Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mariamu Amsifu Mungu
46 Mariamu akasema,
“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47 kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
wangu amenipa furaha kuu!
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
49 Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
Jina lake ni takatifu.
50 Na huwapa rehema zake wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51 Ameonesha nguvu ya mkono wake;
Amewatawanya wanaojikweza.
52 Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
na kuwakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54 Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
Amekumbuka kuonesha rehema;
55 Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
Ibrahimu na wazaliwa wake.”
Tuliuona Utukufu wa Kristo
16 Tuliwaambia kuhusu nguvu ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake katika nguvu kuu. Mambo tuliyowaambia hayakuwa simulizi za kuvutia zilizotungwa watu. Hapana, tuliuona ukuu wa Yesu kwa macho yetu wenyewe. 17 Yesu aliisikia sauti ya Mungu Mkuu na Mwenye Mtukufu alipopokea heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba. Sauti ilisema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda. Ninafurahishwa naye.” 18 Nasi tuliisikia sauti hiyo. Sauti hiyo ilitoka mbinguni tulipokuwa na Yesu juu ya mlima mtakatifu.[a]
19 Hili linatufanya tuwe na ujasiri kwa yale waliyosema manabii. Na ni vizuri ninyi mkifuata yale waliyosema, ambayo ni kama mwanga unaoangaza mahali penye giza. Mna mwanga unaoangaza mpaka siku inapoanza na nyota ya asubuhi huleta mwanga mpya katika fahamu zenu. 20 Jambo la muhimu kuliko yote ambalo ni lazima mlielewe ni hili ya kwamba hakuna unabii katika Maandiko unaotokana na mawazo ya nabii. 21 Nabii hakusema kile alichotaka kusema. Lakini wanadamu waliongozwa na Roho Mtakatifu kusema ujumbe uliotoka kwa Mungu.
© 2017 Bible League International