Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Umati Mkubwa
9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu. Walikuwa wengi hakuna mtu angeweza kuwahesabu wote. Walikuwa wametoka katika kila taifa, kabila, rangi za watu na lugha za dunia. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Wote walikuwa wamevaa majoho meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Walipaza sauti kwa nguvu, wakasema “Ushindi ni wa Mungu wetu, anayeketi kwenye kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo.”
11 Wazee na wenye uhai wanne walikuwa pale. Malaika wote walikuwa wamesimama kuwazunguka na kukizunguka kiti cha enzi. Malaika wakainamisha nyuso zao, wakasujudu mpaka chini mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu. 12 Walisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, nguvu na uweza ni vyake Mungu wetu milele na milele. Amina!”
13 Kisha mmoja wa wazee akaniuliza, “Watu hawa waliovaa kanzu nyeupe ni akina nani? Wametoka wapi?”
14 Nikajibu, “Wewe unajua ni akina nani, bwana.”
Mzee akasema, “Hawa ni wale waliokuja kutokana na mateso makuu. Wamefua kanzu zao[a] kwa kutumia damu ya Mwanakondoo, wako safi na ni weupe. 15 Hivyo sasa watu hawa wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Wanamwabudu Mungu mchana na usiku hekaluni mwake. Naye aketiye kwenye kiti cha enzi atawalinda. 16 Hawatasikia njaa tena. Hawatasikia kiu tena. Jua halitawadhuru. Hakuna joto litakalowachoma. 17 Mwanakondoo mbele ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao. Atawaongoza kwenda kwenye chemichemi za maji ya uzima. Na Mungu atafuta kila chozi kutoka kwenye macho yao.”
© 2017 Bible League International