Luka 1-10
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka Aandika Kuhusu Maisha ya Yesu
1 Mheshimiwa Theofilo:[a]
Watu wengine wengi wamejaribu kuandika juu ya mambo yaliyotokea katikati yetu ili kuukamilisha mpango wa Mungu. 2 Mambo hayo waliyoyaandika yanalingana na yale tuliyosikia kutoka kwa watu walioyaona tangu mwanzo. Na walimtumikia Mungu kwa kuwaambia wengine ujumbe wake. 3 Nimechunguza kila kitu kwa makini tangu mwanzo. Na nimeona kuwa ni vyema nikuandikie kwa mpangilio mzuri. 4 Nimefanya hivi ili uwe na uhakika kuwa yale uliyofundishwa ni ya kweli.
Malaika Amjulisha Zakaria Kuhusu Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
5 Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi[b] cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. 6 Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. 7 Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana.
8 Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. 9 Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. 10 Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba.
11 Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. 12 Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. 13 Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. 15 Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
16 Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.”
18 Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje kuwa haya unayosema ni ya kweli? Maana mimi ni mzee na mke wangu ana umri mkubwa pia.”
19 Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, ambaye daima husimama mbele za Mungu nikiwa tayari. Amenituma kuzungumza nawe na kukujulisha habari hizi njema. 20 Sasa sikiliza! Hautaweza kuzungumza mpaka siku ambayo mambo haya yatatokea kwa sababu hukuyaamini yale niliyokwambia. Lakini nilichosema hakika kitatokea.”
21 Watu waliokuwa nje ya Hekalu wakimngojea Zakaria walishangaa kwa sababu alikaa kwa muda mrefu ndani ya Hekalu. 22 Zakaria alipotoka nje hakuweza kuzungumza nao. Aliwafanyia watu ishara kwa mikono yake. Hivyo watu walitambua kuwa alikuwa ameona maono alipokuwa Hekaluni. 23 Zamu ya utumishi wake ilipokwisha alirudi nyumbani.
24 Wakati fulani baadaye, Elizabeti, mke wa Zakaria akawa mjamzito. Alikaa katika nyumba yake na hakutoka nje kwa miezi mitano. Alisema, 25 “Na sasa, hatimaye Bwana amenisaidia kwa kuniondolea aibu yangu.”
Malaika Atangaza Kuzaliwa kwa Yesu
26-27 Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. 28 Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.”
29 Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?”
30 Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. 31 Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. 32 Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. 33 Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34 Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.”
35 Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. 37 Mungu anaweza kufanya jambo lolote!”
38 Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka.
Mariamu Amtembelea Elizabeti
39 Mariamu akajiandaa na kwenda haraka katika mji mmoja ulio vilimani katika jimbo la Yuda. 40 Alikwenda nyumbani kwa Zakaria, alipofika akamsalimu Elizabeti. 41 Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akirukaruka, na Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu.
42 Kisha akapaza sauti na kumwambia Mariamu, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini jambo hili kuu limetokeaje kwangu, hata mama wa Bwana wangu aje kwangu? 44 Kwa maana sauti ya salamu yako ilipofika masikioni mwangu, mtoto aliye ndani yangu amerukaruka kwa furaha. 45 Umebarikiwa wewe uliyeamini kuwa mambo aliyokuambia Bwana yatatokea.”
Mariamu Amsifu Mungu
46 Mariamu akasema,
“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47 kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
wangu amenipa furaha kuu!
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
49 Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
Jina lake ni takatifu.
50 Na huwapa rehema zake wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51 Ameonesha nguvu ya mkono wake;
Amewatawanya wanaojikweza.
52 Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
na kuwakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54 Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
Amekumbuka kuonesha rehema;
55 Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
Ibrahimu na wazaliwa wake.”
56 Mariamu alikaa na Elizabeti kwa muda wa kama miezi mitatu, kisha alirudi nyumbani kwake.
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
57 Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. 58 Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye.
59 Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri.[c] Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. 60 Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.”
61 Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” 62 Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto.
63 Zakaria akataka ubao wa kuandikia,[d] Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. 64 Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. 65 Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. 66 Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Zakaria Amsifu Mungu
67 Kisha Zakaria, baba yake Yohana, akajaa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema:
68 “Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amekuja kuwasaidia
watu wake na kuwaweka huru.
69 Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu,
kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi.
70 Hivi ndivyo alivyoahidi
kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani.
71 Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu
na milki za wote wanaotuchukia.
72 Ili kuonesha rehema kwa baba zetu,
na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao.
73 Agano hili ni kiapo alichomwapia
baba yetu Ibrahimu.
74 Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu,
ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu.
75 Katika namna iliyo takatifu na yenye haki
mbele zake siku zote za maisha yetu.
76 Sasa wewe, mtoto mdogo,
utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana,
kwa sababu utamtangulia Bwana
kuandaa njia yake.
77 Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa
kwa kusamehewa dhambi zao.
78 Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu,
siku mpya[e] itachomoza juu yetu kutoka mbinguni.
79 Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza,
kwa hofu ya mauti,
na kuongoza hatua zetu
katika njia ya amani.”
80 Na hivyo mtoto Yohana akakua na kuwa na nguvu katika roho. Kisha akaishi maeneo yasiyo na watu mpaka wakati alipotokea hadharani akihubiri ujumbe wa Mungu kwa watu wa Israeli.
Kuzaliwa kwa Yesu
(Mt 1:18-25)
2 Ulikuwa wakati ambapo amri ilitolewa na Kaisari Augusto kwamba watu wote wanaoishi katika utawala wote wa Rumi[f] wahesabiwe na kuorodheshwa[g] katika kumbukumbu za serikali. 2 Orodha hii ilikuwa ya kwanza tangu Kirenio alipokuwa gavana wa Shamu. 3 Kila mtu alikwenda katika mji aliozaliwa ili akahesabiwe na kuingizwa katika orodha hiyo.
4 Hivyo Yusufu alitoka Nazareti, mji uliokuwa katika jimbo la Galilaya na kwenda katika mji wa Bethlehemu uliokuwa katika jimbo la Uyahudi. Pia, mji huu ulijulikana kama mji wa Daudi. Yusufu alikwenda Bethlehemu kwa sababu alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Daudi. 5 Yusufu alijiandikisha akiwa pamoja na Mariamu kwani alikuwa tayari amemchumbia ili amwoe. Na Mariamu alikuwa mjamzito. 6 Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu kujifungua ulifika. 7 Akamzaa mwanawe wa kwanza. Akamvingirishia nguo vizuri, kisha akamlaza katika hori la kulishia mifugo.[h] Walimweka humo kwa sababu chumba cha wageni kilikuwa kimejaa.
Wachungaji wa Mifugo Wajulishwa Kuhusu Yesu
8 Usiku ule, baadhi ya wachungaji walikuwa mashambani nje ya mji wa Bethlehemu wakilinda kondoo zao. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukaangaza kuwazunguka, wakaogopa sana. 10 Malaika akawaambia, “Msiogope, kwa kuwa nimewaletea habari njema zitakazowafurahisha watu wa Mungu wote. 11 Kwa sababu leo katika mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo,[i] Bwana. 12 Na hivi ndivyo mtakavyomtambua: Mtamkuta mtoto mchanga amevingirishiwa nguo na amelala katika hori la kulishia mifugo.”
13 Kisha malaika pamoja na jeshi kubwa la mbinguni wakaanza kumsifu Mungu, wakisema:
14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na amani iwepo duniani
kwa watu wote wanaompendeza.”
15 Malaika walipoondoka kurudi mbinguni, wale wachungaji wakaambiana wakisema, “Twendeni Bethlehemu, tukalione jambo hili lililotokea, ambalo Bwana ametujulisha.”
16 Wakaenda haraka, wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala katika hori la kulishia mifugo. 17 Wachungaji walipomwona huyo mtoto, walisimulia kile walichoambiwa na malaika kuhusu mtoto. 18 Kila aliyesikia maelezo ya wachungaji, alishangaa. 19 Mariamu aliendelea kuyatafakari mambo haya, na kuyaweka moyoni. 20 Wachungaji waliirudia mifugo yao, wakawa wanamsifu na kumshukuru Mungu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona. Ilikuwa kama walivyoambiwa na malaika.
21 Ilipofika siku ya nane mtoto alitahiriwa, akaitwa Yesu. Hili ndilo jina alilopewa na malaika kabla mama yake hajaibeba mimba yake.
Yesu Atambulishwa Hekaluni
22 Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa.[j] Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. 23 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana.[k] 24 Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua[l] au makinda mawili wa njiwa.”
Simeoni Amwona Yesu
25 Alikuwepo mtu mmoja aliyeishi katika mji wa Yerusalemu, mtu huyu aliitwa Simeoni. Alikuwa mtu mwema na mcha Mungu na Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Alikuwa akiusubiri wakati ambao Mungu angeisaidia Israeli. 26 Roho Mtakatifu alimwambia kwamba asingekufa kabla ya kumwona Masihi kutoka kwa Bwana. 27 Roho Mtakatifu alimwongoza mpaka Hekaluni. Hivyo, alikuwemo Hekaluni wakati Mariamu na Yusufu walipomleta mtoto Yesu ili wamfanyie kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Kiyahudi. 28 Simeoni alimbeba mtoto Yesu mikononi mwake, akamshukuru Mungu na kusema,
29 “Sasa, Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako nife kwa amani
kwa kuwa umeitimiza ahadi yako kwangu.
30 Nimeona kwa macho yangu namna utakavyowaokoa watu wako.
31 Sasa watu wote wanaweza kuuona mpango wako.
32 Yeye ni mwanga wa kuionesha njia yako kwa mataifa mengine,
na atawaletea heshima watu wako Israeli.”
33 Mariamu na Yusufu walishangazwa sana na maneno aliyosema Simeoni kuhusu Yesu. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu; “Wayahudi wengi wataanguka na wengi watainuka kwa sababu ya mtoto huyu. Atakuwa ishara kutoka kwa Mungu, lakini baadhi ya watu watamkataa. 35 Mawazo ya siri ya watu wengi yatajulikana. Na mambo yatakayotokea yatakuumiza, kama upanga unaokuchoma moyoni.”
