Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Afundisha Kuhusu Uzinzi
27 Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Usizini’.(A) 28 Lakini ninawaambia kuwa mwanaume akimwangalia mwanamke na akamtamani, amekwisha kuzini naye katika akili yake. 29 Jicho la kuume likikufanya utende dhambi, liondoe na ulitupe. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote ukatupwa Jehanamu. 30 Na mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, uukate na kuutupa. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote kutupwa Jehanamu.
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mt 19:9; Mk 10:11-12; Lk 16:18)
31 Ilisemwa pia kuwa, ‘Kila anayemtaliki mkewe ni lazima ampe hati ya talaka.’(B) 32 Lakini ninawaambia kuwa, kila atakayemtaliki mkewe kutokana na sababu isiyohusiana na uzinzi, anamfanya mke wake kuwa mzinzi. Na kila atakayemwoa mwanamke aliyetalikiwa, atakuwa anazini.
Yesu Afundisha Kuhusu Kiapo
33 Pia, mmesikia hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Unaweka kiapo, usishindwe kutimiza kile ulichoapa kufanya. Timiza kiapo ulichoweka mbele za Bwana.’ 34 Lakini ninawaambia mnapoweka ahadi, msiape kwa jina la mbingu, kwa sababu mbingu ni kiti cha enzi cha Mungu. 35 Na usiape kwa jina la dunia kwa sababu, dunia ni mahali pa kuweka miguu yake. Wala msiape kwa jina la mji wa Yerusalemu, kwa sababu nao ni mali yake Mungu, aliye Mfalme Mkuu. 36 Pia usiape kwa jina la kichwa chako kana kwamba ni uthibitisho kuwa utatimiza kiapo, kwa sababu huwezi kuufanya hata unywele mmoja wa kichwa chako kuwa mweusi au mweupe.
© 2017 Bible League International