Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Tutakuwa na Mwili wa Namna Gani?
35 Lakini mtu mmoja anaweza kuuliza, “Waliokufa wanafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Haya ni maswali ya kijinga. Unapopanda kitu fulani, ni lazima kife udongoni kabla hakijawa hai na kuota. 37 Na unapopanda kitu fulani, unachopanda hakina “mwili” sawa na ule kitakachokuwa nao baadaye. Unapanda mbegu, pengine ngano au kitu kingine. 38 Na yeye Mungu hutoa mwili kwa kila aina ya mbegu. 39 Vitu vyote vilivyoumbwa kwa mwili haviko sawa: Wanadamu wana aina moja ya mwili, wanyama wana aina nyingine, ndege wana nyingine na samaki nao wana aina yao. 40 Pia kuna miili ya kimbingu na miili ya kidunia. Lakini uzuri wa miili ya kimbingu ni wa aina yake na uzuri wa miili ya kidunia ni kitu kingine. 41 Jua lina uzuri wa aina yake, mwezi una aina yake na nyota zina aina nyingine ya uzuri. Na kila nyota iko tofauti kwa uzuri wake.
42 Ndivyo itakavyokuwa waliokufa watakapofufuliwa na kuwa hai. Mwili “uliopandwa” kaburini utaharibika na kuoza, lakini utafufuliwa katika uhai usioharibika. 43 Mwili hauna heshima “unapopandwa”. Lakini utakapofufuliwa, utakuwa na utukufu. Mwili unakuwa dhaifu “unapopandwa”. Lakini unapofufuliwa, unakuwa na nguvu nyingi. 44 Mwili unaopandwa ni mwili wa kawaida, wa asili. Utakapofufuliwa utakuwa mwili wa ajabu uliopewa uwezo na Roho.
Kuna mwili wa asili unaoonekana kwa macho. Na hivyo kuna mwili wa Kiroho wa ajabu. 45 Kama Maandiko yanavyosema, “Mtu[a] wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe asili kilichokuwa hai.”(A) Lakini Adamu[b] wa mwisho akafanyika roho. 46 Mtu wa kiroho hakuja kwanza. Mtu wa asili anayeonekana kwa macho ndiye alikuja kwanza; kisha akaja wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza alitokana na mavumbi ya dunia. Mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Watu wote ni wa dunia. Wako sawa na yule mtu wa kwanza wa dunia. Lakini wale walio wa mbinguni wako kama mtu wa mbinguni. 49 Tumeivaa sura ya mtu aliyetoka mavumbini, pia tutaivaa sura ya mtu aliyetoka mbinguni.
© 2017 Bible League International