Ana Amwona Yesu
36 Alikuwapo nabii aliyeitwa Ana binti Fanueli, kutoka katika kabila la Asheri. Alikuwa mwanamke mzee sana. Aliishi na mume wake kwa miaka saba, 37 kabla ya mume wake kufa na kumwacha peke yake. Na sasa alikuwa na umri wa miaka themanini na nne. Ana alikuwa Hekaluni daima, hakutoka. Alimwabudu Mungu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana.
38 Simeoni alipokuwa anazungumza na Yusufu na Mariamu, Ana alikwenda walipokuwa na akaanza kumsifu Mungu na kuwaambia kuhusu Yesu watu wote waliokuwa wanasubiri Mungu kuikomboa Yerusalemu.
Yusufu, Mariamu na Yesu Warudi Nyumbani
39 Yusufu na Mariamu walipotimiza mambo yote yanayotakiwa katika sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, katika mji wao wa Nazareti. 40 Mtoto Yesu aliendelea kukua na kuwa kijana mwenye nguvu na aliyejaa hekima nyingi. Na Mungu alikuwa anambariki.
Yesu Akiwa Mvulana
41 Kila mwaka wazazi wa Yesu walikwenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. 42 Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walikwenda kwenye sikukuu kama ilivyokuwa desturi ya Kiyahudi. 43 Sikukuu ilipokwisha, walirudi nyumbani, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kutambua. 44 Walianza kumtafuta kwa jamaa na rafiki zao baada ya kusafiri kutwa nzima, wakidhani kuwa alikuwa pamoja nao katika msafara. 45 Walipomkosa, walirudi Yerusalemu kumtafuta.
46 Ikawa baada ya siku tatu wakamkuta Hekaluni, amekaa katikati ya walimu wa dini, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Na wote waliomsikiliza walishangazwa sana kwa ufahamu wake na majibu yake ya busara. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa pia, ndipo mama yake akamwambia, “Mwanangu, kwa nini umefanya hivi? Mimi na baba yako tulikuwa na wasiwasi sana, na tumekuwa tukikutafuta.”
49 Yesu akawaambia, “Kwa nini mlikuwa mnanitafuta? Mnapaswa kujua kuwa inanilazimu kuwemo nyumbani mwa Baba yangu?” 50 Lakini wao hawakuelewa alichowaambia.
51 Yesu alirudi pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii. Mama yake aliendelea kuyaweka mambo haya yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu
(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Yh 1:19-28)
3 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo:
Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi;
Herode alikuwa mtawala wa Galilaya;
Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti;
na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene.
2 Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. 3 Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. 4 Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema,
“Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
nyoosheni njia kwa ajili yake.
5 Kila bonde litajazwa,
na kila mlima na kilima vitasawazishwa.
Barabara zilizopinda zitanyooshwa,
na barabara zenye mashimo zitasawazishwa.
6 Na kila mtu ataona
jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’”(A)
7 Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? 8 Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! 9 Na sasa shoka liko tayari kukata miti,[m] kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”
10 Watu wakamwuliza Yohana, “Tufanye nini?”
11 Akajibu, “Ukiwa na mashati mawili mpe moja asiyekuwa na shati. Kama una chakula, kigawe pia.”
12 Hata watoza ushuru walikuja kwa Yohana. Walitaka wabatizwe. Walimwambia, “Mwalimu, tufanye nini sisi?”
13 Akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi kuliko kiwango kilichoamriwa.”
14 Askari wakamwuliza, “Vipi kuhusu sisi? Tufanye nini?”
Akawaambia, “Msitumie nguvu au kutengeneza mashtaka ya uongo ili watu wawape pesa. Mtosheke na mishahara mnayopata.”
15 Kila mtu alitarajia kuja kwa Masihi,[n] na walijiuliza wakisema, “Labda Yohana ndiye Masihi.”
16 Yohana aliwajibu watu wote, akasema, “Ninawabatiza ninyi katika maji, lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Yuko tayari sasa kuja kusafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri na makapi, na kuiweka katika ghala yake kisha ataichoma ile isiyofaa katika moto usiozimika.” 18 Hivi ndivyo ambavyo Yohana aliwahubiri watu Habari Njema. Aliwaonya sana kuwa wanatakiwa kubadili njia zao.
Kazi ya Yohana Ilivyomalizika Baadaye
19 Yohana alimkosoa Herode kwa sababu ya mambo mabaya aliyokuwa ameyafanya na Herodia, mkewe kaka yake Herode, na pia kwa mambo mengine mabaya aliyokuwa ameyafanya. 20 Hivyo Herode aliongeza jambo jingine baya katika matendo yake maovu. Alimfunga Yohana gerezani.
Yohana Ambatiza Yesu
(Mt 3:13-17; Mk 1:9-11)
21 Watu wote walipokuwa wakibatizwa, Yesu alikuja naye akabatizwa. Na alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka, 22 na Roho Mtakatifu aliyekuwa katika umbo la njiwa akashuka juu yake. Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.”
Ukoo wa Yesu
(Mt 1:1-17)
23 Yesu alipoanza kufundisha, alikuwa na umri kama wa miaka thelathini. Watu walidhani kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Yusufu.
Yusufu alikuwa mwana wa Eli.
24 Eli alikuwa mwana wa Mathati.
Mathati alikuwa mwana wa Lawi.
Lawi alikuwa mwana wa Melki.
Melki alikuwa mwana wa Yana.
Yana alikuwa mwana wa Yusufu.
25 Yusufu alikuwa mwana wa Matathia.
Matathia alikuwa mwana wa Amosi.
Amosi alikuwa mwana wa Nahumu.
Nahumu alikuwa mwana wa Esli.
Esli alikuwa mwana wa Nagai.
26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi.
Maathi alikuwa mwana wa Matathia.
Matathia alikuwa mwana wa Semei.
Semei alikuwa mwana wa Yusufu.
Yusufu alikuwa mwana wa Yoda.
27 Yoda alikuwa mwana wa Yoana.
Yoana alikuwa mwana wa Resa.
Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli.
Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli.
Shealtieli alikuwa mwana wa Neri.
28 Neri alikuwa mwana wa Melki.
Melki alikuwa mwana wa Adi.
Adi alikuwa mwana wa Kosamu.
Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu,
Elmadamu alikuwa mwana wa Eri.
29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua.
Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri.
Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu.
Yorimu alikuwa mwana wa Mathati.
Mathati alikuwa mwana wa Lawi.
30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni.
Simeoni alikuwa mwana wa Yuda.
Yuda alikuwa mwana wa Yusufu.
Yusufu alikuwa mwana wa Yonamu.
Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu.
31 Eliakimu alikuwa mwana wa Melea.
Melea alikuwa mwana wa Mena.
Mena alikuwa mwana wa Matatha.
Matatha alikuwa mwana wa Nathani.
Nathani alikuwa mwana wa Daudi.
32 Daudi alikuwa mwana wa Yese.
Yese alikuwa mwana wa Obedi.
Obedi alikuwa mwana wa Boazi.
Boazi alikuwa mwana wa Salmoni.[o]
Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni.
33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu.
Aminadabu alikuwa mwana wa Admini,
Admini alikuwa mwana wa Aramu.[p]
Aramu alikuwa mwana wa Hesroni.
Hesroni alikuwa mwana wa Peresi.
Peresi alikuwa mwana wa Yuda.
34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo.
Yakobo alikuwa mwana wa Isaka.
Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu.
Ibrahimu alikuwa mwana wa Tera.
Tera alikuwa mwana wa Nahori.
35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi,
Serugi alikuwa mwana wa Ragau.
Ragau alikuwa mwana wa Pelegi.
Pelegi alikuwa mwana wa Eberi,
Eberi alikuwa mwana wa Sala.
36 Sala alikuwa mwana wa Kenani.
Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi.
Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu.
Shemu alikuwa mwana wa Nuhu.
Nuhu alikuwa mwana wa Lameki.
37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela.
Methusela alikuwa mwana wa Henoko.
Henoko alikuwa mwana wa Yaredi.
Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli.
Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani.
38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi.
Enoshi alikuwa mwana wa Sethi.
Sethi alikuwa mwana wa Adamu.
Adamu alikuwa mwana wa Mungu.
Yesu Ajaribiwa na Shetani
(Mt 4:1-11; Mk 1:12-13)
4 Akiwa amejaa Roho Mtakatifu, Yesu akarudi kutoka Mto Yordani. Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza mpaka nyikani 2 kwa muda wa siku arobaini, alikojaribiwa na Ibilisi. Katika muda wote huo hakula chakula chochote na baadaye akahisi njaa sana.
3 Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.”
4 Yesu akamjibu, “Maandiko yanasema, ‘Watu hawataishi kwa mkate tu.’”(B)
5 Kisha mwovu akamchukua Yesu na kwa muda mfupi akamwonyesha falme zote za ulimwengu. 6 Mwovu akamwambia, “Nitakufanya uwe mfalme wa sehemu zote hizi. Utakuwa na mamlaka juu yao, na utapata utukufu wote. Yote yametolewa kwangu. Ninaweza kumpa yeyote kadri ninavyopenda. 7 Nitakupa vyote hivi, ikiwa utaniabudu tu.”
8 Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Ni lazima umwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’”(C)
9 Ndipo Shetani akamwongoza Yesu mpaka Yerusalemu na kumweka mahali palipo juu katika mnara wa Hekalu. Akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe! 10 Kwani Maandiko yanasema,
‘Mungu atawaamuru
malaika zake wakulinde.’(D)
11 Pia imeandikwa kuwa,
‘Mikono yao itakudaka,
ili usijikwae mguu wako kwenye mwamba.’”(E)
12 Yesu akajibu, “Pia, Maandiko yanasema: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(F)
13 Shetani alipomaliza kumjaribu Yesu katika namna zote, alimwacha akaenda zake hadi wakati mwingine.
Yesu Aanza Kazi yake Galilaya
(Mt 4:12-17; Mk 1:14-15)
14 Yesu alirudi Galilaya akiwa na nguvu za Roho Mtakatifu. Habari zake zilisambaa katika eneo lote lililozunguka Galilaya. 15 Alianza kufundisha katika masinagogi na kila mtu alimsifu.
