M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)
6 Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. 2 Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? 3 Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.
4 Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” 5 Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)
7 Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. 8 Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. 9 Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”
12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[a] wagonjwa wengi na kuwaponya.
Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji
(Mt 14:1-12; Lk 9:7-9)
14 Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.”
15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”
Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.”
16 Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.”
Yohana Mbatizaji Alivyouawa
17 Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” 19 Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. 20 Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza.
21 Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. 22 Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo.
Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” 23 Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!”
24 Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?”
Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
25 Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.”
26 Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. 27 Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, 28 na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)
30 Mitume walikusanyika kumzunguka Yesu, na wakamweleza yote waliyofanya na kufundisha. 31 Kisha Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate peke yenu hadi mahali patulivu na palipo mbali na watu wengine ili mpumzike kidogo”, kwani pale walikuwepo watu wengi wakija na kutoka, nao hawakuwa na nafasi ya kula.
32 Kwa hiyo wakaondoka na mtumbwi kuelekea mahali patulivu na mbali na watu wakiwa peke yao. 33 Lakini watu wengi waliwaona wakiondoka na waliwafahamu wao ni kina nani; kwa hiyo walikimbilia pale kwa njia ya nchi kavu kutoka vitongoji vyote vilivyolizunguka eneo hilo wakafika kabla ya Yesu na wanafunzi wake. 34 Alipotoka katika mashua, Yesu aliona kundi kubwa, na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Kwa sasa ilikuwa imekwisha kuwa jioni sana. Kwa hiyo wanafunzi wake walimwijia na kusema, “Hapa ni mahali palipojitenga na sasa hivi saa zimeenda. 36 Uruhusu watu waende zao, ili kwamba waende kwenye mashamba na vijiji vinavyozunguka na waweze kujinunulia kitu cha kula.”
37 Lakini kwa kujibu aliwaambia, “Ninyi wenyewe wapeni kitu cha kula.”
Wao Wakamwambia, “Je, twende kununua mikate yenye thamani ya mshahara wa mtu mmoja[b] wa miezi minane na kuwapa wale?”
38 Yesu akawambia, “Ni mikate mingapi mliyonayo? Nendeni mkaone.”
Walienda kuhesabu, wakarudi kwa Yesu na kusema, “Tunayo mikate mitano na samaki wawili.”
39 Kisha akawaagiza wakae chini kila mmoja kwenye majani mabichi kwa vikundi. 40 Nao wakakaa kwa vikundi vya watu mia na mmoja na vya watu hamsini.
41 Akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akashukuru na akaimega. Akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Pia aligawanya samaki wawili miongoni mwao wote.
42 Wakala na wote wakatosheka. 43 Wakachukua mabaki ya vipande vya mikate na samaki na kujaza vikapu kumi na viwili. 44 Na idadi ya wanaume waliokula ile mikate ilikuwa 5,000.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mt 14:22-33; Yh 6:16-21)
45 Mara Yesu akawafanya wafuasi wake wapande kwenye mashua na wamtangulie kwenda Bethsaida upande wa pili wa ziwa, wakati yeye akiliacha lile kundi liondoke. 46 Baada ya Yesu kuwaaga wale watu, alienda kwenye vilima kuomba.
47 Ilipotimia jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Naye akawaona wanafunzi wake wakihangaika kupiga makasia, kwani upepo uliwapinga. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi Yesu aliwaendea akitembea juu ya ziwa. Yeye akiwa karibu kuwapita, 49 wanafunzi wake wakamwona akitembea juu ya ziwa,[c] na wakafikiri kuwa alikuwa ni mzimu, ndipo walipopiga kelele. 50 Kwa kuwa wote walimwona, na wakaogopa. Mara tu alizungumza nao na kuwaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Usiogope.” 51 Kisha alipanda kwenye mtumbwi pamoja nao, na upepo ukatulia. Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa bado hawajauelewa ule muujiza wa mikate. Kwani fahamu zao zilikuwa zimezibwa.
Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa
(Mt 14:34-36)
53 Walipolivuka ziwa, walifika Genesareti na wakaifunga mashua. 54 Walipotoka katika mashua, watu wakamtambua Yesu, 55 Wakakimbia katika lile jimbo lote na kuanza kuwabeba wagonjwa katika machela na kuwapeleka pale waliposikia kuwa Yesu yupo. 56 Na kila alipoenda vijijini, mijini na mashambani, waliwaweka wagonjwa kwenye masoko, na wakamsihi awaache waguse pindo la koti lake. Na wote walioligusa walipona.
