyo ishini katika namna ambayo watakapoyaona matendo yenu mema, watamtukuza Baba yenu wa mbinguni.

Yesu Afundisha Kuhusu Sheria ya Musa

17 Msifikiri kwamba nimekuja kuiharibu Sheria ya Musa au mafundisho ya manabii. Sikuja kuyaharibu mafundisho yao bali kuyakamilisha. 18 Ninawahakikishia kuwa hakuna jambo litakaloondolewa katika sheria mpaka mbingu na nchi zitakapopita. Hakuna hata herufi ndogo ama nukta katika Sheria ya Musa itakayotoweka mpaka hapo itakapotimizwa.

19 Kila mtu anapaswa kutii kila amri iliyo katika sheria, hata ile isiyoonekana kuwa ya muhimu. Kila atakayevunja mojawapo ya amri hizi ndogo na kuwafundisha wengine kuzivunja atahesabiwa kuwa ni mdogo sana katika ufalme wa Mungu. Lakini kila anayeitii na kuwafundisha wengine kuitii sheria atakuwa mkuu katika ufalme wa Mungu. 20 Ninawambia, ni lazima muitii sheria ya Mungu kwa kiwango bora kuliko kile cha walimu wa sheria na Mafarisayo. La sivyo, hamtaweza kuingia katika ufalme wa Mungu.

Yesu Afundisha Kuhusu Hasira

21 Mmesikia kuwa hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Usimwue yeyote. Na yeyote atakayeua atahukumiwa.’(K) 22 Lakini ninawaambia, msimkasirikie mtu yeyote kwa sababu mkifanya hivyo mtahukumiwa. Na mkimtukana mtu yeyote, vivyo hivyo mtahukumiwa na baraza kuu. Na ukimwita mtu kuwa ni mjinga, utakuwa katika hatari ya kutupwa kwenye moto wa Jehanamu.

23 Unapokwenda kutoa sadaka yako madhabahuni na ukakumbuka kuwa kuna mtu ana jambo dhidi yako. 24 Unapaswa kuiacha sadaka yako kwenye madhabahu na uende kupatana na mtu huyo. Ukiisha patana naye ndipo urudi na kuitoa sadaka hiyo.

25 Akiwepo mtu anayetaka kukushtaki, patana naye haraka. Jitahidi kufanya hivyo kabla ya kufika mahakamani, hata kama bado mpo njiani. Usipofanya hivyo anaweza kukupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakupeleka kwa walinzi watakaokufunga gerezani. 26 Ninakuhakikishia kuwa hautatoka huko mpaka umelipa kila kitu unachodaiwa.

Yesu Afundisha Kuhusu Uzinzi

27 Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Usizini’.(L) 28 Lakini ninawaambia kuwa mwanaume akimwangalia mwanamke na akamtamani, amekwisha kuzini naye katika akili yake. 29 Jicho la kuume likikufanya utende dhambi, liondoe na ulitupe. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote ukatupwa Jehanamu. 30 Na mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, uukate na kuutupa. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote kutupwa Jehanamu.

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Mt 19:9; Mk 10:11-12; Lk 16:18)

31 Ilisemwa pia kuwa, ‘Kila anayemtaliki mkewe ni lazima ampe hati ya talaka.’(M) 32 Lakini ninawaambia kuwa, kila atakayemtaliki mkewe kutokana na sababu isiyohusiana na uzinzi, anamfanya mke wake kuwa mzinzi. Na kila atakayemwoa mwanamke aliyetalikiwa, atakuwa anazini.

Yesu Afundisha Kuhusu Kiapo

33 Pia, mmesikia hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Unaweka kiapo, usishindwe kutimiza kile ulichoapa kufanya. Timiza kiapo ulichoweka mbele za Bwana.’ 34 Lakini ninawaambia mnapoweka ahadi, msiape kwa jina la mbingu, kwa sababu mbingu ni kiti cha enzi cha Mungu. 35 Na usiape kwa jina la dunia kwa sababu, dunia ni mahali pa kuweka miguu yake. Wala msiape kwa jina la mji wa Yerusalemu, kwa sababu nao ni mali yake Mungu, aliye Mfalme Mkuu. 36 Pia usiape kwa jina la kichwa chako kana kwamba ni uthibitisho kuwa utatimiza kiapo, kwa sababu huwezi kuufanya hata unywele mmoja wa kichwa chako kuwa mweusi au mweupe. 37 Sema ‘ndiyo’ tu kama una maana ya ndiyo na ‘hapana’ tu kama una maana ya hapana. Ukisema zaidi ya hivyo, utakuwa unatoa kwa Yule Mwovu.

