Book of Common Prayer
Msiwafuate Maadui wa Kristo
18 Wapendwa wanangu, mwisho umekaribia! Mmesikia kuwa adui wa Kristo anakuja. Na sasa maadui wengi wa Kristo tayari wapo hapa. Hivyo tunajua kwamba mwisho umekaribia. 19 Maadui hawa walikuwa miongoni mwetu, lakini walituacha. Hawakuwa wenzetu hasa. Kama wangelikuwa kweli wenzetu, wangebaki pamoja nasi. Lakini walituacha. Hii inaonesha kuwa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa kwa hakika mwenzetu.
20 Mnayo karama[a] aliyowapa Yeye Aliye Mtakatifu.[b] Hivyo nyote mnaijua kweli. 21 Mnadhani ninawaandikia waraka huu kwa sababu hamuijui kweli? Hapana! Ninawaandikia kwa sababu mnaijua kweli. Na mnajua kuwa hakuna uongo utokao katika kweli.
22 Ni nani basi aliye mwongo? Ni yeye anayesema kuwa Yesu siyo Kristo. Yeyote anayesema hivyo ni adui wa Kristo. Yeye huyo asiyemwamini Baba wala Mwana. 23 Yeyote asiyemwamini Mwana hana Baba, ila yeye anayemkubali Mwana anaye Baba pia.
24 Mnapaswa kuendelea kuyafuata mafundisho mliyoyasikia tangu mwanzo. Kama mkifanya hivyo, mtakuwa siku zote katika Mwana na katika Baba. 25 Na hili ndilo ambalo Mwana ameliahidi kwetu sisi, uzima wa milele.
26 Ninawaandikia barua hii juu ya wale ambao wanataka kuwapotosha katika njia isiyo sahihi. 27 Kristo aliwapa karama maalumu.[c] Nanyi bado mngali na karama hiyo ndani yenu. Hivyo hamumhitaji yeyote kuwafundisha. Karama aliyowapa inawafundisha juu ya kila jambo. Ni karama ya kweli, si ya uongo. Hivyo endeleeni kuishi katika Kristo, kama karama yake ilivyowafundisha.
28 Ndiyo, wanangu wapendwa, ishini ndani yake. Kama tukifanya hivyo, hatutakuwa na hofu siku kristo atakapo kuja tena. Hatutahitaji kujificha na kuwa na aibu ajapo. 29 Mnajua ya kwamba daima Kristo alifanya yaliyo ya haki. Vivyo hivyo mnajua pia ya kwamba wote watendao haki ni watoto wa Mungu.
Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu
(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Yh 1:19-28)
3 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo:
Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi;
Herode alikuwa mtawala wa Galilaya;
Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti;
na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene.
2 Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. 3 Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. 4 Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema,
“Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
nyoosheni njia kwa ajili yake.
5 Kila bonde litajazwa,
na kila mlima na kilima vitasawazishwa.
Barabara zilizopinda zitanyooshwa,
na barabara zenye mashimo zitasawazishwa.
6 Na kila mtu ataona
jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’”(A)
7 Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? 8 Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! 9 Na sasa shoka liko tayari kukata miti,[a] kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”
10 Watu wakamwuliza Yohana, “Tufanye nini?”
11 Akajibu, “Ukiwa na mashati mawili mpe moja asiyekuwa na shati. Kama una chakula, kigawe pia.”
12 Hata watoza ushuru walikuja kwa Yohana. Walitaka wabatizwe. Walimwambia, “Mwalimu, tufanye nini sisi?”
13 Akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi kuliko kiwango kilichoamriwa.”
14 Askari wakamwuliza, “Vipi kuhusu sisi? Tufanye nini?”
Akawaambia, “Msitumie nguvu au kutengeneza mashtaka ya uongo ili watu wawape pesa. Mtosheke na mishahara mnayopata.”
© 2017 Bible League International