Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Petro Amponya Kiwete
3 Siku moja Petro na Yohana walikwenda eneo la Hekalu saa tisa mchana, muda wa kusali na kuomba Hekaluni kama ilivyokuwa desturi. 2 Walipokuwa wanaingia katika eneo la Hekalu, mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu maisha yake yote alikuwa amebebwa na baadhi ya rafiki zake waliokuwa wanamleta Hekaluni kila siku. Walimweka pembezoni mwa mojawapo ya Malango nje ya Hekalu. Lango hilo liliitwa Lango Zuri. Na mtu huyo alikuwa akiwaomba pesa watu waliokuwa wanaingia Hekaluni. 3 Siku hiyo alipowaona Petro na Yohana wakiingia eneo la Hekalu, aliwaomba pesa.
4 Petro na Yohana, walimtazama mtu huyo, wakamwambia, “Tutazame!” 5 Akawatazama akitumaini kuwa wangempa pesa. 6 Lakini Petro akasema, “Sina fedha wala dhahabu yoyote, lakini nina kitu kingine ninachoweza kukupa. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama na utembee!”
7 Kisha Petro akamshika mkono wake wa kulia, akamnyenyua na kumsimamisha. Ndipo nyayo na vifundo vyake vikatiwa nguvu papo hapo. 8 Akaruka juu, akasimama kwa miguu yake na akaanza kutembea. Akaingia ndani ya eneo la Hekalu pamoja nao huku akitembea na kurukaruka akimsifu Mungu. 9-10 Watu wote walimtambua. Walimjua kuwa ni mlemavu wa miguu ambaye mara nyingi huketi kwenye Lango Zuri la Hekalu akiomba pesa. Lakini sasa walimwona anatembea na kumsifu Mungu. Walishangaa na hawakuelewa hili limewezekanaje.
Iweni Kama Mtumishi
24 Baadaye, mitume wakaanza kubishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu. 25 Lakini Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa wanawatawala watu kama watumwa wao, na wenye mamlaka juu ya wengine wanataka kuitwa, ‘Wafadhili Wakuu’. 26 Lakini ni lazima msiwe hivyo. Aliye na mamlaka zaidi miongoni mwenu lazima awe kama asiye na mamlaka. Anayeongoza anapaswa kuwa kama anayetumika. 27 Nani ni mkuu zaidi: Yule anayetumika au yule aliyekaa mezani na kuhudumiwa? Kila mtu hudhani ni yule aliyekaa mezani akihudumiwa, sawa? Lakini nimekuwa pamoja nanyi kama ninayetumika.
28 Na ninyi ndiyo mliobaki pamoja nami katika mahangaiko mengi. 29 Hivyo ninawapa mamlaka kutawala pamoja nami katika ufalme ambao Baba yangu amenipa. 30 Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme huo. Mtakaa katika viti vya enzi na kuwahukumu makabila kumi na mbili ya Israeli.
© 2017 Bible League International