Yesu Afundisha Kuhusu Kisasi

(Lk 6:29-30)

38 Mmesikia ilisemwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’(N) 39 Lakini ninawaambia msishindane na yeyote anayetaka kuwadhuru. Mtu akikupiga shavu la kulia mgeuzie na la kushoto pia. 40 Mtu akitaka kukushitaki ili akunyang'anye shati, mpe na koti pia. 41 Askari akikulazimisha kwenda naye maili moja,[p] nenda maili mbili pamoja naye. 42 Mpe kila anayekuomba, usimkatalie anayetaka kuazima kitu kwako.

Wapende Adui Zako

(Lk 6:27-28,32-36)

43 Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Wapende rafiki zako(O) na wachukie adui zako.’ 44 Lakini ninawaambia wapendeni adui zenu na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 45 Mkifanya hivi mtakuwa watoto halisi walio kama Baba yenu wa mbinguni. Yeye huwaangazia jua watu wote, bila kujali ikiwa ni wema au wabaya. Huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Ikiwa mnawapenda wale wanaowapenda ninyi, kwa nini mpate thawabu toka kwa Mungu? Hata watoza ushuru hufanya hivyo. 47 Na ikiwa mnakuwa wema kwa rafiki zenu tu, ninyi si bora kuliko wengine. Hata watu wasiomjua Mungu ni wakarimu kwa rafiki zao pia. 48 Ninalosema ni kuwa, mkue hata kufikia upendo kamili[q] alionao baba yenu wa Mbinguni kwa watu wote.

Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa

Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.

Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[r] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[s] Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.

Yesu Afundisha Kuhusu Maombi

(Lk 11:2-4)

Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.

Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba:

‘Baba yetu uliye mbinguni,
    Jina lako lipewe utukufu.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa dunia,
    kama yanavyofanyika huko mbinguni.
11 Utupe leo chakula tunachohitaji.
12 Utusamehe dhambi zetu,
    kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea.
13 Usiruhusu tukajaribiwa,
    lakini utuokoe na Yule Mwovu.’[t]

14 Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. 15 Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi.

Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga

16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17 Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18 ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.

Huwezi Kuwatumikia Mabwana Wawili

(Lk 12:33-34; 11:34-36; 16:13)

19 Msijiwekee hazina hapa duniani, mahali nondo na kutu[u] huiharibu. Na wezi wanaweza kuvunja nyumba yako na kuziiba. 20 Badala yake jiwekeeni hazina mbinguni ambako haziwezi kuharibiwa na nondo wala kutu na ambako wezi hawawezi kuvunja na kuziiba. 21 Kwa kuwa roho yako itakuwa mahali ilipo hazina yako.

22 Jinsi unavyowaangalia watu wengine ndivyo inavyoonyesha jinsi wewe mwenyewe ulivyo ndani yako. Ukiwaangalia watu kwa nia njema utajawa na nuru ndani yako. 23 Lakini ukiwaangalia watu kwa nia mbaya, utajawa na giza ndani yako. Na ikiwa yote yanayoonekana ndani yako ni giza peke yake, basi unalo giza baya zaidi![v]

24 Hamwezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Mtamchukia mmoja na kumpenda yule mwingine au mtakuwa waaminifu kwa mmoja na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na pesa.[w]

Utangulizeni Kwanza Ufalme wa Mungu

(Lk 12:22-34)

25 Kwa hiyo ninawaambia, msiyahangaikie mahitaji ya mwili; mtakula nini, mtakunywa nini au mtavaa nini. Uhai ni zaidi ya chakula na mavazi. 26 Waangalieni ndege wa angani. Hawapandi, hawavuni wala kutunza chakula ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, hamjui kuwa ninyi mna thamani zaidi ya ndege? 27 Hamwezi kujiongezea muda wa kuishi kwa kujisumbua.

