Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
5 Kila kuhani Mkuu wa Kiyahudi alichaguliwa kutoka miongoni mwa watu. Kuhani huyo anapewa kazi ya kuwasaidia watu katika mambo wanayopaswa kumfanyia Mungu. Anapaswa kumtolea Mungu sadaka na sadaka za dhambi. 2 Kuhani mkuu anao udhaifu wake binafsi. Hivyo anapaswa kuwa mpole kwa wale wanaokosea kwa sababu ya kutokujua. 3 Hutoa sadaka kwa ajili ya dhambi zao, lakini kutokana na udhaifu wake anapaswa pia kutoa sadaka kwa ajili dhambi zake mwenyewe.
4 Kuwa kuhani mkuu ni heshima. Lakini hayupo anayejichagua mwenyewe kwa ajili ya kazi hii. Mtu huyo anapaswa kuwa amechaguliwa na Mungu kama alivyokuwa Haruni. 5 Ndivyo ilivyo hata kwa Kristo. Hakujichagua mwenyewe kuwa na heshima na kuwa kuhani mkuu. Lakini Mungu alimchagua. Mungu akamwambia:
“Wewe ni mwanangu.
Leo nimekuwa baba yako.”(A)
6 Na katika sehemu nyingine ya Maandiko Mungu anasema:
“Wewe ni kuhani mkuu milele;
kama Melkizedeki alivyokuwa kuhani.”(B)
7 Yesu alipoishi duniani alimwomba Mungu, akiusihi msaada kutoka kwa yule anayeweza kumwokoa kutoka mauti. Alimwomba Mungu kwa sauti kuu na kwa machozi. Na Mungu alizisikia sala zake kwa sababu ya heshima yake kuu kwa Mungu. 8 Yesu alikuwa mwana wa Mungu, lakini aliteseka, na kwa njia ya mateso yake alijifunza kutii chochote alichosema Mungu. 9 Hili lilimfanya yeye awe kuhani mkuu mkamilifu, anayetoa njia kwa ajili ya kila mmoja anayemtii ili kuokolewa milele. 10 Mungu alimfanya yeye kuhani mkuu, kama alivyokuwa Melkizedeki.
Yakobo na Yohana Waomba Kutawala Pamoja na Yesu
(Mt 20:20-28)
35 Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu, wakamwambia, “Mwalimu tunataka utufanyie kile tunachokuomba.”
36 Yesu akawaambia, “Ni kitu gani mnachotaka niwafanyie?”
37 Nao wakamwambia, “Uturuhusu tuketi pamoja nawe katika utukufu wako, mmoja wetu aketi kulia kwako na mwingine kushoto kwako.”
38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnachokiomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninachokinywea[a] mimi? Au mnaweza kubatizwa ubatizo ninaobatizwa?”
39 Wakamwambia, “Tunaweza.”
Kisha Yesu akawaambia, “Mtakinywa kikombe cha mateso ninachokunywa mimi, na mtabatizwa ubatizo[b] ninaobatizwa mimi. 40 Lakini kuhusu kuketi kulia kwangu ama kushoto kwangu siyo mamlaka yangu kusema. Mungu ameandaa nafasi hizo kwa ajili ya wale aliowateuwa.”
41 Wale wanafunzi kumi wengine walipoyasikia maombi haya, waliwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Na Yesu akawaita wale wanafunzi kumi na kusema, “Mnajua kuwa miongoni mwa mataifa watawala huwa na mamlaka makubwa juu ya watu, na viongozi wenye nguvu huwakandamiza watu wao. 43 Haipaswi kuwa hivyo miongoni mwenu. Kwani yeyote atakaye kuwa mkuu miongoni mwenu basi na awe mtumishi wenu. 44 Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima akubali kuwa mtumwa wenu wote. 45 Kwani hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa bali alikuja kuwatumikia wengine na kuyatoa maisha yake ili kuwaweka huru wengi.”
© 2017 Bible League International