M’Cheyne Bible Reading Plan
9 Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.”
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-13; Lk 9:28-36)
2 Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. 3 Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. 4 Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili.
5 Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” 6 Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu.
7 Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.”
8 Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake.
9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu.
10 Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” 11 Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?”
12 Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza[a] kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu[b] ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? 13 Lakini ninawaambia, Eliya amekuja,[c] na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa[d] kuhusu yeye.”
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-20; Lk 9:37-43a)
14 Wakati Yesu, Petro, Yakobo, na Yohana walipowafikia wanafunzi wengine, waliliona kundi kubwa la watu lililowazunguka na wakawaona walimu wa Sheria wakibishana nao. 15 Mara tu watu wote walipomwona Yesu, walishangazwa, na wakakimbia kwenda kumsalimia.
16 Akawauliza, “Mnabishana nao kitu gani?”
17 Na mtu mmoja kundini alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako ili umponye. Yeye amefungwa na pepo mbaya anayemfanya asiweze kuzungumza. 18 Na kila mara anapomshambulia humtupa chini ardhini. Naye hutokwa mapovu mdomoni na kusaga meno yake, huku akiwa mkakamavu. Nami niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze kutoka ndani yake, lakini hawakuweza.”
19 Kisha Yesu akajibu na kuwaambia, “ninyi kizazi kisichoamini, kwa muda gani niwe pamoja nanyi? Kwa muda gani nitapaswa kuchukuliana nanyi? Mleteni huyo mvulana kwangu.”
20 Wakamleta yule mvulana kwake. Na yule pepo alipomwona Yesu, kwa ghafula akamtingisha yule mvulana ambaye alianguka chini kwenye udongo, akivingirika na kutokwa povu mdomoni.
21 Yesu akamwuliza babaye, “Kwa muda gani amekuwa katika hali hii?”
Yule babaye akajibu akisema, “amekuwa katika hali hii tangu utoto. 22 Mara nyingi anamtupa katika moto ama katika maji ili kumwua. Lakini ikiwa unaweza kufanya kitu chochote, uwe na huruma na utusaidie.”
23 Yesu akamwambia, “Una maana gani kusema ‘ikiwa unaweza’? Kila kitu kinawezekana kwake yeye anayeamini.”
24 Mara, babaye yule mvulana alilia kwa sauti kubwa na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.”
25 Yesu alipoona lile kundi likizidi kuwa kubwa, alimkemea yule pepo mchafu na kumwambia, “Wewe pepo uliyemfanya mvulana huyu asiweze kusikia na asiweze kusema, nakuamuru, utoke ndani yake, na usimwingie tena!”
26 Na pepo yule alilia kwa sauti, akamtupa yule mvulana chini katika mishituko ya kutisha, kisha akatoka, naye akawa kama mtu aliyekufa, kiasi kwamba watu wengi wakadhani ya kuwa amekufa. 27 Lakini Yesu akamshika yule mvulana mikononi, na kumwinua naye akasimama.
28 Baada ya Yesu kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuuliza wakiwa peke yao, “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza pepo yule?”
29 Naye akawaambia, “Aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa maombi.”[e]
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Lk 9:43-45)
30 Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, 31 alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32 Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Lk 9:46-48)
33 Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je, mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” 34 Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi.
35 Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.”
36 Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, 37 “Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.”
Yeyote Ambaye Hayuko Kinyume Chetu Yuko Pamoja Nasi
(Lk 9:49-50)
38 Yohana akamwambia Yesu, “Mwalimu tulimwona mtu akifukuza pepo kwa jina lako. Nasi tulijaribu kumzuia, kwa sababu hakuwa mmoja wetu.”
39 Lakini Yesu akawaambia, “Msimzuie, kwa sababu hakuna atendaye miujiza kwa jina langu kisha mara baada ya hilo aseme maneno mabaya juu yangu. 40 Yeye ambaye hapingani na sisi basi yuko pamoja na sisi. 41 Yeyote anayewapa ninyi kikombe cha maji kwa sababu ninyi ni wake Kristo.[f] Hakika ninawaambia ukweli kwamba, hatapoteza thawabu yake.
Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi
(Mt 18:6-9; Lk 17:1-2)
42 Yeyote anayemsababisha mmoja wa hawa walio wadogo ambao wananiamini mimi kujikwaa na kuanguka, itakuwa bora kwake ikiwa atatupwa baharini huku amefungwa jiwe la kusagia shingoni mwake. 43 Ikiwa mkono wako unakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili na kuenda Jehanamu, ambako kuna moto usiozimika. 44 [g] 45 Na ikiwa mguu wako utakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa mlemavu kuliko kuwa na miguu miwili na kutupwa Jehanamu. 46 [h] 47 Na kama jicho lako litakusababisha ufanye dhambi, liondoe. Ni bora uingie katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kuwa nayo macho mawili na kutupwa Jehanamu, 48 ambapo waliomo watatafunwa na funza wasiokufa na kuchomwa na moto usiozimika kamwe.(A)
49 Kwa kuwa kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.[i]
50 Chumvi ni njema. Lakini ikiwa chumvi itaharibika, utawezaje kuifanya chumvi tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu na muishi kwa amani ninyi kwa ninyi.”
Mungu na Wayahudi
9 Nazungumza nayi sasa kama mmojawapo niliye wa Kristo. Hivyo mnaweza kuwa na uhakika kuwa sisemi uongo. Dhamiri yangu, inayotawaliwa na Roho Mtakatifu, inakubali kwamba ninayowaambia sasa ni kweli. 2 Nimejawa na huzuni na maumivu ya moyoni yasiyokwisha 3 kwa ajili ya watu wangu. Wao ni kaka na dada zangu katika mwili. Natamani ningeweza kuwasaidia. Ningekuwa tayari pia kuomba kupokea laana ya kutengwa na Kristo kama hiyo itaweza kuwasaidia. 4 Ni Waisraeli, watoto waliochaguliwa na Mungu. Wameushuhudia utukufu wa Mungu na wanashiriki maagano aliyofanya Mungu na watu wake. Mungu aliwapa Sheria ya Musa, ibada ya Hekalu, na ahadi zake. 5 Ni wazaliwa wa mababa zetu wakuu, na ni familia ya kidunia ya Masihi,[a] ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote. Yeye asifiwe milele![b] Amina.
6 Sina maana kuwa Mungu alishindwa kutimiza ahadi yake kwa Wayahudi. Lakini kwa hakika ni baadhi tu ya Waisraeli ndiyo watu wa Mungu[c]. 7 Na hivyo ni baadhi tu ya watoto wa Ibrahimu ndiyo wazaliwa wake halisi. Hivi ndivyo Mungu alimwambia Ibrahimu: “Wazaliwa wako halisi watakuwa wale waliotoka kwa Isaka.”(A) 8 Hii ina maana kuwa si watoto wote wa Ibrahimu walio watoto halisi wa Mungu. Wazaliwa halisi wa Ibrahamu ni wale wanaofanyika watoto wa Mungu kwa sababu ya agano ambalo Mungu alililiweka na Ibrahamu. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyosema katika agano hilo: “Wakati kama huu mwaka ujao nitakujia tena, na Sara mke wako atazaa mwana.”(B)
10 Na si hivyo tu. Kitu kama hicho kilimtokea Rebeka ambaye baada ya kupata mimba ya wana wawili mapacha waliotokana na baba mmoja, baba yetu Isaka. 11-12 Ndiyo, kabla ya kuzaliwa wana hao mapacha, Mungu alimwambia Rebeka, “Mwana mkubwa atamtumikia mdogo.”(C) Hii ilikuwa kabla wavulana hawa hawajatenda jambo lolote jema au baya. Mungu alisema hivi kabla hawajazaliwa ili kwamba mvulana ambaye Mungu alimtaka atachaguliwa kutokana na mpango wa Mungu mwenyewe. Mvulana huyu alichaguliwa kwa sababu ndiye ambaye Mungu alitaka kumwita, si kwa sababu ya jambo lolote walilofanya wavulana hao. 13 Kama Maandiko yanavyosema, “Nilimpenda Yakobo lakini nilimchukia Esau.”(D)
14 Namsikia mtu akiuliza, “Hivyo hii ina maana gani? Je, Mungu si mwenye haki?” Hapana! 15 Mungu alimwambia Musa, “Nitampa rehema yeyote ninayetaka kumpa rehema. Nitamhurumia yeyote ninayemchagua.”(E) 16 Hivyo Mungu atamchagua yeyote anayeamua kumpa rehema pasipo kujali watu wanataka nini ama kwa jinsi gani wanapiga mbio. 17 Katika Maandiko Mungu anamwambia Farao: “Nilikuweka uwe mfalme kwa kusudi hili hasa: kuonesha nguvu zangu kupitia kwako. Nilitaka jina langu litangazwe ulimwenguni kote”(F) 18 Hivyo Mungu huwarehemu wale anaotaka kuwarehemu na huwafanya jeuri wale anaotaka wawe jeuri.
