Book of Common Prayer
26 Ndugu zangu, wana katika familia ya Ibrahimu na ninyi watu wengine ambao pia mnamwabudu Mungu wa kweli, sikilizeni! Habari kuhusu wokovu huu imeletwa kwetu. 27 Wayahudi waishio Yerusalemu na viongozi wao hawakutambua kuwa Yesu ni Mwokozi. Maneno ambayo manabii waliandika kuhusu yeye yalikuwa yakisomwa kila siku ya Sabato, lakini hawakuyaelewa. Walimhukumu Yesu. Walipofanya hivi, waliyatimiliza maneno ya manabii. 28 Hawakupata sababu ya msingi kwa nini Yesu afe, lakini walimwomba Pilato amwue.
29 Wayahudi hawa walimtendea Yesu mambo yote mabaya ambayo Maandiko yalisema yangempata Yesu. Kisha walimteremsha Yesu kutoka msalabani na kumweka kaburini. 30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu! 31 Baada ya hili, kwa siku nyingi, wale waliofuatana na Yesu kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu walimwona. Wao sasa ni mashahidi wake kwa watu wetu.
32 Tunawahubiri Habari Njema kuhusu ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 33 Sisi ni wazao wao, na Mungu ameitimiza ahadi hii kwa ajili yetu. Mungu aliitimiza ahadi hii kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Tunasoma pia kuhusu hili katika Zaburi 2:
‘Wewe ni Mwanangu.
Leo nimekuwa baba yako.’(A)
34 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu hatarudi kaburini na kuwa mavumbi. Hivyo Mungu alisema,
‘Nitawapa ahadi ya kuaminiwa na
takatifu niliyoiahidi kwa Daudi.’(B)
35 Lakini Zaburi nyingine inasema,
‘Hautaruhusu Mtakatifu wako aoze kaburini.’(C)
36 Daudi aliyatenda mapenzi ya Mungu alipokuwa hai. Kisha alikufa na kuzikwa kama baba zake wote. Na mwili wake ulioza kaburini! 37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuoza kaburini. 38-39 Ndugu zangu, eleweni yale tunayowaambia. Mnaweza kupata msamaha wa dhambi kupitia huyu Yesu. Sheria ya Musa haikuwatoa kutoka katika dhambi zenu. Lakini mnaweza kuwa huru mbali na hukumu. 40 Hivyo iweni waangalifu! Msiruhusu walichosema manabii kikawatokea ninyi:
41 ‘Sikilizeni enyi watu wenye mashaka!
Mnaweza kushangaa,
lakini sasa nendeni na mfe.
Kwa sababu kipindi cha wakati wenu,
nitafanya kitu ambacho hamtaamini.
Hata kama kitafafanuliwa kwenu!’”(D)
42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanaondoka kwenye sinagogi, watu waliwaomba warudi tena Sabato inayofuata ili wawaeleze zaidi kuhusu mambo haya. 43 Baada ya mkutano, watu wengi, Wayahudi na wale waliobadili dini zao na kufuata dini ya Kiyahudi, waliwafuata Paulo na Barnaba; nao waliwatia moyo watu hawa waendelee kuitumaini neema ya Mungu.
Mchungaji na Kondoo Wake
10 Yesu akawaambia, “Hakika ninawaambia, mtu anapoingia katika zizi la kondoo, hutumia mlango. Kama akiingia kwa kutumia njia nyingine yoyote, huyo ni mwizi. Anajaribu kuwaiba kondoo. 2 Lakini mtu anayewachunga kondoo hupitia mlangoni. Yeye ndiye mchungaji. 3 Mtu anayelinda mlangoni humfungulia mlango mchungaji. Na kondoo huisikiliza sauti ya mchungaji wao. Naye huwaita kondoo wake mwenyewe kwa majina yao, na huwaongoza kwenda nje. 4 Mchungaji huwatoa nje kondoo wake wote. Kisha huwatangulia mbele na kuwaongoza. Kondoo nao humfuata, kwa sababu wanaifahamu sauti yake. 5 Lakini kamwe kondoo hawatamfuata wasiyemfahamu. Bali watamkimbia, kwa sababu hawaifahamu sauti yake.”
6 Yesu aliwaambia watu habari hii, lakini hawakuelewa ilikuwa ina maana gani.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. 18 Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.”
© 2017 Bible League International