Book of Common Prayer
Petro akiwa Lida na Yafa
32 Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini[a] walioishi Lida. 33 Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. 35 Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana.
36 Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.[b] Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37 Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38 Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39 Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41 Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42 Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43 Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu
60 Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?”
61 Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je, fundisho hili ni tatizo kwenu? 62 Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? 63 Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” 64 Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) 65 Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’”
66 Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata.
67 Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. 69 Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.”
70 Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” 71 Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake.
© 2017 Bible League International