Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
5 Siku iliyofuata, watawala wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria walikutana Yerusalemu. 6 Kuhani mkuu Anasi alikuwepo. Kayafa, Yohana, Iskanda na jamaa wengine wa kuhani mkuu walikuwepo pia. 7 Waliwasimamisha Petro na Yohana mbele ya watu wote. Wakawauliza maswali mengi, “Mliwezaje kumponya mlemavu wa miguu huyu? Mlitumia nguvu gani? Mmefanya hili kwa mamlaka ya nani?”
8 Ndipo Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, “Enyi watawala nanyi wazee wa watu, 9 mnatuuliza leo ni nini tulifanya kumsaidia huyu mlemavu wa miguu? Mnatuuliza nini kilimponya? 10 Tunataka ninyi nyote na watu wote wa Israeli mtambue kuwa mtu huyu aliponywa na nguvu ya Yesu Kristo kutoka Nazareti. Mlimpigilia Yesu msalabani, lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Mtu huyu alikuwa mlemavu wa miguu, lakini sasa ni mzima. Anaweza kusimama hapa mbele zenu kwa sababu ya nguvu ya Yesu! 11 Yesu ndiye
12 Yesu peke yake ndiye anayeweza kuokoa watu. Jina lake ndiyo nguvu pekee iliyotolewa kumwokoa mtu yeyote ulimwenguni. Ni lazima tuokoke kupitia yeye!”
16 Hivi ndivyo tunavyojua jinsi upendo wa kweli ulivyo: Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hivyo nasi tunapaswa kuyatoa maisha yetu, kwa ajili ya ndugu wa kike na wa kiume katika familia ya Kristo. 17 Itakuwaje pale muumini tajiri mwenye fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote akamwona dada ama kaka yake aliye maskini na asiye na fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote. Endapo muumini huyu tajiri hatamsaidia muumini yule maskini, basi ni wazi kwamba upendo wa Mungu haumo ndani ya muumini yule tajiri. 18 Watoto wangu, upendo wetu usiwe wa maneno na kuongea tu. Hapana, upendo wetu unapaswa kuwa halisi. Hatuna budi kuuonyesha upendo wetu kwa mambo yale tunayofanya.
19-20 Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa sisi tu wa ile njia ya kweli. Pale mioyo yetu inapotufanya tujisikie kuwa na hatia, bado tunaweza kuwa na amani mbele za Mungu, kwa sababu Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu. Yeye anajua kila kitu.
21 Rafiki zangu wapendwa, ikiwa hatujisikii kuwa tunatenda yasiyo haki, basi hatupaswi kuwa na hofu tunapoenda kwa Mungu. 22 Na Mungu anatupa kile tunachomwomba. Nasi tunapokea kwa sababu tunazitii amri za Mungu na kufanya yanayompendeza. 23 Hili ndilo Mungu analoliamuru: Kwamba tumwamini Mwanaye Yesu Kristo, na kwamba tupendane sisi kwa sisi kama alivyoamuru. 24 Wote wanaozitii amri za Mungu wanaishi ndani ya Mungu. Na Mungu anaishi ndani yao. Tunajuaje kuwa Mungu anaishi ndani yetu? Tunajua kwa sababu ya Roho aliyetupa sisi.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. 18 Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.”
© 2017 Bible League International