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Mk 6:1-6)
16 Yesu alisafiri akaenda katika mji aliokulia wa Nazareti. Siku ya Sabato alikwenda kwenye sinagogi kama alivyokuwa akifanya. Alisimama ili asome. 17 Akapewa gombo la nabii Isaya. Akalivingirisha kulifungua na akapata mahali palipoandikwa haya:
18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
amenichagua ili
niwahubiri maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao
na kuwaambia wasiyeona
kuwa wanaweza kuona tena.
Amenituma kuwapa uhuru wale wanaoteswa
19 na kutangaza kuwa wakati wa Bwana
kuonesha wema wake umefika.”(G)
20 Yesu akalivingirisha gombo akalifunga, akalirudisha kwa msaidizi na kuketi chini. Kwa kuwa kila mtu ndani ya sinagogi alimwangalia kwa makini, 21 Alianza kuzungumza nao. Akasema, “Maandiko haya yametimilika mlipokuwa mnanisikia nikiyasoma!”
22 Kila mtu pale akasema alipenda namna ambavyo Yesu alizungumza. Walishangaa kumsikia akisema maneno haya ya ajabu. Wakaulizana, “Inawezekanaje? Huyu si mwana wa Yusufu?”
23 Yesu akawaambia, “Ninafahamu mtaniambia mithali hii ya zamani: ‘Daktari, jitibu mwenyewe.’ Mnataka kusema ‘Tulisikia mambo yote uliyotenda Kapernaumu. Yatende pia hapa katika mji wako mwenyewe!’” 24 Lakini Yesu akasema, “Ukweli ni huu, nabii hakubaliki katika mji wa kwao.
25-26 Wakati wa Eliya mvua haikunyesha katika Israeli kwa miaka mitatu na nusu. Chakula hakikuwepo mahali popote katika nchi yote. Palikuwa wajane wengi katika Israeli wakati huo. Lakini Eliya hakutumwa kwenda kwa mmoja wa wajane waliokuwa katika Israeli bali kwa mjane aliyekuwa katika mji wa Sarepta, jirani na Sidoni.
27 Na, palikuwa wenye ugonjwa mbaya wa ngozi wengi walioishi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakuna aliyeponywa isipokuwa Naamani, aliyetoka katika nchi ya Shamu, siyo Israeli.”
28 Watu wote waliposikia hili, walikasirika sana. 29 Wakasimama na kumlazimisha Yesu atoke nje ya mji. Mji wao ulijengwa juu ya kilima. Wakamchukua Yesu mpaka ukingo wa kilima ili wamtupe. 30 Lakini alipita katikati yao na kwenda zake.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu
(Mk 1:21-28)
31 Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji uliokuwa Galilaya. Siku ya Sabato aliwafundisha watu. 32 Nao walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha kwa sababu mafundisho yake yalikuwa na mamlaka.
33 Ndani ya sinagogi alikuwepo mtu aliyekuwa na roho chafu, kutoka kwa yule Mwovu, ndani yake. Akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, “Aiii! 34 Unataka nini kwetu Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani; Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” 35 Lakini Yesu akamkemea yule pepo na kumwambia, “Nyamaza kimya! Umtoke mtu huyu!” Ndipo pepo akamtupa yule mtu chini mbele ya watu, akamtoka bila kumjeruhi sehemu yoyote ya mwili wake.
36 Watu wakashangaa. Wakasemezana wao kwa wao, “Hii inamaanisha nini? Kwa mamlaka na uwezo anaamuru pepo wachafu na wanatoka!” 37 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea kila mahali katika eneo lote.
Yesu Amponya Mkwewe Petro
(Mt 8:14-17; Mk 1:29-34)
38 Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni.[q] Mama mkwe wa Simoni alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa kali. Nao walimwomba Yesu amsaidie. 39 Yesu alisimama karibu yake na kuiamuru homa kuondoka. Homa ikamwacha, naye akasimama na kuanza kuwahudumia.
Yesu Aponya Wengine Wengi
40 Jua lilipokuchwa, watu wote waliwaleta kwa Yesu jamaa na rafiki zao walioumwa na wenye magonjwa mengi tofauti. Yesu aliweka mikono yake juu ya kila mgonjwa na kuwaponya wote. 41 Pepo nao waliwatoka watu wengi. Mapepo yalipiga kelele yakisema “Wewe ni Mwana wa Mungu.” Lakini Yesu alitoa amri yenye nguvu kwa mapepo yasiseme, kwa sababu yalijua alikuwa ni Masihi.
Yesu Aenda Katika Miji Mingine
(Mk 1:35-39)
42 Siku iliyofuata Yesu alijitenga na kwenda mahali ili awe peke yake. Watu wakawa wakimtafuta. Walipompata, walijaribu kumzuia asiondoke. 43 Lakini akawaambia, “Ni lazima nihubiri Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa sababu nilitumwa kufanya hivyo.”
44 Kisha Yesu akahubiri Habari Njema katika masinagogi ya Uyahudi.
Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi
(Mt 4:18-22; Mk 1:16-20)
5 Yesu aliposimama ukingoni mwa Ziwa Galilaya[r] kundi la watu lilimsogelea ili wasikie mafundisho kuhusu Mungu. 2 Yesu aliona mashua mbili zikiwa kando ya ziwa. Wavuvi walikuwa wametoka katika mashua zao na walikuwa wanaosha nyavu zao. 3 Yesu aliingia kwenye mashua ya Simoni. Akamwomba Simoni aisogeze mbali kidogo na ufukwe wa ziwa. Kisha akaketi ndani ya mashua na akawafundisha watu waliokuwa ufukweni mwa ziwa.
4 Yesu alipomaliza kufundisha, alimwambia Simoni, “Ipeleke mashua mpaka kwenye kilindi cha maji kisha mshushe nyavu zenu majini na mtapata samaki.”
5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi usiku kucha kuvua samaki na hatukupata chochote. Lakini kwa kuwa unasema nishushe nyavu majini, nitafanya hivyo.” 6 Walipofanya hivi, nyavu zao zilijaa samaki wengi mpaka zikaanza kuchanika. 7 Waliwaita rafiki zao waliokuwa katika mashua nyingine ili waje wawasaidie. Rafiki zao walikuja kuwasaidia, na mashua zote mbili zilijaa samaki kiasi cha kutaka kuzama.
8-9 Wavuvi wote walistaajabu kwa sababu ya wingi wa samaki waliovua. Simoni Petro alipoona hili, akapiga magoti mbele ya Yesu na akasema, “Nenda mbali nami Bwana, mimi ni mwenye dhambi!” 10 Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, walishangaa pia. (Yakobo na Yohana walikuwa wanavua pamoja na Simoni.)
Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope. Kuanzia sasa kazi yako haitakuwa kuvua samaki bali kukusanya watu!”
11 Wakaziendesha mashua zao mpaka pwani, kisha wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Mk 1:40-45)
12 Wakati mmoja Yesu alikuwa katika mji ambao mwanaume mmoja mgonjwa alikuwa anaishi. Mwanaume huyo alikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi mwili wake wote. Alipomwona Yesu, alimsujudia na kumsihi akisema, “Bwana, ikiwa unataka una uwezo wa kuniponya.”
13 Yesu akasema, “Hakika ninataka kukuponya, upone!” Kisha akamgusa, na ugonjwa ukatoweka papo hapo. 14 Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.[s] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”
15 Lakini habari kuhusu Yesu zilizidi kuenea zaidi. Watu wengi walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 Mara nyingi Yesu alikwenda sehemu zingine zisizokuwa na watu na akaomba huko.
Yesu Amponya Aliyepooza
(Mt 9:1-8; Mk 2:1-12)
17 Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wameketi hapo pia. Walitoka katika kila mji wa Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu. BWANA alimpa Yesu uwezo wa kuponya watu. 18 Alikuwepo mtu aliyepooza na baadhi ya watu walikuwa wamembeba kwenye machela. Walijaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. 19 Lakini walishindwa kufika alipokuwa Yesu kwa sababu kulikuwa na watu wengi sana. Hivyo walikwenda juu ya paa ya nyumba na kumshusha aliyepooza chini kupitia tundu kwenye dari. Waliishusha machela alimokuwa aliyepooza kwa usawa kiasi kwamba akawa amelala mbele ya Yesu. 20 Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, akamwambia yule mgonjwa: “Rafiki yangu, dhambi zako zimesamehewa!”
21 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wao kwa wao wakisema: “Huyu mtu ni nani kiasi cha kuthubutu kusema hivi? Si anamtukana Mungu! Mungu peke yake ndiye anayesamehe dhambi.”
22 Lakini Yesu alijua walichokuwa wanawaza, akawaambia: “Kwa nini mna maswali haya mioyoni mwenu? 23-24 Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia, mtu huyu, beba machela yako na utembee? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, Inuka! Beba machela yako uende nyumbani!”
25 Yule mtu akasimama saa ile ile mbele ya kila mtu. Akaubeba machela yake na kwenda nyumbani kwake, akimsifu Mungu. 26 Kila mtu alishangaa na kuanza kumsifu Mungu. Wakajawa na hofu kuu baada ya kuiona nguvu ya Mungu. Wakasema, “Leo tumeona mambo ya kushangaza!”
Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu
(Mt 9:9-13; Mk 2:13-17)
27 Baada ya hayo Yesu alitoka nje akamwona mtoza ushuru amekaa sehemu yake ya kukusanyia ushuru. Jina lake aliitwa Lawi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” 28 Lawi akasimama, akaacha kila kitu na kumfuata Yesu.
29 Lawi akaandaa chakula cha usiku nyumbani kwake kwa kumheshimu Yesu. Mezani walikuwepo watoza ushuru wengi na baadhi ya watu wengine. 30 Lakini Mafarisayo na wale wanaofundisha sheria kwa ajili ya Mafarisayo wakaanza kulalamika kwa wafuasi wa Yesu wakisema, “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”
31 Yesu akawajibu, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari, si wenye afya njema. 32 Sikuja kuwaambia wenye haki wabadilike, bali wenye dhambi.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mt 9:14-17; Mk 2:18-22)
33 Baadhi ya watu wakamwambia Yesu, “Wafuasi wa Yohana hufunga na kuomba mara kwa mara, vivyo hivyo wafuasi wa Mafarisayo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa kila wakati.”