28 Na kwa nini mna wasiwasi kuhusu mavazi? Yaangalieni maua ya kondeni. Yatazameni namna yanavyomea. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. 29 Lakini ninawaambia kuwa hata Suleimani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya maua haya. 30 Ikiwa Mungu anayafanya majani yanayoota mashambani kuwa mazuri mnafikiri atawafanyia ninyi kitu gani? Hayo ni majani tu, siku moja yako hai na siku inayofuata hutupwa katika moto. Lakini Mungu anajali kiasi cha kuyafanya kuwa mazuri ya kupendeza. Muwe na hakika basi atawapa ninyi mavazi mnayohitaji. Imani yenu ni ndogo sana!

31 Msijisumbue na kusema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Haya ndiyo mambo ambayo watu wasiomjua Mungu huyawazia daima. Msiwe na wasiwasi, kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnayahitaji haya yote. 33 Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na mambo yote ambayo Mungu anahesabu kuwa ni mema na yenye haki. Ndipo Mungu atakapowapa yote mnayohitaji. 34 Msiisumbukie kesho. Kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Kila siku ina mahangaiko yake ya kutosha.

Iweni Waangalifu Mnapokosoa Wengine

(Lk 6:37-38,41-42)

Msiwahukumu wengine, ili Mungu asiwahukumu ninyi pia. Mtahukumiwa jinsi ile ile mnavyowahukumu wengine. Mungu atawatendea kama mnavyowatendea wengine.

Kwa nini unaona vumbi iliyo katika jicho la rafiki yako, na hujali kipande cha mti kilicho katika jicho lako? Kwa nini unamwambia rafiki yako, ‘Ngoja nitoe vumbi lililo katika jicho lako wakati wewe mwenyewe bado una kipande cha mti katika jicho lako?’ Ewe mnafiki! Ondoa kwanza kipande cha mti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utaweza kuona vizuri na kutoa vumbi katika jicho la rafiki yako.

Msiwape mbwa kitu kitakatifu, watawageuka na kuwadhuru. Na msiwatupie nguruwe lulu zenu kwa kuwa watazikanyaga tu.

Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji

(Lk 11:9-13)

Endeleeni kumwomba Mungu, naye atawapa, endeleeni kutafuta nanyi mtapata, endeleeni kubisha nanyi mtafunguliwa mlango. Ndiyo, yeyote anayeendelea kuomba atapokea. Yeyote anayeendelea kutafuta atapata. Na yeyote anayeendelea kubisha atafunguliwa mlango.

Ni nani kati yenu aliye na mwana ambaye akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au akimwomba samaki, atampa nyoka? Bila shaka hakuna! 11 Ijapokuwa ninyi watu ni waovu, lakini bado mnajua kuwapa vitu vyema watoto wenu. Hakika Baba yenu wa mbinguni atawapa vitu vyema wale wamwombao.

Kanuni ya Muhimu Sana

12 Watendee wengine kama ambavyo wewe ungetaka wao wakutendee. Hii ndiyo tafsiri ya torati[x] na mafundisho ya manabii.

Wachache tu Ndiyo Huiona Njia ya Uzima

(Lk 13:24)

13 Unapaswa kuingia katika uzima wa kweli kupitia lango lililo jembamba. Kwa kuwa lango ni pana na njia inayoelekea katika uharibifu nayo ni pana na watu wengi wanaifuata njia hiyo. 14 Lakini lango la kuelekea katika uzima wa kweli ni jembamba. Na njia iendayo huko ni ngumu kuifuata. Na ni watu wachache wanaoiona.

Kile Wanachokifanya watu Kinadhihirisha jinsi gani Walivyo

(Lk 6:43-44; 13:25-27)

15 Mjihadhari na manabii wa uongo wanaokuja kwenu wakijifanya kondoo wasio na madhara ingawa ni watu hatari kama mbwa mwitu. 16 Mtawatambua watu hawa kwa matendo yao. Mambo mazuri hayatoki kwa watu wabaya, kama ambavyo zabibu haitokani na miiba, na tini hazitokani na mbigiri. 17 Vile vile, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. 20 Mtawatambua manabii hawa wa uongo kwa matendo yao.