Kufa kwa Dhambi Lakini Hai Kwa Ajili ya Mungu
6 Hivyo, je, mnadhani inatupasa tuendelee kutenda dhambi ili Mungu atupe neema nyingi zaidi na zaidi? 2 Hapana! Utu wetu wa zamani wa dhambi ulikwisha. Umekufa. Je, tutaendeleaje kuishi katika dhambi? 3 Je, mmesahau kwamba sisi sote tulifanyika sehemu ya Kristo Yesu tulipobatizwa? Katika ubatizo wetu tulishiriki katika kifo chake. 4 Hivyo, tulipobatizwa, tulizikwa pamoja na Kristo na kushiriki katika kifo chake. Na kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya ajabu ya Baba, ndivyo nasi tunaweza kuishi maisha mapya sasa.
5 Kristo alikufa, nasi tumeunganishwa pamoja naye kwa kufa kama yeye alivyokufa. Kwa hiyo tutaunganishwa pamoja naye kwa kufufuka kutoka katika kifo kama yeye alivyofanya. 6 Tunajua kuwa utu wetu wa zamani ulikufa msalabani pamoja naye. Hivyo ndivyo maisha ya utumwa tuliyokuwa nayo yalivyoangamizwa ili tusiendelee kuitumikia dhambi tena. 7 Yeyote aliyekufa amewekwa huru kutoka katika nguvu za dhambi.
8 Ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunajua kwamba tutaishi pamoja naye pia. 9 Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na tunajua kuwa hawezi kufa tena. Sasa mauti haina nguvu juu yake. 10 Ndiyo, Kristo alipokufa, alikufa ili aishinde nguvu ya dhambi mara moja, na siyo mara nyingine tena. Sasa anao uzima mpya, na uzima wake huo upo kwa nguvu za Mungu. 11 Kwa namna hiyo hiyo, mnapaswa kujiona kama mliokufa kwa dhambi na mlio hai kwa nguvu za Mungu kupitia Kristo Yesu.
12 Mwili mlionao katika uhai wenu wa sasa hapa duniani utakufa. Msiruhusu dhambi iutawale na kuwafanya ninyi kuzitumikia tamaa zake. 13 Msiitoe sehemu ya miili yenu kwa dhambi kwa ajili ya kutumika kutenda maovu. Jitoeni kwa Mungu, kama watu waliokufa lakini walio hai. Toeni sehemu za miili yenu kwa Mungu ili zitumiwe kwa kutenda mema. 14 Dhambi haitakuwa mtawala wenu, kwa sababu hamko chini ya sheria. Sasa mnaishi chini ya neema ya Mungu.
Watumwa wa Haki
15 Hivyo tufanye nini? Je, tutende dhambi kwa sababu tuko chini ya neema na siyo chini ya sheria? Hapana! 16 Hakika mnajua kuwa unakuwa mtumwa wa jambo lolote unaojitoa kulifanya. Chochote au yeyote unayemtii atakuwa bwana wako. Unaweza kufuata dhambi, au kumtii Mungu. Kufuata dhambi kunaleta kifo cha kiroho, lakini kumtii Mungu kunakufanya uhesabiwe na Mungu. 17 Hapo zamani mlikuwa watumwa wa dhambi na dhambi iliwatawala. Lakini ashukuriwe Mungu, mlitii kwa hiyari mafundisho yote aliyowaelekeza. 18 Mliwekwa huru kutoka katika dhambi, na sasa ninyi ni watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu. 19 Natumia dhana hii ya utumwa kutoka katika maisha ya kila siku kwa sababu mnahitaji msaada katika kuielewa kweli hii ya kiroho. Zamani mliitoa sehemu ya miili yenu kuwa watumwa wa mawazo yenu yaliyo machafu na maovu. Matokeo yake mliishi kwa ajili ya dhambi tu. Kwa njia hiyo hiyo, sasa mnapaswa kujitoa wenyewe kama watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu ili mweze kufaa kabisa kwa utumishi kwake.
20 Zamani mlikuwa watumwa wa dhambi, na wala hamkufikiri juu ya kutenda haki. 21 Mlifanya mambo maovu, na sasa mnaaibishwa kwa yale mliyotenda. Je, mambo haya yaliwasaidia? Hapana, yalileta kifo tu. 22 Lakini sasa mko huru dhidi ya dhambi. Mmekuwa watumwa wa Mungu, na mnaishi kwa ajili ya Mungu tu. Hili litawaletea uzima wa milele. 23 Watu wanapotenda dhambi, wanapokea malipo ya dhambi, ambayo ni kifo. Lakini Mungu huwapa watu wake zawadi ya bure, yaani uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
© 2017 Bible League International