34 Yesu akawaambia, “Kwenye harusi huwezi kuwaambia marafiki wa bwana harusi wafunge wakati bwana harusi bado yuko pamoja nao. 35 Lakini muda ukifika na bwana harusi akaondolewa kwao. Watakuwa na huzuni, na watafunga.”
36 Yesu akawaambia mfano huu: “Hakuna anayekata kiraka kwenye vazi jipya na kukishona kwenye vazi la zamani. Ataharibu vazi jipya, na kiraka kutoka vazi jipya hakitakuwa sawa na vazi la zamani. 37 Pia hakuna mtu anayeweka divai mpya[t] katika viriba vya zamani. Divai mpya itavipasua, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. 38 Daima mnaweka divai mpya kwenye viriba vipya. 39 Hakuna mtu ambaye baada ya kunywa divai ya zamani hutaka divai mpya. Kwa sababu husema, ‘Divai ya zamani ni nzuri.’”
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mt 12:1-8; Mk 2:23-28)
6 Wakati fulani siku ya Sabato, Yesu alikuwa akitembea kupitia katika baadhi ya mashamba ya nafaka. Wafuasi wake wakachukua masuke, wakayapukusa mikononi mwao na kula nafaka. 2 Baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, “Kwa nini mnafanya hivyo? Ni kinyume na Sheria ya Musa kufanya hivyo siku ya Sabato.”
3 Yesu akawajibu, “Je, mmesoma kuhusu jambo alilofanya Daudi, wakati yeye na watu wake walipohisi njaa? 4 Daudi alikwenda katika nyumba ya Mungu, akachukua mikate iliyotolewa kwa Mungu na kuila. Na kuwapa wenzake baadhi ya mikate hiyo. Hii ilikuwa kinyume na Sheria ya Musa, inayosema kuwa makuhani pekee ndiyo wanaoruhusiwa kula mikate hiyo.” 5 Kisha Yesu akawaambia Mafarisayo, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Mk 3:1-6)
6 Siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na kuwafundisha watu. Katika sinagogi hili alikuwemo mtu aliyepooza mkono wake wa kulia. 7 Walimu wa sheria na Mafarisayo walikuwa wakimvizia Yesu. Walikuwa wanasubiri waone ikiwa ataponya siku hiyo ya Sabato. Walitaka kumwona akifanya jambo lolote lililo kinyume ili wamshitaki. 8 Lakini Yesu alijua walilokuwa wanawaza. Akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyenyuka na simama hapa ambapo kila mtu anaweza kukuona!” Yule mtu akanyenyuka na kusimama pale. 9 Ndipo Yesu akawaambia, “Ninawauliza ninyi, Sheria inaturuhusu tufanye nini siku ya Sabato: kutenda mema au kutenda mabaya? Je, ni halali kuokoa uhai au kuuangamiza?”
10 Yesu akawatazama watu wote kila upande, kisha akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyosha mkono wake, na akaponywa. 11 Mafarisayo na walimu wa sheria wakakasirika sana kiasi cha kutofikiri sawasawa, wakashauriana wao kwa wao wamfanye nini Yesu.
Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili
(Mt 10:1-4; Mk 3:13-19)
12 Siku chache baadaye, Yesu alikwenda mlimani kuomba. Alikaa huko usiku kucha akimwomba Mungu. 13 Asubuhi iliyofuata aliwaita wafuasi wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao na kuwaita Mitume. Nao ni:
14 Simoni (ambaye Yesu alimwita Petro),
Andrea aliyekuwa kaka yake Petro,
Yakobo,
Yohana,
Filipo,
Bartholomayo,
15 Mathayo na
Tomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Simoni aliyeitwa Mzelote,
16 Yuda mwana wa Yakobo,
na Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).
Yesu Afundisha na Kuponya Watu
(Mt 4:23-25; 5:1-12)
17 Yesu na mitume wakatelemka kutoka mlimani. Yesu akasimama mahali tambarare. Kundi kubwa la wafuasi wake lilikuwa pale. Walikuwepo pia watu wengi waliotoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu, na maeneo ya pwani karibu na Tiro na Sidoni. 18 Wote walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya watu waliokuwa wanasumbuliwa na mapepo. 19 Kila mtu alijaribu kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa unamtoka. Yesu aliwaponya wote.
20 Yesu akawatazama wafuasi wake na kusema,
“Heri ninyi mlio maskini.
Maana Ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Heri ninyi mlio na njaa sasa.
Maana mtashibishwa.
Heri ninyi mnaolia sasa.
Maana mtafurahi na kucheka.
22 Watu watawachukia kwa sababu ninyi ni wa milki ya Mwana wa Adamu. Watawabagua na watawatukana. Watajisikia vibaya hata kutamka majina yenu. Mambo haya yatakapotukia, mjue kuwa baraka kuu ni zenu. 23 Ndipo mfurahi na kurukaruka kwa furaha, kwa sababu mna thawabu kuu mbinguni. Baba zao waliwafanyia manabii vivyo hivyo.
24 Lakini ole wenu ninyi matajiri,
kwa kuwa mmekwishapata maisha yenye raha.
25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,
kwa kuwa mtasikia njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
kwa kuwa mtalia na kuhuzunika.
26 Ole wenu watu wote wanapowasifu ninyi. Maana mababu zao waliwasifu manabii wa uongo vivyo hivyo daima.
Wapende Adui Zako
(Mt 5:38-48; 7:12a)
27 Lakini ninawaambia ninyi mnaonisikiliza, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wale wanaowachukia. 28 Mwombeni Mungu awabariki wale wanaowalaani ninyi, waombeeni wale wanaowaonea. 29 Mtu akikupiga shavu moja, mwache akupige na la pili pia. Mtu akichukua koti lako, usimkataze kuchukua shati pia. 30 Mpe kila akuombaye kitu. Mtu yeyote akichukua kitu chako, usitake akurudishie. 31 Watendeeni wengine kama mnavyotaka wao wawatendee ninyi.
32 Je, msifiwe kwa sababu ya kuwapenda wale wanaowapenda ninyi tu? Hapana, hata wenye dhambi, wanawapenda wale wanaowapenda. 33 Je, msifiwe kwa kuwa mnawatendea mema wale wanaowatendea mema ninyi? Hapana, hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo! 34 Je, msifiwe kwa kuwa mnawakopesha watu kwa kutarajia kupata vitu kutoka kwao? Hapana, hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wengine, ili warudishiwe kiasi kile kile!
35 Ninawaambia kuwa wapendeni adui zenu na kuwatendea mema. Wakopesheni watu bila kutarajia kitu kutoka kwao. Mkifanya hivyo, mtapata thawabu kuu. Mtakuwa wana wa Mungu Mkuu Aliye Juu. Ndiyo kwa sababu Mungu ni mwema hata kwa wenye dhambi na wasiomshukuru. 36 Iweni na upendo na huruma, kama Baba yenu alivyo.
Iweni Waangalifu Mnapokosoa Wengine
(Mt 7:1-5)
37 Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa na Mungu. Msiwalaani wengine nanyi hamtalaaniwa. Wasameheni wengine nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni wengine vitu, nanyi mtapokea. Mtapewa vingi; kipimo chenye ujazo wa kusukwasukwa na kumwagika. Mungu atawapa ninyi kwa kadri mnavyotoa.”
39 Yesu akawaambia mfano huu, “Je, asiyeona anaweza kumwongoza asiyeona mwenzake? Hapana. Wote wawili watatumbukia shimoni. 40 Wanafunzi si bora kuliko mwalimu wao. Lakini wakiisha kufundishwa na kuhitimu, wanakuwa kama mwalimu wao.
41 Kwa nini unaona kipande kidogo cha vumbi kilicho katika jicho la rafiki yako, lakini hujali kipande cha ubao kilicho ndani ya jicho lako mwenyewe? 42 Unawezaje kumwambia rafiki yako, ‘Hebu nikitoe kipande cha vumbi kilicho katika jicho lako’? Je, huwezi kukiona kipande cha ubao kilicho katika jicho lako mwenyewe? Wewe ni mnafiki. Kwanza kitoe kipande cha ubao katika jicho lako, ndipo utaona vyema na utaweza kukitoa kipande cha vumbi kilicho katika jicho la rafiki yako.
Yale Unayofanya Yanaonesha Jinsi Ulivyo
(Mt 7:17-20; 12:34b-35)
43 Mti mzuri hauzai matunda mabaya. Na mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44 Kila mti unatambuliwa kutokana na aina ya matunda unayozaa. Huwezi kupata tini kwenye vichaka vya miiba. Na huwezi kuchuma zabibu kwenye michongoma! 45 Watu wema wana mambo mazuri katika mioyo yao. Ndiyo sababu hutamka mambo mema. Lakini waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu hutamka mambo maovu. Mambo wanayotamka watu katika midomo yao, ndiyo yaliyojaa katika mioyo yao.
Aina Mbili za Watu
(Mt 7:24-27)
46 Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana’ lakini hamtendi kama ninavyosema? 47 Nitawaonesha namna walivyo watu wanaokuja kwangu, wale wanaoyasikia na kuyatii mafundisho yangu. 48 Ni kama mtu anayejenga nyumba, huchimba chini sana, na kujenga nyumba yake kwenye mwamba. Mafuriko yanapokuja, huigonga nyumba kwa nguvu, nyumba hiyo haiwezi kuanguka kwa kuwa imejengwa vizuri.
49 Lakini watu wanaoyasikia maneno yangu na hawayatii ni kama mtu anayejenga nyumba bila kutayarisha msingi. Mafuriko yanapokuja, nyumba huanguka chini kwa urahisi na kubomoka kabisa.”
Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi
(Mt 8:5-13; Yh 4:43-54)
7 Yesu alipomaliza kuwaambia watu mambo yote aliyotaka kuwaambia, alikwenda mjini Kapernaumu. 2 Afisa wa jeshi katika mji wa Kapernaumu alikuwa na mtumishi aliyekuwa wa muhimu sana kwake. Mtumishi huyu alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa. 3 Afisa huyu aliposikia kuhusu Yesu, aliwatuma baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi kwa Yesu. Aliwataka wamwombe Yesu aende kumponya mtumishi wake. 4 Wazee walikwenda kwa Yesu, wakamsihi amsaidie afisa. Walisema, “Mtu huyu anastahili msaada wako, 5 Kwa sababu anawapenda watu wetu na ametujengea sinagogi.”