21 Si kila aniitaye Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu. Watakaoingia ni wale tu wafanyao yale ambayo Baba yangu wa mbinguni anataka. 22 Siku ya mwisho wengi wataniiita Bwana. Watasema, ‘Bwana, kwa nguvu za jina lako tulihubiri. Na kwa nguvu za jina lako tulitoa mashetani na kufanya miujiza mingi.’ 23 Ndipo nitawaambia waziwazi, ‘Ondokeni kwangu, ninyi waovu. Sikuwahi kuwajua.’

Aina Mbili za Watu

(Lk 6:47-49)

24 Kila anayeyasikia mafundisho yangu na kuyatii ni kama mwenye hekima aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko yakaja, na upepo ukavuma sana, na kuipiga sana nyumba yake. Lakini, nyumba yake haikuanguka kwa sababu ilijengwa kwenye mwamba.

26 Lakini kila anayeyasikia mafundisho yangu na asiyatii ni kama mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko kuja, na upepo ukavuma sana, nyumba yake ilianguka kwa kishindo kikuu.”

28 Yesu alipomaliza kufundisha, watu walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. 29 Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[y]

Yesu Amponya Mgonjwa

(Mk 1:40-45; Lk 5:12-16)

Yesu alipotelemka kutoka kwenye kilima, umati mkubwa wa watu ulimfuata. Mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea, akainama mbele yake mpaka chini na akasema, “Bwana ukitaka una uwezo wa kuniponya.”

Yesu aliunyoosha mkono wake akamshika mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Akasema, “Hakika, ninataka kukuponya. Upone!” Mtu huyo akapona ugonjwa mbaya sana wa ngozi saa hiyo hiyo. Kisha Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea, lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.[z] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”

Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi

(Lk 7:1-10; Yh 4:43-54)

Yesu alikwenda Kapernaumu. Alipoingia mjini, afisa wa jeshi alimjia na kumwomba msaada. Akasema, “Bwana, mtumishi wangu ni mgonjwa sana nyumbani na amelala kitandani. Hawezi hata kutingishika na ana maumivu makali sana.”

Yesu akamwambia yule afisa, “Nitakwenda nimponye.”

Yule afisa akajibu, “Bwana, mimi si mwema kiasi cha wewe kuingia katika nyumba yangu. Toa amri tu, na mtumishi wangu atapona. Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”

10 Yesu aliposikia maneno hayo alishangaa. Akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye, “Ukweli ni kuwa, mtu huyu ana imani kuliko mtu yeyote niliyewahi kumwona katika Israeli. 11 Watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi na kula pamoja na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo katika ufalme wa Mungu. 12 Na wale wanaopaswa kuwa katika ufalme watatupwa nje gizani. Na huko watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”

13 Kisha Yesu akamwambia yule afisa, “Rudi nyumbani kwako. Mtumishi wako atapona kama unavyoamini.” Mtumishi wa afisa huyo akapona wakati ule ule.

Yesu Awaponya Watu Wengi

(Mk 1:29-34; Lk 4:38-41)

14 Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa na homa. 15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, kisha akasimama na kuanza kumhudumia.

16 Ilipofika jioni, watu wengi waliokaliwa na mashetani waliletwa kwa Yesu. Naye aliyaamuru mashetani hayo kuwaacha watu. Na aliowaponya wagonjwa wote. 17 Hii ilitokea ili kutimiza maneno yaliyosemwa na nabii Isaya aliposema:

“Aliyaondoa magonjwa yetu
    na kuyabeba madhaifu yetu.”(P)

Kumfuata Yesu

(Lk 9:57-62)

18 Yesu alipoona kundi la watu waliomzunguka, aliawaambia wafuasi waende upande mwingine wa ziwa. 19 Kisha, mwalimu wa sheria ya Musa akamwendea na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kila mahali utakapokwenda.”

20 Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo wanamoishi, ndege wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kupumzika.”

21 Mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana mimi pia nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”

22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate mimi, na uwaache wale waliokufa wawazike wafu wao.”

Yesu Atuliza Dhoruba

(Mk 4:35-41; Lk 8:22-25)

23 Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake. 24 Baada ya mashua kutoka pwani, upepo wenye nguvu sana ukaanza kuvuma ziwani. Mawimbi yakaifunika mashua. Lakini Yesu alikuwa amelala. 25 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha. Wakamwambia, “Bwana tuokoe! Tutazama majini!”

