Book of Common Prayer
13 Viongozi wa Kiyahudi walijua kuwa Petro na Yohana walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu yo yote. Lakini walikuwa wanazungumza kwa ujasiri bila woga; viongozi walishangaa. Walitambua pia kuwa Petro na Yohana walikuwa pamoja na Yesu. 14 Walimwona aliyeponywa akiwa amesimama kwa miguu yake mwenyewe pembeni mwa mitume. Na hivyo walishindwa kuzungumza chochote kilicho kinyume na mitume.
15 Viongozi wa Kiyahudi wakawaambia mitume watoke nje ya chumba cha mkutano wa baraza. Kisha viongozi wakajadiliana wao wenyewe juu ya nini wanachopaswa kufanya. 16 Wakaulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Kila mtu katika Yerusalemu anajua kuhusu muujiza walioufanya kama ishara kutoka kwa Mungu. Ni dhahiri, hatuwezi kusema muujiza huo haukufanyika. 17 Lakini ni lazima tuwatishe ili wasiendelee kuwaambia watu kutumia jina lile.[a] Ili tatizo hili lisisambae miongoni mwa watu.”
18 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaita Petro na Yohana ndani tena. Wakawaambia wasiseme wala kufundisha kitu chochote kwa kutumia jina la Yesu. 19 Lakini Petro na Yohana wakawajibu, “Mnadhani kipi ni sahihi? Mungu angetaka nini? Je, tunapaswa kuwatii ninyi au tumtii Mungu? 20 Hatuwezi kukaa kimya. Ni lazima tuwaambie watu kuhusu yale tuliyoona na kusikia.”
21-22 Viongozi wa Kiyahudi hawakupata sababu za kuwaadhibu mitume, kwa sababu watu wote walikuwa wanamsifu Mungu kwa kile kilichotendeka. Muujiza huu ulikuwa ishara kutoka kwa Mungu. Mtu aliyeponywa alikuwa na miaka zaidi ya arobaini. Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaonya mitume tena na kuwaacha waende wakiwa huru.
Petro na Yohana Warudi kwa Waamini
23 Petro na Yohana waliondoka kwenye mkutano wa viongozi wa Kiyahudi na kurudi kwa waamini wenzao. Wakalieleza kundi la waamini kila kitu walichoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 24 Waamini waliposikia hili, wote kwa pamoja wakamwomba Mungu wakiwa na nia moja. Wakasema, “Bwana wa wote, wewe ndiye uliyeumba mbingu, dunia, bahari na kila kitu ulimwenguni. 25 Baba yetu Daudi alikuwa mtumishi wako. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliandika maneno haya:
‘Kwa nini mataifa yanatenda kwa kiburi?
Kwa nini watu wanapanga mipango isiyofaa kama hii?
26 Wafalme wa dunia hujiandaa kwa mapigano,
na watawala hukusanyika pamoja kinyume na Bwana
na kinyume na Masihi wake.’(A)
27 Ndicho hasa kilichotokea wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa mengine na watu wa Israeli walipokusanyika pamoja hapa Yerusalemu wakawa kinyume na Yesu; Masihi, Mtumishi wako mtakatifu. 28 Watu hawa waliokusanyika pamoja kinyume na Yesu waliwezesha mpango wako kukamilika. Ilifanyika kwa sababu ya nguvu zako na matakwa yako. 29 Na sasa, Bwana, sikiliza wanayosema. Wanajaribu kututisha. Sisi ni watumishi wako. Tusaidie ili tuseme yale unayotaka tuseme bila kuogopa. 30 Tusaidie, ili tuwe jasiri kwa kutuonesha nguvu zako. Ponya Wagonjwa. Fanya ishara na maajabu kutokea kwa mamlaka[b] ya Yesu mtumishi wako mtakatifu.”
31 Baada ya waamini kuomba, mahali walipokuwa palitikisika. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaendelea kuhubiri Habari Njema bila woga.
Huzuni Itageuzwa Kuwa Furaha
16 Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kingine kifupi mtaniona tena.”
17 Baadhi ya wafuasi wake wakaambiana wao kwa wao, “Ana maana gani anaposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona tena. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena?’ Tena ana maana gani anaposema, ‘Kwa sababu naenda kwa Baba’?” 18 Wakauliza pia, “Ana maana gani anaposema ‘Kipindi kifupi’? Sisi hatuelewi anayosema.” 19 Yesu alitambua kuwa wafuasi wake walitaka kumwuliza juu ya jambo hilo. Hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana ninyi kwa ninyi kwamba nilikuwa na maana gani niliposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena’? 20 Hakika nawaambia, ninyi mtapata huzuni na kulia, bali ulimwengu utakuwa na furaha. Ndio, mtapata huzuni, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21 Mwanamke anapojifungua mtoto, hupata maumivu, kwa sababu wakati wake umefika. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, huyasahau maumivu yale. Husahau kwa sababu huwa na furaha kwa kuwa mtoto amezaliwa ulimwenguni. 22 Ndivyo ilivyo hata kwenu pia. Sasa mna huzuni lakini nitawaona tena, nanyi mtafurahi. Mtakuwa na furaha ambayo hakuna mtu atakayewaondolea. 23 Katika siku hiyo, hamtapaswa kuniuliza mimi kitu chochote. Nami kwa hakika nawaambia, Baba yangu atawapa lo lote mtakalomwomba kwa jina langu. 24 Hamjawahi kuomba lo lote kwa namna hii hapo awali. Bali ombeni kwa jina langu nanyi mtapewa. Kisha mtakuwa na furaha iliyotimia ndani yenu.
Ushindi Dhidi ya Ulimwengu
25 Nimewaambia mambo haya kwa kutumia maneno yenye mafumbo. Isipokuwa utakuja wakati ambapo sitatumia tena maneno ya jinsi hiyo kuwaeleza mambo. Nami nitasema nanyi kwa maneno ya wazi wazi juu ya Baba. 26 Kisha, mtaweza kumwomba Baba vitu kwa jina langu. Sisemi kwamba nitapaswa kumwomba Baba kwa ajili yenu. 27 Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu ninyi mmenipenda mimi. Naye anawapenda kwa sababu mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28 Mimi nimetoka kwa Baba kuja ulimwenguni. Sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
29 Kisha wafuasi wake wakasema, “Tayari unaongea nasi wazi wazi. Hutumii tena maneno yanayoficha maana. 30 Sasa tunatambua kuwa unajua mambo yote. Wewe unajibu maswali yetu hata kabla hatujayauliza. Hii inatufanya tuamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
31 Yesu akasema, “Kwa hiyo sasa mnaamini? 32 Basi nisikilizeni! Wakati unakuja mtakapotawanywa, kila mmoja nyumbani kwake. Kwa hakika, wakati huo tayari umekwisha fika. Ninyi mtaniacha, nami nitabaki peke yangu. Lakini kamwe mimi siko peke yangu, kwa sababu Baba yupo pamoja nami.
33 Nimewaambia mambo haya ili muwe na amani ndani yangu. Katika ulimwengu huu mtapata mateso. Lakini muwe jasiri! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
© 2017 Bible League International