6 Hivyo Yesu alikwenda nao. Alipoikaribia nyumba ya yule afisa, afisa aliwatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, huhitaji kufanya kitu chochote maalumu kwa ajili yangu. Sistahili wewe uingie nyumbani mwangu. 7 Ndiyo maana sikuja mimi mwenyewe kwako. Unahitaji kutoa amri tu na mtumishi wangu atapona. 8 Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”
9 Yesu aliposikia hayo alishangaa, akawageukia watu waliokuwa wanamfuata, akawaambia, “Ninawaambia, Sijawahi kuona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”
10 Kundi lililotumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani, walimkuta yule mtumishi amepona.
Yesu Amfufua Kijana wa Mama Mjane
11 Siku iliyofuata Yesu na wafuasi wake walikwenda katika mji wa Naini. Kundi kubwa la watu walisafiri pamoja nao. 12 Yesu alipolikaribia lango la mji, aliona watu wamebeba maiti. Alikuwa ni mwana pekee wa mama mjane. Watu wengi kutoka mjini walifuatana na yule mama mjane. 13 Bwana alipomwona yule mama, alimwonea huruma na kumwambia, “Usilie.” 14 Akakaribia, akaligusa jeneza. Wanaume waliokuwa wamebeba jeneza wakasimama. Ndipo Yesu akamwambia kijana aliyekufa, “Kijana, nakuambia, inuka!” 15 Yule kijana, akaketi, akaanza kuongea. Yesu akamrudisha kwa mama yake.
16 Kila mtu aliingiwa hofu. Wakaanza kumsifu Mungu na kusema, “Nabii mkuu yuko hapa pamoja nasi!” na “Mungu amekuja kuwasaidia watu wake!”
17 Habari hii kuhusu Yesu ikaenea katika Uyahudi yote, na kila sehemu kuzunguka pale.
Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali
(Mt 11:2-19)
18 Wafuasi wa Yohana Mbatizaji walimweleza Yohana Mbatizaji kuhusu mambo haya yote. Naye aliwaita wanafunzi wake wawili. 19 Akawatuma waende na kumwuliza Yesu, “Wewe ndiye tuliyesikia anakuja, au tumsubiri mwingine?”
20 Wafuasi wa Yohana walipofika kwa Yesu, wakasema, “Yohana Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule ajaye, au tumsubiri mwingine?’”
21 Wakati ule ule Yesu alikuwa amewaponya watu wengi madhaifu na magonjwa yao. Aliwaponya waliokuwa na pepo wabaya na kuwafanya wasiyeona wengi kuona. 22 Kisha aliwaambia wanafunzi wa Yohana, “Nendeni mkamweleze Yohana yale mliyoyaona na kuyasikia: wasiyeona wanaona, walemavu wa miguu wanatembea, wenye magonjwa mabaya ya ngozi wanatakasika, wasiyesikia wanasikia. Waliokufa wanafufuliwa na Habari Njema inahubiriwa kwa maskini. 23 Heri wale wasio na mashaka kunikubali mimi.”[u]
24 Baada ya wanafunzi wa Yohana kuondoka, Yesu akaanza kuwaambia watu kuhusu Yohana, “Mlitoka kwenda jangwani kuona nini? Mtu aliyekuwa dhaifu, kama unyasi unaotikiswa na upepo? 25 Mlitegemea kuona nini? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hilo. Watu wanaovaa mavazi mazuri na kuishi kwa anasa wako katika majumba ya wafalme. 26 Sasa, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yohana ni zaidi ya nabii. 27 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(H)
28 Ninawaambia, hakuna aliyewahi kuzaliwa aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini mwenye umuhimu mdogo, katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”
29 (Watu waliposikia hili, wote walikubali kuwa mafundisho ya Mungu yalikuwa mazuri. Hata watoza ushuru waliobatizwa na Yohana walikiri. 30 Lakini Mafarisayo na wanasheria walikataa kuukubali mpango wa Mungu kwa ajili yao; hawakumruhusu Yohana awabatize.)
31 “Niseme nini kuhusu watu wa wakati huu? Niwafananishe na nini? Wanafanana na nini? 32 Ni kama watoto waliokaa sokoni. Kundi moja la watoto likawaita watoto wengine na kusema,
‘Tuliwapigia filimbi
lakini hamkucheza.
Tuliwaimba wimbo wa huzuni,
lakini hamkulia.’
33 Yohana Mbatizaji alikuja na hakula chakula cha kawaida au kunywa divai. Nanyi mkasema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 34 Mwana wa Adamu amekuja anakula na kunywa. Mnasema, ‘Mwangalieni anakula sana na kunywa sana divai. Ni rafiki wa watoza ushuru na watenda dhambi wengine.’ 35 Lakini hekima huoneshwa kuwa sahihi kwa wale wanaoikubali.”
Yesu na Mwanamke Mwenye Dhambi
36 Mmoja wa Mafarisayo alimwalika Yesu kula chakula nyumbani mwake. Yesu akaenda nyumbani kwa yule Farisayo, akaketi[v] katika nafasi yake sehemu ya kulia chakula.
37 Alikuwepo mwanamke mmoja katika mjini ule aliyekuwa na dhambi nyingi. Alipojua kuwa Yesu alikuwa anakula chakula nyumbani kwa Farisayo, alichukua chupa kubwa yenye manukato ya thamani sana. 38 Alisimama karibu na miguu ya Yesu akilia. Kisha alianza kuisafisha miguu ya Yesu kwa machozi yake na akaifuta kwa nywele zake, akaibusu mara nyingi na kuipaka manukato.
39 Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona hili, alijisemea moyoni mwake, “Mtu huyu angekuwa nabii, angetambua kuwa mwanamke huyu anayemgusa ni mwenye dhambi.”
40 Katika kujibu kile Farisayo alichokuwa akifikiri, Yesu akasema, “Simoni nina kitu cha kukwambia.”
Simoni akajibu, “Nieleze, Mwalimu.”
41 Yesu akasema, “Kulikuwa watu wawili. Wote wawili walikuwa wanadaiwa na mkopeshaji mmoja. Mmoja alidaiwa sarafu mia tano za fedha, na wa pili sarafu hamsini za fedha. 42 Watu wale hawakuwa na fedha, hivyo hawakuweza kulipa madeni yao. Lakini mkopeshaji aliwasamehe wote wawili. Kati ya wote wawili ni yupi atakayempenda mkopeshaji zaidi?”
43 Simoni akajibu, “Nafikiri ni yule aliyekuwa anadaiwa fedha nyingi.”
Yesu akamwambia, “Umejibu sawa.” 44 Kisha akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako hukunipa maji ili ninawe miguu yangu. Lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kuikausha kwa nywele zake. 45 Wewe hukunisalimu kwa busu, lakini amekuwa akinibusu miguu yangu tangu nilipoingia. 46 Hukuniheshimu kwa mafuta kwa ajili ya kichwa changu, lakini yeye amenipaka miguu yangu manukato yanayonukia vizuri. 47 Ninakwambia kuwa dhambi zake zilizo nyingi zimesamehewa. Hii ni wazi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa. Watu wanaosamehewa kidogo hupenda kidogo.”
48 Kisha akamwambia mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”
49 Watu waliokaa naye sehemu ya chakula wakaanza kusema mioyoni mwao, “Mtu huyu anadhani yeye ni nani? Anawezaje kusamehe dhambi?”
50 Yesu akamwambia mwanamke, “Kwa sababu uliamini, umeokolewa kutoka katika dhambi zako. Nenda kwa amani.”
Yesu Akiwa Galilaya
8 Siku iliyofuata, Yesu alisafiri kupitia katika baadhi ya miji na vijiji. Yesu aliwahubiri watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Mitume kumi na wawili walikuwa pamoja naye. 2 Walikuwepo pia baadhi ya wanawake ambao Yesu aliwaponya magonjwa na pepo wabaya. Mmoja wao alikuwa Mariamu aitwaye Magdalena ambaye alitokwa na pepo saba; 3 Pia pamoja na wanawake hawa alikuwepo Yoana mke wa Kuza (msimamizi wa mali za Herode), Susana, na wanawake wengine wengi. Wanawake hawa walitumia fedha zao kuwahudumia Yesu na mitume wake.
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mt 13:1-17; Mk 4:1-12)
4 Kundi kubwa la watu lilikusanyika. Watu walimjia Yesu kutoka katika kila mji, naye Yesu akawaambia fumbo hili:
5 “Mkulima alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akizitawanya, baadhi zilianguka kandokando ya njia. Watu wakazikanyaga, na ndege wa angani wakazila. 6 Zingine zikaanguka kwenye udongo wenye mawe. Zilipoanza kukua zikafa kwa sababu ya kukosa maji. 7 Mbegu zingine ziliangukia kwenye miiba. Miiba ikakua pamoja nazo, miiba ikazisongasonga na hazikukua. 8 Zilizosalia ziliangukia kwenye udongo mzuri wenye rutuba. Mbegu hizi zikaota na kuzaa kila moja mia.”
Yesu akamalizia fumbo. Kisha akapaza sauti, akasema, “Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!”
9 Wafuasi wake wakamwuliza, “Fumbo hili linamaanisha nini?”
10 Akasema, “Mmechaguliwa kujua kweli za siri kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini ninatumia mafumbo kuzungungumza na watu wengine. Ninafanya hivi ili,
‘Watazame,
lakini wasiweze kuona.
Wasikia,
lakini wasielewe.’(I)
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mt 13:18-23; Mk 4:13-20)
11 Hii ndiyo maana ya fumbo hili: Mbegu ni Neno la Mungu. 12 Watu wengine ni kama mbegu zilizoanguka njiani. Husikia mafundisho ya Mungu, lakini Shetani huja na kuwafanya waache kuyatafakari. Hii huwafanya kutoamini na kuokoka. 13 Wengine wanafanana na mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye mawe. Ni watu ambao huyasikia mafundisho ya Mungu na kuyapokea kwa furaha, lakini kwa kuwa hawana mizizi yenye kina, huamini kwa muda mfupi. Majaribu yanapokuja, humwacha Mungu.