19 Hivyo utaniuliza, “Ikiwa unayosema ni kweli, kwa nini Mungu amlaumu mtu yeyote kwa kufanya makosa? Hayupo anayeweza kukataa kufanya yale anayotaka Mungu, Je, yupo?” 20 Hilo si la kuuliza. Wewe ni mwanadamu tu na huna haki ya kumhoji Mungu. Chungu hakiwezi kumhoji aliyekifinyanga. Hakiwezi kusema, “Kwa nini ulinifinyanga hivi?” 21 Yeye aliyefinyanga chungu anaweza kufinyanga kitu chochote anachotaka. Anautumia udongo ule ule wa mfinyanzi kufinyanga vitu mbalimbali. Anaweza kufinyanga kitu kimoja kwa makusudi maalumu na kingine kwa matumizi ya kila siku.
22 Ni kwa jinsi hiyo hiyo Mungu amefanya. Alitaka kuionesha hasira yake na kuwafanya watu waone nguvu zake. Lakini kwa uvumilivu wake aliwastahimili wale waliomuudhi, watu waliokuwa tayari kuangamizwa. 23 Alingoja kwa uvumilivu ili aweze kuutangaza utajiri wa utukufu wake kwa watu aliowachagua wapokee rehema zake. Mungu alikwisha waandaa kuushiriki utukufu wake. 24 Sisi ndiyo watu hao, ambao Mungu alituchagua si tu kutoka kwa Wayahudi lakini pia kutoka kwa wale wasio Wayahudi. 25 Kama Mungu anavyosema katika kitabu cha Hosea,
“Watu wasiokuwa wangu,
nitasema ni watu wangu.
Na watu ambao sikuwapenda,
nitasema ni watu ninaowapenda.(G)
26 Na pale Mungu aliposema zamani:
‘Ninyi si watu wangu’;
hapo wataitwa watoto wa Mungu aliye hai.”(H)
27 Na Isaya huililia Israeli:
“Wako watu wengi sana wa Israeli,
kuliko mchanga ulio pwani ya baharini.
Lakini wachache wao watakaookolewa.
28 Ndiyo, Bwana atakamilisha kwa haraka
aliyosema atayafanya duniani.”(I)
29 Ni kama vile alivyosema Isaya:
“Ikiwa Bwana Mwenye Uweza wote
asingewaruhusu watu wachache wakaishi,
tungekuwa tumeangamizwa kabisa,
kama vile miji miovu ya Sodoma, na Gomora.”(J)
30 Hivyo haya yote yanamaanisha nini? Je, tunasema kwamba watu wasio Wayahudi walifanikiwa kukipata kibali cha Mungu, hata kama hawakuwa wakijaribu kukipata kibali hicho? Ndiyo. Walipata kibali hicho kwa sababu ya imani kwa Mungu. 31 Na vipi kuhusu watu wa Israeli? Wao walitaka kujipatia kibali cha Mungu kwa kuifuata sheria. Je, tunasema kuwa hawakufanikiwa? 32 Ndiyo, na sababu yake ni hii: Walijitahidi kukipata kwa kufanya kwa usahihi mambo yote yaliyoamriwa katika sheria badala ya kumtumaini Mungu. Walijikwaa kwenye jiwe linalowafanya watu waanguke. 33 Maandiko yanazungumza kuhusu jiwe hilo:
“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni litakalowafanya watu wajikwae.
Ni mwamba utakaowaangusha watu.
Lakini yeyote atakayemtumaini yeye
hataaibika kamwe.”(K)
© 2017 Bible League International