Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Tunapaswa Kuendelea Kumfuata Mungu
7 Ni kama vile anavyosema Roho Mtakatifu:
“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
8 msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani,
mlipomgeuka Mungu.
Hiyo ndiyo siku ulipomjaribu Mungu mle jangwani.
9 Kwa miaka 40 jangwani, watu wako wakaona niliyoyatenda.
Lakini walinijaribu na ustahimilivu wangu.
10 Hivyo nikawakasirikia.
Nikasema, ‘Mawazo yao siku zote hayako sahihi.
Hawajawahi kamwe kuzielewa njia zangu.’
11 Hivyo nilikasirika na kuweka ahadi:
‘Kamwe hawataingia katika sehemu yangu ya pumziko.’”(A)
12 Hivyo ndugu na dada, muwe makini ili asiwepo miongoni mwenu atakayekuwa na mawazo maovu yanayosababisha mashaka mengi ya kuwafanya muache kumfuata Mungu aliye hai. 13 Bali mhimizane ninyi kwa ninyi kila siku, maadamu mna kitu kinachoitwa “leo.”[a] Msaidiane ninyi kwa ninyi ili asiwepo miongoni mwenu atakayedanganywa na dhambi akawa mgumu sana kubadilika. 14 Tunayo heshima ya kushirikishana katika yote aliyo nayo Kristo endapo tutaendelea hadi mwisho kuwa na imani ya uhakika tuliyokuwa nayo mwanzoni. 15 Ndiyo sababu Roho anasema:
“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani,
wakati mlipogeuka mbali na Mungu.”(B)
16 Ni nani hawa walioisikia sauti ya Mungu na kugeuka kinyume naye? Walikuwa watu wote ambao Musa aliwaongoza kutoka Misri. 17 Na ni kina nani waliokasirikiwa na Mungu kwa miaka 40? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi. Na maiti zao zikaachwa jangwani. 18 Na ni watu gani ambao Mungu alikuwa akisema nao alipotoa ahadi kuwa kamwe wasingeingia mahali penye mapumziko? Alikuwa anazungumza nao ambao hawakumtii. 19 Hivyo tunaona kuwa hawakuruhusiwa kuingia na kupata pumziko la Mungu, kwa sababu hawakuamini.
© 2017 Bible League International