14 Zilizoanguka katika miiba, zinafanana na watu wanaoyasikia Mafundisho ya Mungu, lakini wanaruhusu wasiwasi, mali na anasa za maisha haya kuwasimamisha na hawaendelei kukua. Hivyo mafundisho hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao.[w] 15 Na zile zilizoangukia katika udongo mzuri, ni wale ambao huyasikia mafundisho ya Mungu kwa moyo safi na mnyoofu. Huyatii na kwa uvumilivu wao huzaa mazao mazuri.
Zingatieni Nuru
(Mk 4:21-25)
16 Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa bakuli au kuificha uvunguni mwa kitanda. Badala yake huiweka kwenye kinara cha taa mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani wapate nuru ya kuwawezesha kuona. 17 Kila jambo lililofichwa litawekwa wazi na kila siri itajulikana na kila mtu ataiona. 18 Hivyo yatafakarini kwa umakini yale mnayosikia. Watu wenye uelewa kiasi watapokea zaidi. Lakini wale wasio na uelewa watapoteza hata ule wanaodhani kuwa wanao.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Mk 3:31-35)
19 Mama yake Yesu na wadogo zake wakaenda kumwona, lakini walishindwa kumfikia kwa sababu walikuwepo watu wengi sana. 20 Mtu mmoja akamwambia Yesu, “Mama yako na wadogo zako wamesimama nje. Wanataka kukuona.”
21 Yesu akawajibu “Mama yangu na wadogo zangu ni wale wanaolisikia na kulitii Neno la Mungu.”
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Mk 4:35-41)
22 Siku moja Yesu na wafuasi wake walipanda mashua. Akawaambia, “Tuvuke mpaka upande mwingine wa ziwa.” Wakaanza safari kuvuka ziwa. 23 Walipokuwa wanasafiri, Yesu alisinzia. Tufani kubwa ikalikumba ziwa na mashua ikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. 24 Wafuasi wakamwendea, wakamwamsha, wakasema, “Mkuu, mkuu, tutazama!”
Yesu akasimama, akaukemea upepo na mawimbi ya maji. Upepo ukakoma na ziwa likatulia. 25 Ndipo Yesu akawaambia wafuasi wake, “Imani yenu iko wapi?”
Lakini wao waliogopa na kustaajabu, wakanong'onezana, “Huyu ni mtu wa namna gani? Anaamuru upepo na maji, na vinamtii?”
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Mk 5:1-20)
26 Yesu na wafuasi wake wakasafiri mpaka katika nchi walimoishi Wagerasi[x] iliyokuwa ng'ambo ya ziwa Galilaya. 27 Yesu alipotoka katika mashua, mwanaume mmoja kutoka katika mji ule alimwendea. Mtu huyu alikuwa na mapepo ndani yake. Kwa muda mrefu hakuwahi kuvaa nguo na aliishi makaburini.
28-29 Pepo aliyekuwa ndani yake alikuwa akimpagaa mara nyingi na alikuwa akifungwa gerezani, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo. Lakini kila mara aliivunja. Pepo ndani yake alikuwa anamlazimisha kwenda nje ya mji mahali pasipoishi watu. Yesu alimwamuru kumtoka mtu yule. Alipomwona Yesu, alianguka mbele yake huku akipiga kelele kwa sauti, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu Aliye Juu? Tafadhali usiniadhibu!”
30 Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?”
Mtu yule akajibu, “Jeshi.”[y] (Alisema jina lake ni “Jeshi” kwa sababu pepo wengi walikuwa wamemwingia.) 31 Pepo wale wakamsihi Yesu asiwaamuru kwenda shimoni.[z] 32 Katika kilima kile, kulikuwa kundi kubwa la nguruwe wakichungwa. Pepo wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie wale nguruwe. Hivyo Yesu akawaruhusu. 33 Pepo wakamtoka yule mtu, na kuwaingia nguruwe. Kundi lote la wale nguruwe likakimbia kutelemkia ziwani kwa kasi, nguruwe wakazama na kufia humo.
34 Wachungaji wa nguruwe walipoona lililotokea, walikimbia, wakaenda kutoa taarifa mjini na mashambani. 35 Watu wakaenda kuona lililotokea. Walipofika alipokuwa Yesu wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, akiwa na akili zake timamu; pepo walikuwa wamemtoka. Jambo hili likawaogopesha watu. 36 Wale walioona mambo haya yalivyotokea waliwaambia wengine namna Yesu alivyomponya yule mtu. 37 Watu wote waliokuwa wakiishi eneo lote la Gerasi wakamtaka Yesu aondoke kwa sababu waliogopa.
Hivyo Yesu akapanda mashua na kurudi Galilaya. 38 Mtu aliyeponywa alimsihi amfuate Yesu. Lakini Yesu akamtuma, akamwambia, 39 “Rudi nyumbani, ukawaeleze watu mambo ambayo Mungu amekutendea.”
Hivyo mtu yule alikwenda sehemu zote za mji akieleza mambo ambayo Yesu amemtendea.
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mt 9:18-26; Mk 5:21-43)
40 Yesu aliporudi Galilaya, watu walimkaribisha. Kila mtu alikuwa anamsubiri. 41-42 Mtu mmoja jina lake Yairo, aliyekuwa mkuu wa sinagogi alimwendea. Alikuwa na binti mmoja tu mwenye umri wa miaka kumi na mbili na alikuwa mgonjwa sana katika hali ya kufa. Hivyo Yairo alisujudu miguuni pa Yesu na akamsihi aende nyumbani kwake.
Yesu alipokuwa akienda nyumbani kwa Yairo, watu walimzonga kila upande. 43 Mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili alikuwepo katika umati huo. Alikuwa ametumia mali zake zote kwa madaktari,[aa] lakini hakuna daktari aliyeweza kumponya. 44 Alikwenda nyuma ya Yesu na kugusa pembe ya vazi lake. Wakati huo huo damu ikaacha kumtoka. 45 Ndipo Yesu akasema, “Nani amenigusa?”
Kila mtu alikataa kuwa hajamgusa, Petro akasema, “Mkuu, watu wamekuzunguka na wanakuzongazonga kila upande.”
46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu amenigusa. Nimesikia nguvu ikinitoka.” 47 Yule mwanamke alipoona ya kwamba hataweza kujificha akajitokeza akitetemeka. Akasujudu mbele ya Yesu. Huku kila mmoja akisikia, akaeleza sababu iliyomfanya amguse, na kwamba alipona wakati ule ule alipomgusa. 48 Yesu alimwambia, “Binti yangu umeponywa kwa sababu uliamini. Nenda kwa amani.”
49 Yesu alipokuwa bado anaongea, mtu mmoja kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi alikuja na akasema, “Binti yako amekwisha kufa! Hakuna haja ya kuendelea kumsumbua Mwalimu.”
50 Yesu aliposikia maneno hayo, alimwambia Yairo, “Usiogope! Amini tu na binti yako ataponywa.”
51 Yesu akaenda nyumbani, alipofika akaruhusu Petro, Yohana, Yakobo pamoja na baba na mama wa yule mtoto tu kuingia ndani pamoja naye. 52 Kila mtu alikuwa akilia na kusikia huzuni kwa sababu msichana alikuwa amekufa. Lakini Yesu akasema, “Msilie. Hajafa. Amelala usingizi tu.”
53 Watu wakamcheka, kwa sababu walijua kuwa amekwisha kufa. 54 Lakini Yesu akamshika mkono na kumwambia, “Mtoto inuka!” 55 Roho yake ikamrudia, akasimama hapo hapo. Yesu akasema, “Mpeni chakula.” 56 Wazazi wa yule binti wakashangaa. Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote lililotokea.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mt 10:5-15; Mk 6:7-13)
9 Yesu aliwaita mitume wake kumi na wawili pamoja, akawapa nguvu kuponya magonjwa na kutoa pepo kwa watu. 2 Akawatuma kwenda kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3 Akawaambia, “Mnaposafiri, msibebe kitu chochote: msichukue fimbo ya kutembelea, msibebe mkoba, chakula au fedha. Chukueni nguo mlizovaa tu kwa ajili ya safari yenu. 4 Mkiingia katika nyumba; kaeni katika nyumba hiyo mpaka mtakapokuwa mnatoka katika mji huo. 5 Ikiwa watu katika mji mtakaoingia hawatawakaribisha, nendeni nje ya mji na kuyakung'uta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.”
6 Hivyo mitume wakaondoka. Walisafiri katika miji yote. Walihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
Herode Achanganyikiwa Kuhusu Yesu
(Mt 14:1-12; Mk 6:14-29)
7 Herode, mtawala wa Galilaya alisikia mambo yote yaliyokuwa yanatokea. Alichanganyikiwa kwa sababu baadhi ya watu walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu.” 8 Wengine walisema, “Eliya amekuja kwetu,” na baadhi ya watu wengine walisema “Mmoja wa manabii wa kale amefufuka kutoka kwa wafu”. 9 Herode alisema, “Nilimkata kichwa Yohana. Sasa, mtu huyu ninayesikia habari zake ni nani?” Herode aliendelea kutaka kumwona Yesu.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Yh 6:1-14)
10 Mitume waliporudi, walimwambia Yesu waliyoyafanya katika safari yao. Ndipo akawachukua mpaka kwenye mji uitwao Bethsaida. Ili yeye Yesu na mitume wawe peke yao pamoja. 11 Lakini watu walipotambua mahali alikokwenda Yesu walimfuata. Aliwakaribisha na kuwaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Na aliwaponya waliokuwa wagonjwa.
12 Baadaye nyakati za jioni. Mitume kumi na mbili walimwendea na kumwambia, “Hakuna anayeishi mahali hapa. Waage watu. Wanahitaji kutafuta chakula na mahali pa kulala katika mashamba na miji iliyo karibu na eneo hili.”