26 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Hamna imani ya kutosha.” Yesu akasimama akaukemea upepo na mawimbi, na ziwa likatulia.

27 Wanafunzi wake wakashangaa sana, wakasema, “Huyu ni mtu wa namna gani? Hata upepo na maji vinamtii!”

Yesu Afukuza Mashetani Kutoka Kwa Watu Wawili

(Mk 5:1-20; Lk 8:26-39)

28 Yesu alifika ng'ambo ya ziwa katika nchi walimoishi Wagadarini.[aa] Hapo wanaume wawili waliokuwa na mashetani ndani yao na kuishi makaburini walimwijia Yesu. Watu hao walikuwa hatari sana na watu hawakuitumia njia iliyopita karibu na makaburi yale. 29 Wakapaza sauti na akasema, “Unataka nini kwetu, Mwana wa Mungu? Umekuja kutuadhibu kabla ya wakati uliopangwa?”

30 Mbali kidogo na mahali hapo lilikuwepo kundi la nguruwe waliokuwa wanapata malisho yao. 31 Mashetani yakamsihi Yesu yakasema, “Ikiwa utatufukuza kutoka ndani ya watu hawa, tafadhali tuache tuwaingie wale nguruwe.”

32 Ndipo akawaamuru na akasema, “Nendeni!” Wale mashetani wakatoka ndani ya wale watu na kuwaingia nguruwe. Kisha kundi lote la nguruwe likaporomoka ziwani na nguruwe wote wakazama na kufa. 33 Wachungaji waliokuwa wakiwachunga wale nguruwe wakakimbia. Wakaenda mjini na kuwaambia watu kila kitu kilichotukia, hasa juu ya wanaume wale wawili waliokuwa na mashetani. 34 Kisha watu wote mjini walikwenda kumwona Yesu. Walipomwona, walimsihi aondoke katika eneo lao.

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mk 2:1-12; Lk 5:17-26)

Yesu akapanda katika mashua na akasafiri kwa kukatisha ziwa kurudi kwenye mji wake. Baadhi ya watu wakamletea mtu aliyepooza akiwa amelala kwenye machela. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Changamka mtoto wangu! Dhambi zako zimesamehewa.”

Baadhi ya walimu wa sheria walisikia alichosema Yesu. Wakaambizana wao kwa wao, “Si anamtukana Mungu mtu huyu akasema hivyo!”

Yesu alipotambua walichokuwa wanafikiri, akasema, “Kwa nini mna mawazo maovu kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kitanda chako na utembee’? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kitanda chako uende nyumbani!’”

Mtu yule akasimama na kwenda nyumbani. Watu walipoliona tukio hili wakashangaa. Wakamsifu Mungu kwa kuwapa watu mamlaka hii.

Mathayo Amfuata Yesu

(Mk 2:13-17; Lk 5:27-32)

Yesu alipokuwa anaondoka, alimwona mtu aliyeitwa Mathayo amekaa mahali pa kukusanyia ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Hivyo Mathayo akasimama na kumfuata Yesu.

10 Baadaye Yesu alikula chakula nyumbani kwa Mathayo. Watoza ushuru wengi na watu wenye sifa mbaya walikuja na kula chakula pamoja na Yesu pamoja na wafuasi wake. 11 Mafarisayo walipoona kuwa Yesu anakula pamoja na watu hao, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”

12 Yesu alipowasikia wakisema hili, akawaambia, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari si wenye afya. 13 Nendeni mkajifunze andiko hili linamaanisha nini: ‘Sihitaji dhabihu ya mnyama; Ninataka ninyi mwoneshe wema kwa watu.’(Q) Sikuja kuwaalika wema kujiunga nami, bali wenye dhambi.”

Swali Kuhusu Kufunga

(Mk 2:18-22; Lk 5:33-39)

14 Kisha wafuasi wa Yohana wakamjia Yesu na kusema, “Sisi na Mafarisayo tunafunga mara kwa mara, lakini wafuasi wako hawafungi. Kwa nini?”

