Book of Common Prayer
Nani anaweza kukifungua kitabu?
5 Kisha niliona kitabu[a] katika mkono wa kulia wa aliyekaa kwenye kiti cha enzi. Kitabu hiki kilikuwa na maandishi pande zote na kilikuwa kimefungwa kwa mihuri saba. 2 Na nikamwona malaika mwenye nguvu, aliyeita kwa sauti kubwa, “Ni nani anayestahili kuivunja mihuri na kukifungua kitabu?” 3 Lakini hakukuwa yeyote mbinguni au duniani au chini ya dunia ambaye angeweza kukifungua kitabu na kutazama ndani yake. 4 Nililia sana kwa sababu hakuwepo aliyestahili kukifungua kitabu na kuangalia ndani yake. 5 Lakini mmoja wa wazee akaniambia, “Usilie! Simba[b] kutoka kabila la Yuda ameshinda. Ni mzaliwa wa Daudi. Anaweza kukifungua kitabu na mihuri yake saba.”
6 Kisha nikamwona Mwanakondoo amesimama katikati karibu na kiti cha enzi kilichozungukwa na viumbe wanne wenye uhai. Wazee pia walikuwa wamemzunguka Mwanakondoo aliyeonekana kama aliyeuawa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambayo ni roho saba za Mungu zilizotumwa ulimwenguni kote. 7 Mwanakondoo alikuja na akakichukua kile kitabu kutoka katika mkono wa kulia wa yule aliyeketi kwenye kiti enzi. 8 Baada ya Mwanakondoo kukichukua kile kitabu, viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na wanne wakainama mbele za Mwanakondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi. Pia walikuwa wameshikilia bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni maombi ya watu watakatifu wa Mungu. 9 Na wote walimwimbia wimbo mpya Mwanakondoo:
“Unastahili kukichukua kitabu
na kuifungua mihuri yake,
kwa sababu uliuawa,
na kwa sadaka ya damu yako uliwanunua watu kwa ajili ya Mungu,
kutoka kila kabila, lugha, rangi na taifa.
10 Uliwafanya kuwa ufalme na makuhani kwa ajili ya Mungu wetu.
Nao watatawala duniani.”
11 Kisha, nilipotazama, nikasikia sauti ya malaika wengi waliozunguka kiti cha enzi pamoja na viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne. Walikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika, elfu kumi mara elfu kumi. 12 Kwa sauti kuu malaika walisema:
“Mamlaka yote, utajiri, hekima na nguvu ni kwa Mwanakondoo aliyeuawa.
Anastahili kupokea heshima, utukufu na sifa!”
13 Ndipo nikasikia kila kiumbe kilichoumbwa kilichoko mbinguni na duniani na chini ya dunia na baharini, viumbe vyote sehemu hizo vikisema:
“Sifa zote na heshima
na utukufu na nguvu kuu ni kwa ajili yake Yeye aketiye
kwenye kiti cha enzi na kwa Mwanakondoo milele na milele!”
14 Viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amina!” Na wazee wakainama chini wakasujudu.
Mafundisho ya Yesu Mlimani
(Lk 6:20-23)
5 Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda kwenye kilima na kukaa chini. Wanafunzi wake walimjia Yesu. 2 Kisha Yesu akaanza kuwafundisha watu kwa akasema:
3 “Heri[a] kwa walio maskini na wenye kujua kwamba wanamhitaji Mungu.[b]
Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao.
4 Heri kwa wenye huzuni sasa.
Kwa kuwa watafarijiwa na Mungu.
5 Heri kwa walio wapole.
Kwa kuwa watairithi nchi.[c]
6 Heri kwa wenye kiu na njaa ya kutenda haki.[d]
Kwa kuwa Mungu ataikidhi kiu na njaa yao.
7 Heri kwa wanaowahurumia wengine.
Kwa kuwa watahurumiwa pia.
8 Heri kwa wenye moyo safi,[e]
Kwa kuwa watamwona Mungu.
9 Heri kwa wanaotafuta amani.[f]
Kwa kuwa wataitwa watoto wa Mungu.
10 Heri kwa wanaoteswa kwa sababu ya kutenda haki.
Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao.
11 Heri kwenu ninyi pale watu watakapowatukana na kuwatesa. Watakapodanganya na akasema kila neno baya juu yenu kwa kuwa mnanifuata mimi. 12 Furahini na kushangilia kwa sababu thawabu kuu inawasubiri mbinguni. Furahini kwa kuwa ninyi ni kama manabii walioishi zamani. Watu waliwatendea wao mambo mabaya kama haya pia.
© 2017 Bible League International