Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
8 1-3 Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.
Matatizo Kwa waamini
Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. 4 Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Ahubiri Katika Samaria
5 Filipo[a] alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. 6 Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. 7 Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. 8 Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!
© 2017 Bible League International