Book of Common Prayer
Mkutano Yerusalemu
15 Kisha baadhi ya watu kutoka Uyahudi wakaja Antiokia na kuanza kuwafundisha jamii ya waamini wasio Wayahudi, wakisema, “Hamwezi kuokolewa ikiwa hamkutahiriwa kama Musa alivyotufundisha.” 2 Paulo na Barnaba wakayapinga mafundisho haya na wakahojiana na kubishana na watu hawa juu ya hili. Hivyo kundi la waamini likaamua kuwatuma Paulo, Barnaba, na baadhi ya watu wengine Yerusalemu ili kujadiliana na mitume na wazee kuhusu suala hili.
3 Kanisa liliwapa wale waliotumwa kila kitu walichohitaji kwa ajili ya safari yao. Walisafiri kupitia maeneo ya Foeniki na Samaria, ambako walieleza kwa undani mambo yote namna ambavyo wasio Wayahudi wamemgeukia Mungu wa kweli. Habari hii iliwafurahisha waamini wote. 4 Walipofika Yerusalemu, mitume, wazee na kanisa lote waliwakaribisha. Paulo, Barnaba, na wengine wakaeleza yote ambayo Mungu alitenda kupitia wao. 5 Baadhi ya waamini mjini Yerusalemu waliokuwa Mafarisayo,[a] walisimama na kusema, “Waamini wasio Wayahudi lazima watahiriwe. Ni lazima tuwaambie waitii Sheria ya Musa!”
6 Ndipo mitume na wazee wakakusanyika kulichunguza jambo hili. 7 Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Petro akasimama na kuwaambia, “Ndugu zangu, nina uhakika mnakumbuka kilichotokea siku za nyuma. Mungu alinichagua kutoka miongoni mwenu kuzihubiri Habari Njema kwa watu wasio Wayahudi. Kupitia mimi walisikia Habari Njema na kuamini. 8 Mungu anamfahamu kila mtu, hata mawazo yao, na amewakubali watu hawa wasio Wayahudi. Amelionyesha hili kwetu kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. 9 Mbele za Mungu, wasio Wayahudi hawako tofauti na sisi. Mungu aliisafisha mioyo yao walipoamini. 10 Kwa nini sasa mnawatwisha mzigo mzito kwenye shingo zao? Je, mnajaribu kumkasirisha Mungu? Sisi na baba zetu hatukuweza kuubeba mzigo huo. 11 Hapana, tunaamini kuwa sisi na watu hawa tutaokolewa kwa namna moja iliyo sawa, ni kwa neema ya Bwana Yesu.”
Yesu Akiwa Bethania
17 Yesu akaenda Bethania na huko akakuta Lazaro amekufa na kuwa kaburini kwa siku nne. 18 Mji wa Bethania ulikuwa kama kilomita tatu[a] kutoka Yerusalemu. 19 Wayahudi wengi wakaja ili kuwaona Martha na Mariamu. Walikuja ili kuwafariji kwa ajili ya msiba wa kaka yao, Lazaro.
20 Martha aliposikia kuwa Yesu alikuwa anakuja, alikwenda kumpokea. Lakini Mariamu alibaki nyumbani. 21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwepo hapa, ndugu yangu asingelikufa. 22 Lakini najua kwamba hata sasa Mungu atakupa chochote utakachomwomba.”
23 Yesu akasema, “Kaka yako atafufuka na kuwa hai tena.”
24 Martha akajibu, “Ninajua kuwa atafufuka tena wakati wa ufufuo siku ya mwisho.”
25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo. Mimi ndiye uzima. Kila anayeniamini atakuwa na uzima, hata kama atakufa. 26 Kila atakayeniamini hatakufa kiroho hata kama atakufa kimwili. Je, Martha, unaliamini jambo hili?”
27 Martha akajibu, “Ndiyo Bwana naliamini. Nakuamini kwamba wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu. Ndiwe unayekuja ulimwenguni.”
Yesu Alia
28 Baada ya Martha kusema maneno haya, alirejea kwa Mariamu dada yake. Aliongea naye peke yake na kusema, “Mwalimu yupo hapa. Anakutafuta.” 29 Mariamu aliposikia hivyo, aliinuka na kwenda haraka kwa Yesu.
© 2017 Bible League International