Book of Common Prayer
16 Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. 17 Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe.
18 Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. 19 Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.”(A) 20 Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.”(B) 21 Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: 22 Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. 23 Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu
(Mt 9:9-13; Lk 5:27-32)
13 Mara nyingine tena Yesu akaelekea kandoni mwa ziwa, na watu wengi walikuwa wakimwendea, naye akawafundisha. 14 Alipokuwa akitembea kando ya ufukwe wa ziwa, alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi katika mahala pake pa kukusanyia kodi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Hivyo Lawi akainuka na kumfuata.
15 Baadaye Yesu na wafuasi wake wa karibu walikuwa wakila chakula cha jioni nyumbani kwa Lawi. Wakusanya kodi wengi na watu wengine wenye sifa mbaya nao wakamfuata Yesu. Hivyo wengi wao walikuwa wakila pamoja na Yesu na wanafunzi wake. 16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa pamoja na Mafarisayo walipomwona Yesu akila na wenye dhambi na wanaokusanya kodi, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Yesu anakula na wenye kukusanya kodi na watu wengine wenye dhambi?”
17 Yesu alipolisikia hili akawaambia, “Wale walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari si wale walio wazima wa afya. Mimi nimekuja kuwakaribisha wenye dhambi waje kwangu sikuja kwa ajili ya wale wanaotenda kila kitu kwa haki.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mt 9:14-17; Lk 5:33-39)
18 Siku moja wafuasi wa Yohana Mbatizaji na Mafarisayo walikuwa wanafunga. Baadhi ya watu walimjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wafuasi wa Yohana na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini kwa nini wanafunzi wako hawafungi.”
19 Yesu akawajibu, “Katika sherehe ya arusi hutarajii marafiki wa bwana arusi wawe na huzuni wakati yeye mwenyewe yupo pamoja nao. Hakika hawatafunga ikiwa bwana arusi bado yuko pamoja nao. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, na wakati huo ndipo watakapofunga.
21 Hakuna anayeshona kiraka kipya cha nguo kwenye vazi la zamani. Ikiwa atafanya hivyo kiraka hicho kipya kitajikunjakunja na kulinyofoa vazi hilo zee nalo litachanika vibaya zaidi. 22 Vivyo hivyo hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vya zamani[a] vilivyozeeka. Akifanya hivyo, divai ile itachacha na hewa yake itavipasua vibuyu hivyo vya ngozi na kuviharibu kabisa pamoja na divai yenyewe. Badala yake mtu anaweka divai mpya ndani ya vibuyu vipya vya ngozi vya kuwekea divai.”
© 2017 Bible League International