13 Lakini Yesu akawaambia mitume, “Wapeni chakula.”
Wakasema, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Unataka twende tukanunue vyakula kwa ajili ya watu wote hawa? Ni wengi mno!” 14 (Walikuwepo wanaume kama 5,000 pale.)
Yesu akawaambia wafuasi wake, “Waambieni watu wakae katika vikundi vya watu hamsini hamsini.”
15 Hivyo wafuasi wake wakafanya hivyo na kila mtu akakaa chini. 16 Ndipo Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili. Akatazama juu mbinguni na kumshukuru Mungu kwa ajili ya chakula hicho. Kisha akaimega vipande vipande, akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. 17 Watu wote wakala mpaka wakashiba. Vikasalia vikapu kumi na mbili vilivyojaa vipande vya mikate na samaki ambavyo havikuliwa.
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mt 16:13-19; Mk 8:27-29)
18 Wakati mmoja Yesu alikuwa anaomba akiwa peke yake. Wafuasi wake walimwendea na aliwauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?”
19 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, lakini wengine wanasema wewe ni mmoja wa manabii wa zamani aliyefufuka.”
20 Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ni Masihi kutoka kwa Mungu.”
21 Yesu akawatahadharisha wasimwambie mtu yeyote.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mt 16:21-28; Mk 8:31-9:1)
22 Yesu akasema, “Ni lazima Mwana wa Adamu apate mateso mengi. Nitakataliwa na viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Na nitauawa. Lakini siku ya tatu nitafufuliwa kutoka kwa wafu.”
23 Kisha Yesu akamwambia kila mmoja aliyekuwa pale, “Mtu yeyote miongoni mwenu akitaka kuwa mfuasi wangu ni lazima ajikane yeye mwenyewe na mambo anayopenda. Ni lazima uubebe msalaba unaotolewa kwako kila siku kwa sababu ya kunifuata mimi. 24 Yeyote miongoni mwenu anayetaka kuyaponya maisha yake atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25 Haina thamani kwenu kuupata ulimwengu wote ikiwa ninyi wenyewe mtateketezwa au kupoteza kila kitu. 26 Msione aibu kwa sababu ya kunifuata na kusikiliza mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, Mimi, Mwana wa Adamu, nitawaonea aibu nitakapokuja nikiwa na utukufu wangu, utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu. 27 Niaminini ninaposema kwamba baadhi yenu ninyi mliosimama hapa mtauona Ufalme wa Mungu kabla hamjafa.”
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-8; Mk 9:2-8)
28 Baada ya siku kama nane tangu Yesu aseme maneno haya, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akapanda mlimani kuomba. 29 Yesu alipokuwa akiomba, uso wake ulianza kubadilika. Nguo zake zikawa nyeupe, zikang'aa. 30 Kisha watu wawili walikuwa pale, wakiongea naye. Walikuwa Musa na Eliya; 31 Wao pia walionekana waking'aa na wenye utukufu. Walikuwa wanazungumza na Yesu kuhusu kifo chake kitakachotokea Yerusalemu. 32 Petro na wenzake walikuwa wanasinzia. Lakini waliamka na kuuona utukufu wa Yesu. Waliwaona pia watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33 Musa na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akasema, “Mkuu, ni vizuri tuko hapa. Tutajenga vibanda vitatu hapa, kimoja kwa ajili ya kukutukuza wewe, kingine kwa ajili kumtukuza Musa na kingine wa ajili ya kumtukuza Eliya.” Petro hakujua alichokuwa anasema.
34 Petro alipokuwa akisema mambo haya, wingu likaja, likawafunika wote. Petro, Yohana na Yakobo waliogopa walipofunikwa na wingu. 35 Sauti ikatoka katika wingu na kusema, “Huyu ni Mwanangu. Ndiye niliyemchagua. Mtiini yeye.”
36 Sauti hiyo ilipomalizika, Yesu peke yake ndiye alikuwa pale. Petro, Yohana na Yakobo hawakusema chochote. Na kwa muda mrefu baada ya hilo, hawakumwambia mtu yeyote yale waliyoyaona.
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-18; Mk 9:14-27)
37 Siku iliyofuata, Yesu, Petro, Yohana na Yakobo walitelemka kutoka mlimani. Kundi kubwa la watu likaenda kukutana naye. 38 Mtu mmoja katika umati huo alimwita Yesu akisema, “Mwalimu, tafadhali njoo umwonee mwanangu. Ni mtoto pekee niliye naye. 39 Pepo mchafu humvaa na hupiga kelele, humtia kifafa na kumtoa povu mdomoni. Huendelea kumwumiza na hamwachi kirahisi. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyu mchafu lakini wameshindwa.”
41 Yesu akajibu, “Enyi watu msio na imani. Maisha yenu ni mabaya. Nitakaa na kuchukuliana nanyi mpaka lini?” Ndipo Yesu akamwambia yule mtu, “Mlete kijana wako hapa.”
42 Kijana alipokuwa anakwenda kwa Yesu, pepo mchafu akamwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamwamuru atoke. Kijana akaponywa, na Yesu akampeleka kwa baba yake. 43 Watu wote wakaushangaa ukuu wa nguvu ya Mungu.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Mk 9:30-32)
Watu walipokuwa bado wanayashangaa mambo yote aliyofanya Yesu. Akawaambia wanafunzi wake, 44 “Msiyasahau nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu yu karibu kukamatwa na kuwekwa katika mikono ya watu wengine.” 45 Lakini wanafunzi hawakuelewa alichomaanisha. Maana ilifichwa kwao ili wasitambue. Lakini waliogopa kumwuliza Yesu kuhusiana na alilosema.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Mk 9:33-37)
46 Wafuasi wa Yesu walianza kubishana wakiulizana nani ni mkuu kuliko wote miongoni mwao. 47 Yesu alijua walichokuwa wanafikiri, hivyo akamchukua mtoto mdogo na kumsimamisha karibu yake. 48 Kisha akawaambia, “Yeyote anayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu kwa jina langu ananikaribisha mimi. Na yeyote anayenikaribisha mimi anamkaribisha yule aliyenituma. Aliye mnyenyekevu zaidi miongoni mwenu, ndiye mkuu.”
Asiye Kinyume Nanyi ni Mmoja Wenu
(Mk 9:38-40)
49 Yohana akajibu; “Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kutoka kwa watu akitumia jina lako. Tulimwambia aache kwa sababu hayuko katika kundi letu.”
50 Yesu akamwambia, “Msimkataze. Asiye kinyume nanyi yu pamoja nanyi.”
Katika Mji wa Samaria
51 Wakati ulikuwa unakaribia ambapo Yesu alikuwa aondoke na kurudi mbinguni. Hivyo aliamua kwenda Yerusalemu. 52 Alituma baadhi ya watu kumtangulia. Waliondoka na kwenda katika mji mmoja wa Samaria, ili kumwandalia mahali pa kufikia. 53 Lakini watu katika mji huo hawakumkaribisha Yesu kwa sababu alikuwa anakwenda Yerusalemu. 54 Wafuasi wake; Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema, “Bwana, unataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni na kuwateketeza watu hawa?”[ab]
55 Lakini Yesu aligeuka na akawakemea baada ya wao kusema hivi.[ac] 56 Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaondoka wakaenda katika mji mwingine.
Kumfuata Yesu
(Mt 8:19-22)
57 Walipokuwa wakisafiri pamoja njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote utakakokwenda.”
58 Yesu akamwambia, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate!”
Lakini mtu yule akamwambia, “Bwana, niache nikamzike baba yangu kwanza.”
60 Lakini Yesu akamwambia, “Waache waliokufa wawazike wafu wao. Ni lazima uende kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu.”
61 Mtu mwingine pia akamwambia, “Nitakufuata Bwana, lakini niruhusu kwanza nikaiage familia yangu.”
62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote anayeanza kulima, kisha akaangalia nyuma hajajiandaa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.”
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake 72
10 Baada ya hili, Bwana alichagua wafuasi sabini na wawili[ad] zaidi. Aliwatuma watangulie katika kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda wakiwa wawili wawili. 2 Aliwaambia, “Kuna mavuno mengi ya watu wa kuwaingiza katika Ufalme wa Mungu. Lakini watenda kazi wa kuwaingiza katika ufalme wa Mungu ni wachache. Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni ili atume watenda kazi wengi ili wasaidie kuyaingiza mavuno yake.
3 Mnaweza kwenda sasa. Lakini sikilizeni! Ninawatuma na mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. 4 Msibebe mfuko wowote, wala pesa au viatu. Msisimame kusalimiana na watu njiani. 5 Kabla ya kuingia katika nyumba, mseme, ‘Amani iwemo katika nyumba hii.’ 6 Ikiwa watu wanaoishi katika nyumba hiyo wanapenda amani, baraka yenu ya amani itakaa nao. Lakini kama siyo, baraka yenu ya amani itawarudia. 7 Kaeni katika nyumba inayopenda amani. Kuleni na kunywa chochote watakachowapa kwa maana mfanyakazi anastahili ujira. Msihame kutoka katika nyumba hiyo na kwenda kukaa katika nyumba nyingine.
8 Mkiingia katika mji wowote na watu wakawakaribisha, kuleni vyakula watakavyowapa. 9 Waponyeni wagonjwa wanaoishi katika mji huo, na waambieni Ufalme wa Mungu umewafikia![ae]
10 Lakini mkiingia katika mji wowote na watu wasiwakaribishe, nendeni katika mitaa ya mji huo na mseme, 11 ‘Tunafuta mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana katika miguu yetu! Lakini kumbukeni kwamba: Ufalme wa Mungu umewafikia!’ 12 Ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa watu wa mji huo kuliko watu wa Sodoma.
Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu
(Mt 11:20-24)
13 Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida![af] Watu wenu wameniona nikifanya miujiza mingi ndani yenu, lakini hamkubadilika. Miujiza hiyo hiyo ingefanyika katika miji ya Tiro na Sidoni,[ag] watu katika miji hiyo wangelikwisha badili mioyo na maisha yao siku nyingi. Wangelikwisha vaa nguo za magunia na kukaa kwenye majivu kuonesha kusikitika na kutubu dhambi zao. 14 Lakini itakuwa rahisi kwa miji ya Tiro na Sidoni siku ya hukumu kuliko ninyi. 15 Nawe Kapernaumu, Je! Utatukuzwa mpaka mbinguni? Hapana, utatupwa chini hadi mahali pa kifo.