15 Yesu akajibu, “Kwenye harusi marafiki wa bwana harusi hawana huzuni anapokuwa pamoja nao, hivyo hawawezi kufunga. Lakini wakati unakuja ambao bwana harusi ataondolewa kwao. Ndipo watakuwa na huzuni kisha watafunga.

16 Mtu anaposhona kiraka kwenye vazi la zamani, atatumia kiraka chakavu. Akitumia kiraka kipya vazi lake litachanika kwa sababu ya kusinyaa kwa kiraka hicho kipya. Kisha tundu litakuwa baya zaidi. 17 Pia, watu hawawaweki divai mpya kwenye viriba[ab] vya zamani. Wakifanya hivyo viriba vitapasuka, na divai itamwagika na viriba vitaharibika. Daima watu huweka divai mpya katika viriba vipya, ambavyo haviwezi kupasuka, na divai huwa salama.”

Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa

(Mk 5:21-43; Lk 8:40-56)

18 Yesu alipokuwa bado anaongea, kiongozi wa sinagogi akamwendea. Kiongozi akainama chini mbele yake na akasema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini ikiwa utakuja na kumgusa kwa mkono wako, atafufuka.”

19 Hivyo Yesu na wafuasi wake wakaenda na mtu huyo.

20 Wakiwa njiani, alikuwepo mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili. Alimwendea Yesu kwa nyuma na akagusa sehemu ya chini ya vazi lake. 21 Aliwaza, “Ikiwa nitagusa tu joho lake, nitapona.”

22 Yesu aligeuka na kumwona mwanamke. Akasema, “Uwe na furaha, mwanamke. Imani yako imekuponya.” Kisha yule mwanamke akapona saa ile ile.

23 Yesu aliendelea kwenda na kiongozi wa Kiyahudi na kuingia nyumbani kwake. Aliwaona watu wapigao muziki kwa ajili ya mazishi pale. Na aliliona kundi la watu waliohuzunika sana. 24 Yesu akasema, “Ondokeni. Msichana hajafa. Amelala tu.” Lakini watu wakamcheka. 25 Baada ya watu kutolewa nje ya nyumba, Yesu aliingia kwenye chumba cha msichana. Aliushika mkono wa msichana na msichana akasimama. 26 Habari kuhusu jambo hili ilienea kila mahali katika eneo lile.

Yesu Awaponya Watu Watatu

27 Yesu alipokuwa anaondoka kutoka pale, wasiyeona wawili walimfuata. Walisema kwa sauti, “Mwana wa Daudi, uwe mwema kwetu.”

28 Baada ya Yesu kuingia ndani, wasiyeona wakamwendea. Akawauliza, “Mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone?” Wakajibu, “Ndiyo, Bwana, tunaamini.”

29 Kisha Yesu akayagusa macho yao na akasema, “Kwa kuwa mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone, hivyo itatokea.” 30 Ndipo wakaweza kuona. Yesu akawaonya kwa nguvu. Akasema, “Msimwambie yeyote kuhusu hili.” 31 Lakini waliondoka na kutawanya habari kuhusu Yesu kila mahali katika eneo lile.

32 Watu hawa wawili walipokuwa wanaondoka, baadhi ya watu walimleta mtu mwingine kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa haongei kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. 33 Yesu akamtoa nje pepo na mtu yule aliweza kuongea. Watu walishangaa na akasema, “Hakuna mtu yeyote aliyewahi kuona kitu kama hiki katika Israeli.”

34 Lakini Mafarisayo walisema, “Mtawala wa mashetani ndiye anayempa nguvu ya kuyatoa mashetani.”

Mwombeni Mungu Atume Watenda Kazi Zaidi

35 Yesu alisafiri akipita katika miji yote na vijiji. Alifundisha katika masinagogi yao na kuwaeleza watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Aliponya kila aina ya magonjwa na udhaifu. 36 Yesu aliona watu wengi na kuwahurumia kwa sababu walikuwa wanakandamizwa na hawakuwa na tumaini; kama kondoo bila mchungaji wa kuwaongoza. 37 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kuna mavuno mengi ya watu ya kuleta. Lakini kuna wafanyakazi wachache wa kusaidia kuwavuna. 38 Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni atume wafanyakazi wengi zaidi wa kusaidia kukusanya mavuno yake.”

