Book of Common Prayer
11 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Na ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu, ataifanya hai tena miili yenu inayokufa. Ndiyo, Mungu ndiye aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu, naye atawafufua ninyi na kuwapa uzima kupitia Roho wake anayeishi ndani yenu.
12 Hivyo, kaka na dada zangu, ni lazima tusitawaliwe na udhaifu wa kibinadamu kwa kufuata tamaa zake. 13 Ikiwa mtayatumia maisha yenu kufanya yale ambayo udhaifu wenu wa kibinadamu unataka, mtakufa kiroho. Lakini ikiwa mtaupokea msaada wa Roho na mkaacha kutenda mambo mabaya mnayotenda na miili yenu, mtakuwa na uzima wa kweli.
14 Watoto wa kweli wa Mungu ni wale wanaokubali kuongozwa na Roho wa Mungu. 15 Roho tuliyempokea si roho anayetufanya kuwa watumwa tena na kutusababisha tuwe na hofu. Roho tuliye naye hutufanya tuwe watoto waliochaguliwa na Mungu. Na kwa Roho huyo twalia “Aba,[a] yaani Baba.” 16 Na Roho mwenyewe huzungumza na roho zetu na kutuhakikishia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. 17 Nasi kwa kuwa ni watoto wa Mungu, basi sisi ni warithi, warithi wa Mungu na warithi pamoja na Kristo. Mungu atatupa yale yote aliyompa Kristo. Sisi tunaoteseka sasa kama Kristo alivyoteseka tutashiriki katika utukufu wake.
Wakati Wetu wa Utukufu Unakuja
18 Nanayachukulia mateso ya sasa kuwa si kitu ukilinganisha na utukufu mkuu tunaoutarajia. 19 Hata uumbaji una shauku kuu, ukisubiri kwa hamu wakati ambapo atawadhihirisha “watoto halisi wa Mungu”[b] kuwa ni na. 20 Kila alichokiumba Mungu kiliruhusiwa kuwa na mapungufu kana kwamba hakitafikia utimilifu wake. Hilo halikuwa kwa matakwa ya viumbe, lakini Mungu aliruhusu hayo yatokee kwa mtazamo wa tumaini hili: 21 kwamba uumbaji ungewekwa huru mbali na uharibifu, na kwamba kila alichokiumba Mungu kiwe na uhuru na utukufu ule ule ulio wa watoto wa Mungu.
22 Tunajua kuwa kila kitu alichoumba Mungu kimekuwa kikingoja hadi sasa katika kuugua na uchungu kama wa mwanamke aliye tayari kuzaa mtoto. 23 Siyo uumbaji tu, bali sisi pia tumekuwa tukingoja kwa kuugua na uchungu ndani yetu. Tunaye Roho kama sehemu ya kwanza ya ahadi ya Mungu. Kwa hiyo tunamngoja Mungu amalize kutufanya sisi watoto wake yeye mwenyewe. Nina maana kuwa tunasubiri kuwekwa huru kwa miili yetu. 24 Tuliokolewa ili tuwe na tumaini hili. Ikiwa tunaweza kuona kile tunachokisubiri, basi hilo siyo tumaini la kweli. Watu hawatumaini kitu ambacho tayari wanacho. 25 Lakini tunatumaini kitu tusichokuwa nacho, na hivyo tunakisubiri kwa uvumilivu.
27 Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.”
28 Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?”
29 Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.”
30 Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? 31 Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”(A)
32 Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33 Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34 Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.”
35 Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna ajaye kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. 36 Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya,[a] lakini bado hamuniamini. 37 Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. 38 Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. 39 Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. 40 Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.”
© 2017 Bible League International