16 Mtu yeyote akiwasikiliza ninyi wafuasi wangu, hakika ananisikiliza mimi. Lakini mtu yeyote akiwakataa ninyi, hakika ananikataa mimi. Na mtu yeyote akinikataa mimi anamkataa Yule aliyenituma.”
Shetani Aangushwa
17 Wale wafuasi sabini na wawili waliporudi kutoka katika safari yao, walikuwa na furaha sana. Walisema, “Bwana, hata pepo walitutii tulipotumia jina lako!”
18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kama mwanga wa radi kutoka mbinguni! 19 Yeye ndiye adui, lakini tambueni kuwa nimewapa mamlaka zaidi yake. Nimewapa mamlaka ya kuponda nyoka na nge zake kwa miguu yenu. Hakuna kitakachowadhuru. 20 Ndiyo, hata pepo wanawatii. Na mnaweza kufurahi, lakini si kwa sababu mna mamlaka hii. Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Yesu Aomba Kwa Baba
(Mt 11:25-27; 13:16-17)
21 Ndipo Yesu akajisikia furaha kwa uweza wa Roho Mtakatifu, akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, BWANA wa mbingu na nchi. Ninashukuru kwamba umewaficha mambo haya wenye hekima na akili nyingi. Lakini umeyafunua kwa watu walio kama watoto wadogo. Ndiyo, Baba, umefanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulitaka kufanya.
22 Baba yangu amenipa vitu vyote. Hakuna anayejua Mwana ni nani, Baba peke yake ndiye anayejua. Na Mwana peke yake ndiye anayejua Baba ni nani. Watu pekee watakaojua kuhusu Baba ni wale ambao Mwana amechagua kuwaambia.”
23 Wafuasi walikuwa na Yesu peke yao na Yesu aliwageukia akasema, “Ni baraka kubwa kwenu kuyaona mnayoyaona sasa! 24 Ninawaambia, Manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mambo haya mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona, na walitamani kuyasikia mnayoyasikia ninyi lakini hawakuweza.”
Simulizi Kuhusu Msamaria Mwema
25 Kisha mwanasheria mmoja alisimama ili amjaribu Yesu. Akasema, “Mwalimu, ninatakiwa nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26 Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Unaielewaje?”
27 Yule mwana sheria akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.’(J) Pia ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(K)
28 Yesu akasema, “Jibu lako ni sahihi. Fanya hivi nawe utaupata uzima wa milele.”
29 Lakini mwanasheria alitaka kuonesha kuwa alikuwa mwenye haki na aliishi kwa usahihi. Hivyo akamwuliza Yesu, “Lakini si kila mtu aliye jirani yangu, au unasemaje?”
30 Katika kujibu swali hili, Yesu akasema, “Mtu mmoja alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani alivamiwa na majambazi, wakamchania nguo na kumpiga. Kisha wakamwacha amelala chini akiwa katika hali ya kufa.
31 Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa anasafiri kupitia njia hiyo hiyo. Alipomwona, hakusimama ili amsaidie, alikwenda zake. 32 Kisha Mlawi[ah] alipokaribia na kumwona yule mtu, alipita upande mwingine. Hakusimama ili amsaidie, Alikwenda zake.
33 Ndipo Msamaria[ai] mmoja aliyekuwa anasafiri kupitia njia ile ile, alipofika mahali ambapo mtu aliyejeruhiwa alikuwa amelala, alipomwona alimhurumia. 34 Alimkaribia ili amsaidie, akamsafisha majeraha kwa mafuta ya zeituni na divai,[aj] kisha akayafunga majeraha yake. Msamaria alikuwa na punda. Akampandisha juu ya punda wake na kumpeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni. Akamhudumia huko. 35 Siku iliyofuata, Msamaria alitoa sarafu mbili za fedha na kumpa mtunza nyumba ya wageni, akamwambia, ‘Mtunze mtu huyu aliyejeruhiwa. Ukitumia pesa nyingi zaidi kwa kumhudumia, nitakulipa nitakapokuja tena.’”
36 Kisha Yesu akasema, “Ni yupi kati ya hawa watu watatu unadhani hakika alikuwa jirani wa yule mtu aliyepigwa na majambazi?”
Footnotes
- 1:1 Theofilo Theofilo ndiye aliyemdhamini Luka katika mradi wa utafiti na uandishi wa kitabu hiki na kingine (Matendo ya Mitume). Ijapokuwa ni kama aliandikiwa yeye, makusudi ya mwandishi na Roho Mtakatifu ni kuwa watu wote wakisome. Theofilo maana yake ni “Mpendwa wa Mungu”.
- 1:5 makuhani wa kikundi Makuhani wa Kiyahudi waligawanywa katika vikundi 24. Tazama 1 Mambo ya Nyakati sura ya 24. Vikundi hivi 24 vya Makuhani vilihudumu katika Hekalu mjini Yerusalemu kwa zamu (mzunguko). Kila kikundi kilikuwa na zamu kwa wiki nzima, aghalabu wiki mbili kwa mwaka.
- 1:59 kumtahiri Yaani, kumfanyia tohara kama ilivyokuwa katika sheria ya Musa.
- 1:63 ubao wa kuandikia Ni ubao uliokuwa umepakwa nta au mpira ili usiloe.
- 1:78 siku mpya Kwa maana ya kawaida, “Alfajiri”, imetumika hapa kama ishara ikimaanisha Masihi, Bwana.
- 2:1 Rumi Au “dola ya ulimwengu ya Rumi”.
- 2:1 wahesabiwe na kuorodheshwa Yaani, “Sensa”, lengo hasa ilikuwa waorodheshwe katika kumbukumbu za serikali kwa ajili ya kulipa kodi.
- 2:7 hori la kulishia mifugo Sehemu au chombo cha kulishia mifugo. Pia katika mstari wa 12 na 16.
- 2:11 Kristo Kwa maana ya kawaida “Kristo”, ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi” linalomaanisha “Mpakwa Mafuta”, ambapo katika Agano la Kale linawakilisha sherehe ya kupakwa mafuta (Kuwekwa Wakfu) mfalme mpya. Pia linamaanisha Mfalme Mteule. Tazama Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 26 na katika kitabu chote hiki.
- 2:22 baada ya mtoto kuzaliwa Sheria ya Musa iliagiza kuwa ifikapo siku 40 baada mwanamke wa Kiyahudi kuzaa mtoto, yule mtoto anapaswa kutakaswa kwa sherehe maalumu Hekaluni. Tazama Law 12:2-8.
- 2:23 wakfu kwa ajili ya Bwana Tazama Kut 13:2,12.
- 2:24 hua Hua (au tetere) ni njiwa wa porini, ni wadogo kuliko wale wanaofugwa na huruka kwa mwendo kasi. Imenukuliwa kutoka Law 12:8.
- 3:9 miti Watu wasiomtii Mungu ni kama miti itakayokatwa.
- 3:15 Masihi Ni neno la Kiebrania lililo na maana sawa na Kristo kwa Lugha ya Kiyunani (Kigiriki), maana yake ni Mpakwa Mafuta.
- 3:32 Salmoni Au “Sala”, kama ilivyo katika nakala za zamani za tafsiri ya Kiyunani ya Kale. Tazama Mt 1:4-5 na 1 Nya 2:11.
- 3:33 Aramu Baadhi ya nakala za Kiyunani zina “Arni” au “Ramu”; majina mengine ya Aramu.
- 4:38 Simoni Jina jingine la Simoni lilikuwa Petro. Pia katika 5:3,4,5,10.
- 5:1 Galilaya Kwa maana ya kawaida, “Genesareti”.
- 5:14 kuhani akakuchunguze Sheria ya Musa ilisema ni lazima kuhani aamue ikiwa mtu aliyekuwa na ukoma amepona.
- 5:37 divai mpya Maji ya zabibu ambayo ndiyo yanaanza kuchachuka na hutengeneza mgandamizo ndani ya chombo kilichofungwa.
- 7:23 Heri … kunikubali mimi Au “Baraka kuu ni kwa wale wasio na mashaka kunikubali.”
- 7:36 akaketi Waliketi kwa kujilaza kidogo kuelekea katika meza ya chakula katika mzunguko, miguu yao ikiwa imenyooka kwa nyuma.
- 8:14 hayazalishi matokeo mazuri … yao Hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao ina maana ya, “kukua kiroho”, ama watu hawa hawafanyi mambo mazuri ambayo Mungu anataka wayafanye.
- 8:26 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”.
- 8:30 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi.
- 8:31 shimoni Hii ina maana kuwa ni shimo lisilo na mwisho. Ni kama shimo refu ambalo mapepo hukaa (kuzimu).
- 8:43 Alikuwa ametumia … madaktari Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.
- 9:54 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza “Kama Eliya alivyofanya?”
- 9:55 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza “Na akasema, ‘Hamjui mna roho ya namna gani. 56 Mwana wa Adamu hakuja kuyateketeza maisha ya watu bali kuyaokoa.’”
- 10:1 sabini na wawili Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza wafuasi sabini. Pia katika mstari wa 17.
- 10:9 umewafikia Au “unakuja kwenu haraka” au “umewafikia”.
- 10:13 Korazini, Bethsaida Miji ya Kiyahudi iliyokuwa kando kando mwa Ziwa Galilaya ambapo Yesu alifanya miujiza mingi kudhihirisha mamlaka yake yanayotoka kwa Mungu. Pamoja na hili, watu walikataa kubadili maisha waliyoishi yasiyokuwa na Mungu.
- 10:13 Tiro na Sidoni Miji iliyojaa ibada ya sanamu ambayo ilijulikana sana kwa uovu uliokuwemo humo.
- 10:32 Mlawi Yaani mtumishi wa Hekalu.
- 10:33 Msamaria Wayahudi waliwachukulia Wasamaria kama maadui. Tazama Msamaria katika Orodha ya Maneno.
- 10:34 mafuta ya zeituni na divai Vilitumika kama dawa kwa ajili ya kulainisha na kusafisha majeraha.
© 2017 Bible League International