Footnotes

  1. 1:1 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Kristo”, tafsiri ya Kiyunani kwa neno “Masihi”. Tazama Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 16-17 na katika kitabu chote hiki.
  2. 1:11 baba wa Yekonia Mfalme Nebukadneza aliuangusha mji wa Yerusalemu na kuvunja hekalu mwaka 586 KK na kuwapeleka Babeli wakiwa mateka watu Mashuhuri pamoja na vyombo vya thamani vilivyokuwa hekaluni. Tazama 1 Nya 3:15-16.
  3. 1:21 Yesu Jina la Yesu maana yake “Bwana anayeokoa”.
  4. 2:23 Mnazareti Mtu anayetoka katika mji wa Nazareti. Jina hili linafanana na neno la Kiebrania linalomaanisha “tawi”. Hivyo inawezekana Mathayo anamaanisha ahadi ya “tawi” la ukoo wa Daudi. Tazama Isa 11:1. Yer 23:5; 33:15; Zek 3:8; 6:12.
  5. 3:10 mti Watu wasiomtii Mungu ni kama “miti” itakayokatwa.
  6. 3:12 Atatenganisha nafaka … makapi Inamaanisha kuwa Yesu atawatenganisha watu wema na waovu.
  7. 3:16 hua Ndege mfano wa njiwa, aendaye kwa kasi au “njiwa pori”, “tetere”.
  8. 4:3 Mjaribu Kwa maana ya kawaida, “Shetani”.
  9. 4:25 Miji Kumi Jimbo hili lilikuwa mashariki ya Ziwa la Galilaya na wakazi wake hawakuwa Wayahudi. Miji Kumi imejulikana pia kama Dekapoli.
  10. 5:3 Heri Maana yake ni baraka kuu.
  11. 5:3 maskini … wanamhitaji Mungu Kwa maana ya kawaida, “maskini wa roho”, ama wenye uhitaji wa kiroho.
  12. 5:5 watairithi nchi Wataurithi ulimwengu ujao yaani ufalme wa Mungu unaokuja.
  13. 5:6 wenye kiu na njaa ya kutenda haki Kwa maana ya kawaida, “wenye njaa na kiu ya kutenda haki zaidi ya kitu kingine chochote”.
  14. 5:8 wenye moyo safi Au wenye mawazo safi ama wenye kukusudia mema moyoni, ama wenye nia njema moyoni.
  15. 5:9 wanaotafuta amani Au “wapatanishi wa watu waliofarakana”.
  16. 5:41 maili moja Kama kilomita moja na nusu.
  17. 5:48 kamili Neno “kamilifu”, hapa lina maana “imeendelezwa kwa ukamilifu”, na inaelezea aina ya upendo ambao watoto wanaweza kujifunza kutoka kwa baba.
  18. 6:2 makusanyiko Au “masinagogi”.
  19. 6:3 asijue unachofanya Kwa maana ya kawaida, “Mkono wako wa kushoto usijue kile ambacho mkono wako wa kushoto unafanya.”
  20. 6:13 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza: “Kwa kuwa ufalme na nguvu na utukufu ni vyako milele na milele. Amina.”
  21. 6:19 nondo na kutu Pia katika mstari wa 20.
  22. 6:22-23 Kwa maana ya kawaida, 22 Taa ya mwili ni jicho. Hivyo, jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru tele. 23 Lakini jicho lako likiwa na uovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Hivyo ikiwa nuru ndani yako ni giza, giza hilo ni linatisha.
  23. 6:24 pesa Au “mamona”, neno la Kiaramu linalomaanisha “utajiri”.
  24. 7:12 torati Au “Sheria ya Musa”.
  25. 7:29 mamlaka Hakuhitaji mamlaka yoyote zaidi ya kwake. Kinyume chake waandishi daima waliwanukuu walimu wa kale wa Kiyahudi kama mamlaka ya mafundisho yao.
  26. 8:4 kuhani akakuchunguze Sheria ya Musa (torati) ilisema kuhani ni lazima aamue ikiwa mtu amepona ukoma.
  27. 8:28 Wagadarini Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagerasi” na zingine zina “Wagergesini”.
  28. 9:17 viriba Kibuyu au chombo cha kuhifadhia divai au maji kilichotengenezwa kwa ngozi.