Revised Common Lectionary (Complementary)
Yohana Aonya juu ya Walimu wa Uongo
4 Rafiki zangu wapenzi, manabii wengi wa uongo wapo duniani sasa. Hivyo msiiamini kila roho, lakini zijaribuni hizo roho ili muone kama zinatoka kwa Mungu. 2 Hivi ndivyo mwezavyo kuitambua Roho ya Mungu. Roho inayosema, “Naamini kuwa Yesu ni Masihi aliye kuja duniani na akafanyika mwanadamu.” Roho hiyo inatoka kwa Mungu. 3 Roho inayokataa kutamka hayo juu ya Yesu, hii ni roho iliyo adui kwa Kristo. Mmesikia kuwa adui wa kristo anakuja, na sasa amekwishakuja naye yupo tayari ulimwenguni.
4 Wanangu wapenzi, ninyi ni wa Mungu, hivyo mmeshawashinda tayari hawa manabii wa uongo. Hii ni kwa sababu yule aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliyeko duniani. 5 Wao ni wa ulimwengu. Hivyo kile wanachokisema ni cha ulimwengu pia. Na ulimwengu husikia kile wanachokisema. 6 Lakini sisi tunatokana na Mungu. Kwa hiyo watu wanaomjua Mungu hutusikia sisi. Lakini watu wasiotokana na Mungu hawatusikii sisi. Hivi ndivyo tunavyiojua Roho iliyo ya kweli na ile iliyo ya uongo.
© 2017 Bible League International