Book of Common Prayer
10 Manabii waliotabiri juu ya neema ambayo ingeoneshwa kwenu, walipeleleza kwa makini na kwa uangalifu wakaulizia habari za wokovu huu. 11 Roho wa Kristo alikuwa ndani yao, naye aliwapa ushuhuda mapema kuhusu Kristo kwamba itamlazimu kuteswa na baada ya hapo atapokea utukufu. Manabii waliuliza kutaka kujua wakati gani na katika mazingira gani mambo haya yangetokea.
12 Ilifunuliwa kwao kwamba walikuwa hawajitumikii wenyewe. Badala yake, waliwatumikia ninyi walipotabiri juu ya mambo haya. Na sasa mmesikia juu ya mambo haya kutoka kwa wale waliyowaambia habari Njema kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wangetamani sana kufahamu zaidi juu ya mambo haya mliyoambiwa.
Mwito Kwa Maisha Matakatifu
13 Hivyo mkeshe katika fahamu zenu na kuwa na kiasi. Yawekeni kikamilifu matumaini yenu katika baraka mtakazopewa wakati Yesu Kristo atakapofunuliwa. 14 Kama watoto watiifu, msiyaache maisha yenu yandelee kutawaliwa na tamaa mbaya mlizokuwa nazo awali mlipokuwa wajinga. 15 Badala yake, kama ambavyo yeye Mungu aliyewaita alivyo mtakatifu, hata ninyi muwe watakatifu katika kila mnalotenda. 16 Hivyo Maandiko yanasema: “Iweni watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu.”(A)
17 Na kama Baba mnayemwita Mungu anayewahukumu watu bila upendeleo kwa kadri ya matendo ya kila mtu, muishi maisha ya utauwa na hofu kwa Mungu katika miaka yenu ya kukaa humu duniani kama wageni. 18 Mnajua kwamba siyo kwa mambo yaharibikayo kama fedha au dhahabu, kwamba mliokolewa kutoka katika maisha yasiyofaa mliyoyapokea kutoka kwa babu zenu, 19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, kama ile ya mwanakondoo asiye na dosari wala ila. 20 Kristo alichaguliwa kabla ya uumbaji wa ulimwengu, lakini alidhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.
Yesu Asema Petro Atamkana
(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Lk 22:31-34)
36 Simoni Petro akamwuliza Yesu, “Bwana, unaenda wapi?”
Yesu akajibu, “Kule niendako hamwezi kunifuata sasa. Lakini mtanifuata baadaye.”
37 Petro akauliza, “Bwana, kwa nini nisikufuate sasa? Mimi niko radhi kufa kwa ajili yako!”
38 Yesu akajibu, “Je, ni kweli utayatoa maisha yako kwa ajili yangu? Hakika nakwambia, kabla jogoo hajawika, utasema mara tatu kwamba hunijui mimi.”
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Lk 23:50-56)
38 Baadaye, mtu mmoja aliyeitwa Yusufu wa kutoka Arimathaya akamwomba Pilato mwili wa Yesu. (Yusufu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini hakumweleza mtu yeyote, kwa sababu aliwaogopa viongozi wa Kiyahudi.) Pilato akasema Yusufu anaweza kuuchukua mwili wa Yesu, hivyo naye akaja na kuuchukua.
39 Nikodemu akaenda pamoja na Yusufu. Nikodemu, alikuwa ni yule mtu aliyekuja kwa Yesu hapo kabla na kuzungumza naye usiku. Huyu alileta kadiri ya lita[a] mia moja ya marashi yenye mchanganyiko wa manemane na uvumba. 40 Watu hawa wawili wakauchukua mwili wa Yesu na wakauzungushia vipande vya sanda ya kitani pamoja na marashi yale. (Hivi ndivyo Wayahudi walivyowazika watu.) 41 Pale msalabani sehemu alipouawa Yesu, palikuwepo na bustani. Katika bustani ile palikuwemo na kaburi[b] jipya la kuzikia. Hakuna mtu aliyewahi kuzikwa ndani ya kaburi lile. 42 Wanaume wakauweka mwili wa Yesu katika kaburi lile kwa kuwa lilikuwa karibu, na Wayahudi walikuwa wakijiandaa kuianza siku yao ya Sabato.
© 2017 Bible League International