Book of Common Prayer
Kuja kwa Roho Mtakatifu
2 Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. 2 Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. 3 Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. 4 Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.
5 Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. 6 Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.
7 Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[a] 8 Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: 9 Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”
12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.
Petro Azungumza na Watu
14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:
17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
Vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
yangu kwa watumishi wangu,
wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
Nitasababisha ishara chini duniani.
Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[b] ataokolewa.(A)
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mk 16:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)
28 Alfajiri mapema siku iliyofuata baada ya siku ya Sabato, yaani siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu alikwenda kuliangalia kaburi.
2 Ghafla malaika wa Bwana akaja kutoka mbinguni, na tetemeko kubwa likatokea. Malaika alikwenda kaburini na kulivingirisha jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi. Kisha akaketi juu ya jiwe. 3 Malaika alikuwa anang'aa kama miali ya radi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 Askari waliokuwa wanalinda kaburi walimwogopa sana malaika, walitetemeka kwa woga na wakawa kama watu waliokufa.
5 Malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope. Ninajua mnamtafuta Yesu, aliyeuawa msalabani. 6 Lakini hayupo hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu, kama alivyosema. Njooni mwone mahali ulipokuwa mwili wake. 7 Nendeni haraka mkawaambie wafuasi wake, ‘Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Amekwenda Galilaya na atafika huko kabla yenu. Na mtamwona huko.’” Kisha malaika akasema, “Sasa nimewaambia.”
8 Hivyo wanawake wakaondoka haraka kaburini. Waliogopa sana, lakini walijawa na furaha. Walipokuwa wanakimbia kwenda kuwaambia wafuasi wake kilichotokea, 9 ghafla Yesu alisimama mbele yao. Akasema, “Salamu!” Wanawake wakamwendea wakamshika miguu na wakamwabudu. 10 Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie wafuasi wangu[a] waende Galilaya, wataniona huko.”
© 2017 Bible League International