Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
11 Watu walipewa sheria chini ya mfumo wa makuhani waliotoka katika ukoo wa Lawi. Lakini hayupo awezaye kufanywa mkamilifu kiroho kwa njia ya mfumo wa makuhani. Hivyo lilikuwepo hitaji la kuhani mwingine kuja. Namaanisha kama Melkizedeki, siyo Haruni. 12 Na anapokuja kuhani wa aina nyingine, basi sheria pia inabidi ibadilishwe. 13-14 Tunazungumza juu ya Bwana Yesu, aliyetoka katika kabila lingine. Hakuwepo yeyote kutoka katika kabila hilo kamwe aliyeweza kutumika kama kuhani madhabahuni. Ni dhahiri kwamba Bwana Yesu alitoka katika kabila la Yuda. Na Musa hakusema chochote kuhusu makuhani waliyetokana na kabila hilo.
Yesu Ni Kuhani Mfano wa Melkizedeki
15 Na mambo haya yalizidi kuwa wazi zaidi tunapomwona kuhani mwingine aliye kama Melkizedeki. 16 Alifanywa kuhani, lakini siyo kwa sababu alikamilisha mahitaji ya kuzaliwa katika familia sahihi. Alifanyika kuhani kwa nguvu ya uhai ambayo haitakwisha. 17 Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema kumhusu yeye: “Wewe ni kuhani milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.”(A)
18 Hivyo mfumo wa sheria za zamani zilizowekwa sasa zinaisha kwa sababu zilikuwa dhaifu na hazikuweza kutusaidia. 19 Sheria ya Musa haikuweza kukamilisha kitu chochote. Lakini sasa tumaini bora zaidi limeletwa kwetu. Na kwa tumaini hilo tunaweza kumkaribia Mungu.
20 Vile vile, ni muhimu kwamba Mungu aliweka ahadi kwa kiapo alipomfanya Yesu kuwa kuhani mkuu. Watu hawa wengine walipofanyika makuhani, hapakuwepo kiapo. 21 Lakini Yesu akafanyika kuhani kwa kiapo cha Mungu. Mungu alimwambia:
“Bwana anaweka ahadi kwa kiapo
naye hatabadili mawazo yake:
‘Wewe ni kuhani milele.’”(B)
22 Hivyo hii inamaanisha kwamba Yesu ni uhakika wa agano zuri zaidi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake.
© 2017 Bible League International